Matukio ya hivi karibuni ya nchini Sudan yanatukumbusha umuhimu mkubwa wa dhana ya kung’atuka, neno la Kizanaki lililoingia kwenye msamiati wa lugha ya Kiswahili na ambalo husikika pia kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.

Raia wa Sudan wamekuwa kwenye kipindi cha miezi kadhaa ya maandamano ya kushinikiza serikali yao kuachia madaraka na kuanzisha mchakato wa kurudisha utawala wa kiraia.

Maandamano ya sasa ambayo bado yanaendelea yalianza Desemba, 2018 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupanda kwa bei ya mkate. Lakini tayari maandamano yaliyoanzishwa kwa kupanda kwa bei ya mkate yamesababisha kuondolewa madarakani na jeshi kwa Rais Omar-al-Bashir ambaye amekuwa rais wa Sudan kwa miaka 30, na kwa kuachia ngazi – baada ya siku mbili tu – mrithi wake mwanajeshi na waziri wa ulinzi, Awad Mohamed Ahmed Ibn Auf.

Sasa nafasi ya Ibn Auf imechukuliwa na Luteni Jenerali Omar Zein Alabedin anayeongoza baraza la kijeshi linalotawala Sudan.

Kuwapo viongozi watatu wa nchi ndani ya juma moja si suala ambalo hutokea sana kwenye historia, lakini ni moja ya athari za kukaa madarakani kwa muda mrefu. Mwarobaini wa matatizo ya kukaa kwenye uongozi sana ni pamoja na kung’atuka.

Kuelewa dhana ya kung’atuka ni rahisi sana. Ni makubaliano ndani ya jamii kuwa katika uhai wake, binadamu anapitia rika mbalimbali za maisha na katika kila rika huyu binadamu anakabiliwa na majukumu kadha wa kadha. La msingi, ni kutambua majukumu yake na kuyatekeleza.

Mtoto hana wajibu mkubwa, ingawa enzi hizo watoto walianza kushiriki kwenye shughuli za ufugaji na kilimo katika umri mdogo.

Vijana ndiyo waliokuwa nguvu kazi kubwa ya jamii, wakishiriki kikamilifu kwenye ufugaji, kilimo, uwindaji, na hasa kwenye ulinzi wa jamii yao.

Uongozi ulikuwa ni jukumu linalopewa wale waliyovuka rika la ujana na hawa waliendelea kuwa na wajibu huu muhimu mpaka walipofikia umri wa utu uzima.

Sina hakika sana tukio lipi la maisha lilitenganisha utu uzima na uzee, lakini mtu alipofikia uzee huyu aliachana na majukumu ya uongozi na akabaki kwenye nafasi ya ushauri pamoja na wazee wenzake na akaongezewa jukumu la kuamua mashauri, hasa yale ambayo yalienda kinyume na mila na desturi za kabila.

Sudan imepitia kipindi kirefu cha matatizo ya kiusalama na kisiasa kwa hiyo siyo sawa kusema kuwa suala la kung’atuka kwa kiongozi peke yake kungeweza kufuta matatizo haya. Lakini tunaweza kusema kuwa kiongozi anavyozidi kubaki madarakani, iwe kwa njia za kikatiba au kwa kuvunja katiba, hujiongezea mzigo wa matatizo yanayozuka kwa sababu tu ya kuwepo sehemu moja kwa muda mrefu.

Kama haitamkwi wazi wazi, faida mojawapo ya kung’atuka ni kuoanisha rika la viongozi na rika la wapiga kura, au kupunguza tofauti ya umri kati ya kiongozi na anaowaongoza. Wanaweza kuoanishwa kwa uelewa mpana miongoni mwao; lakini wanaweza pia kuoanishwa hata kwa ujinga.

Inawezekana kiongozi, kwa tofauti kubwa ya umri wake na umri wa sehemu kubwa ya wapiga kura akakosa kabisa uelewa wa mahitaji na malengo ya wapiga kura wa wakati huo. Hili ni tatizo la wazi kabisa linalowakabili watu wazima kila wanapochambua mienendo ya vijana.

Suala siyo kwamba kiongozi anayeng’atuka ni mzuri kiasi gani au kiongozi atakayemrithi ni mbovu kiasi gani. Inawezekana kabisa kuwa mengi ya yale yanayokubalika na wapiga kura  wengi ni masuala ambayo hayana maslahi kwa taifa. Kiongozi mwenye kuelewa dhana ya kung’atuka na akang’ang’ania madarakani anaweza akafanikiwa kubaki madarakani kwa muda tu akipingana na wimbi la kiu ya mabadiliko ambalo si rahisi kuhimili.

Kiongozi anayeelewa dhana ya kung’atuka na akaachia ngazi muda wa kutumikia umma unapomfikisha kwenye uzee, atakaa pembeni na kuwaacha vijana wapambane na changamoto za wakati huo. Lakini iwapo ni kiongozi mwenye uwezo mzuri anajipa pia nafasi ya kutafutwa atoe ushauri wa kuepusha taifa na majanga na kusaidia kulinda maslahi ya wengi.

Nimesikia hivi karibuni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, akitahadharisha baadhi ya wanachama wenzake kuacha kabisa kushabikia wazo la kuanzisha mchakato wa kumuongezea muda kikatiba Rais John Magufuli ili aweze kuendelea kuongoza Tanzania. Alisema wazo la aina hiyo siyo desturi ya CCM.

Alisema Rais Magufuli ataomba ridhaa ya kuongoza kwa kipindi cha pili na akichaguliwa atamaliza muda wake na kumuachia kiongozi mwingine aendelee.

Tanzania, kama nchi yoyote nyingine, ina matatizo mengi yanayoikabili. Lakini kati ya hayo hatuna tatizo la kuwepo mijadala mirefu ya kisheria na kikatiba ya suala la ukomo wa nafasi ya kiongozi wa nchi. Kuna kitu tunapatia. Tujipongeze.

Yapo mengi ya maana tumeachana nayo, lakini msimamo huu ni muhimu sana kuulinda na kuuimarisha. Utatuepusha na matatizo mengi.

Kwa maoni, niandikie: [email protected]

Please follow and like us:
Pin Share