Ujenzi wasimama uwanja wa Kombe la Dunia

Kazi ya ujenzi katika uwanja utakaotumika kwa mashindano ya soko Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil, zimesimamishwa baada ya Jaji wa Mahakama kuhofia usalama.

Uwanja huo wa Arena da Baixada katika Jiji la Curitiba, ulipangiwa kutumika kwa mechi nne za Kombe la Dunia. Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema kuwa ukarabati wa uwanja huo umecheleweshwa kwa muda kadhaa.

 

Jaji Lorena Colnago alisema maisha ya wafanyakazi yanahatarishwa kutokana na hali ya kuzorota kwa ujenzi huo. Aliongeza kwamba kuna hatari ambayo inaweza kusababisha vifo na hata kudondoka kwa kuta za uwanja huo, kutokana na kuta za juu kutokuwa katika viwango bora.

 

Aliagiza kuwa ukaguzi wa uwanja huo ufanywe upya kabla ya kuanza tena shughuli za ujenzi, akisisitiza kwamba zimegunduliwa kasoro nyingi katika ujenzi wa uwanja huo wa kisasa. Taarifa hizo zinakuja wiki moja baada ya uchunguzi kufichua kwamba kuna wafanyakazi walioajiriwa katika ujenzi wa mradi mwingine wa Kombe la Dunia nchini humo, ambao kwa sasa wanakabiliwa na vitendo vya kitumwa.

 

Wachunguzi husika walisema pia kwamba zaidi ya wafanyakazi 100 walioajiriwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sao Paulo wanaishi katika hali duni ya maisha.

Mapema Agosti mwaka huu, Waziri wa Michezo, Aldo Rebelo, alieleza kuwa na wasiwasi jinsi ujenzi ulivyochelewa katika viwanja vitano vitakavyotumika kwa mechi mbalimbali za michuano ya Kombe la Dunia mwakani.

 

Baada ya ziara yake nchini Brazil, Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke, alisema viwanja vyote lazima viwe tayari ifikapo Desemba, mwaka huu, na kuonya kuwa hatavumilia tena kuchelewesha ujenzi, huku  akasisitiza kuwa hakutakuwa na mpango mbadala. Michuano ya Kombe la Dunia imepangwa kufanyika mwakani katika viwanja 12 nchini Brazil.