Tatizo la vibaka limeendelea kuota mizizi katika daladala za abiria, hasa jijini Dar es Salaam. Baadhi ya watu wanaotumia usafiri huo wa umma wamekuwa wakiibiwa fedha na simu za kiganjani kila kukicha!

Wengi tunasikitika kuona vyombo vya ulinzi na usalama, hasa Jeshi la Polisi lenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao halishughulikii kero hiyo licha ya kupelekewa taarifa za vibaka hao mara kwa mara.

 

Vibaka hao sasa ni miongoni wa vyanzo vya umaskini na mifarakano ya ndoa na familia miongoni mwa wananchi. Watu, hasa wanawake wamekuwa wakiibiwa fedha ambazo ni bajeti ya kujikimu katika familia zao. Baadhi ya wanaume wa wanawake walioibiwa fedha na simu za mkononi wameweza kuwapiga na hata kuwafukuza wake zao wakisema kitendo cha kuibiwa cha uzembe.

 

Vibaka hao inadaiwa wanafahamiana na baadhi ya makondakta na madereva wa daladala, na mara nyingi wamekuwa wakiiba fedha na simu wakati watu wanapambana kuingia kwenye daladala, na au wakati abiria wamebanana ndani ya usafiri huo.

 

Kutokana na tratizo hilo la vibaka kuendelea kuwa kero katika miji mingi hapa Tanzania, ninachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wema kuviomba vyombo vya dola viwamulike wahalifu hao ili kuwaondolea wananchi kero hiyo ya muda mrefu sasa.

 

Lakini pia, wananchi na abiria husika nao wana jukumu la kudhibiti tatizo hilo, wajenge tabia ya kushirikiana kuwadhibiti vibaka hao ikiwa ni pamoja na kuviarifu vyombo vya dola kila wanapoona uhalifu hao. Ushirikiano huo utasaidia kupunguza kama si kumaliza kero hiyo katika jamii.

 

Mtumia usafiri wa daladala DSM

 

 

By Jamhuri