Siku mbili kabla ya kuingia mwaka mpya nilipokea ujumbe kutoka kwa watu mbalimbali. Ujumbe huu ulikuwa wa kunitakia heri ya mwaka mpya mimi na familia yangu, lakini mwingine ulikuwa ukigusa masuala ya kitaifa na kimataifa. Nimepoke meseji nyingi, hivyo si rahisi kuziweka zote gazetini, isipokuwa hizi mbili tu nilidhani niziweke.

Ujumbe wa kwanza ulitoka kwa rafiki yangu Mseminari, kwa jina simtaji maana hakunipa ruhusa hiyo. Huyu alinitumia majina ya miaka kama inavyobatizwa huko Bukoba tangu mwaka 1959. Baada ya kupitia majina haya nikaona ni vyema nikayachapisha kwa nia njema kuwa wenyeji wa Bukoba wayasome na hata wakaazi wa mikoa mingine wakipenda wajue Bukoba kila mwaka unaitwaje.

 

Kama wapo wengine wenye kubatiza miaka majina sawa na Bukoba kutoka mikoa mingine, basi itakuwa vyema nikiyapata majina haya nayo nikayachapisha kwa lugha zao. Gazeti ni chombo cha kufikisha mawazo na matukio yaliyopo kwenye jamii bila kujali ukubwa au udogo wa eneo zinakotokea habari husika. Yafuatayo ni majina ya miaka tangu 1959. Majina yatakuwa kwenye mabano.

 

Mwaka wa kwanza ni 1959 Bilema Olengile, Ijawebobele (1960), Bilye Oyekomile, (1961), Gumisa Omwoyo (1962), Otula Obungya (1963), Kalamaishanyo (1964), Ndalweboine (1965), Babindangiile (1966), Tekaana (1967), Tabaro (1968), Nyiikila (1969), Tweyambe (1970), Sisimuka (1971), Shaaya (1972), Gendelela (1973) na Wekebuke (1974).

 

Majina ya miaka mingine ni Kakikweyo (1975), Ijabalebe (1976), Enjuuza (1977), Shuliza (1978), Tikiliwaigamba (1979), Bululula Obone (1980), Galaziwa Enzii (1981), Goshooko (1982), Shobokelwa (1983), Ikingula (1984), Kankweanuzeo (1985), Shubi (1986), Yemoge (1987), Kakutatantalikwa (1988), Kwatilao (1989) na Anuniliwa (1990).

 

Miaka iliyofuata kwa majina ni Umula (1991), Nyineiliwo (1992), Yombeka (1993), Umbya (1994), Guma (1995), Wechuze (1996), Chwazika (1997), Tekeleza (1998), Fukama (1999), Shanduka (2000), Shamura (2001), Rundana (2002), Webaze (2003), Shabuka (2004), Siima (2005), Milembe (2006), Tegeka (2007), Rashana (2008), Jwahuka (2009), Chulela (2010), Tongana (2011), Wechonche (2012) na Webange (2013).

 

Najua aya hizo tatu kwa mtu asiye Mwenyeji wa Bukoba zitakuwa zimekupa shida kutamka na kufuatilizia nini kinaendelea, lakini kimsingi majina haya yanaendana na utabiri wa neema au shari kwa mwaka husika. Utaratibu huu ulianza siku nyingi kwa Bukoba na unatumiwa pia kuweka kumbukumbu kwa baadhi ya watu wanapofanya mambo yao. Je, kuna kitu orodha hii imekufundisha mpendwa msomaji? Nijulishe.

 

Ujumbe wa pili nilioupata ni huu: “Moja ya mikakati aliyoitangaza [Rais Jakaya] Kikwete baada ya kuingia Ikulu ni kuitoa nchi mahala ilipo na kuifikisha mahala pengine! Je, unajua kama ameishatimiza hilo? Ametutoa kutoka mchele kilo 1 tsh 800 hadi 2,500, nyama 2,500 hadi 6,000, sembe 250, hadi 1,200, kutoka kuwa na ndege 11 za ATCL hadi ndege 1 mbovu.

 

“Treni zilizokuwa zinazunguka Dar to Kgm, Dar to Mwz, Kilombelo to Mufindi sasa imezinduliwa Dar to Dar kwa majaribio. Hii ndo CCM na Magamba yao.”

 

Nilipoupata ujumbe huu nikatafakari kwa kina. Nikakumbuka kuwa mwaka 2006 lita ya petrol pia ilikuwa inauzwa Sh 600 leo inauzwa Sh 2,200. Sukari kilo moja ilikuwa inauzwa Sh 600 leo ni Sh 2500. Deni la Taifa, Rais Benjamin Mkapa alikuwa amelipunguza hadi Sh trilioni 5.5 chini ya mpango wa kuzisamehe madeni nchi masikini sana duniani (HIPC), leo limefikia trilioni 22.

 

Kikwete ameipokea Tanzania ikwa nchi moja, lakini leo Tanzania ni nchi mbili. Zanzibar wametwambia Watanzania na walimwengu kuwa Zanzibar ni nchi na mipaka yake imerejea katika hali ya kawaida ilivyokuwa kabla ya Muungano mwaka 1964, Rais Kikwete amekaa kimya. Pengine anaona bora akae kimya kikombe hiki kumwepuke.

 

Kikwete aliichukua nchi hii walimu wakiwa wanafundisha, lakini baada ya kuwambia hahitaji kura zao walimu nao wameacha kufundisha na ndiyo maana tunapata wanafunzi wanaoshinda mitihani ya darasa la saba wasiojua kusoma na kuandika.

 

Kikwete alichukua nchi hii walimu wakiwa wanasahihisha mitihani ya darasa la saba, lakini kwa sasa inatumika teknolojia ya kusiriba na mbaya zaidi hata mitihani ya hesabu ni ya kuchagua. Mitihani ya jiografia pia na ramani zake ni ya kuchagua. Hakuna mwanafunzi kupoteza muda kuchora ramani kwenye mtihani! Tumeendelea eheee?

 

Nimejaribu kuangalia kwenye siasa. Kikwete alikuta Baraza la Mawaziri lina Uwajibikaji wa pamoja. Leo mawaziri kila mtu anatoa kauli yake. Naibu Waziri anaweza kuziambia kampuni za wawekezaji kuwa yeye ni rafiki na wakubwa na hivyo waziri wake asiwababaishe atahakikisha wanapata wakitakacho.

 

Rais wetu alikuta wanafunzi wa elimu ya juu wanaochaguliwa kuingia vyuo vikuu wakipewa mikopo bila ubaguzi, lakini leo yeye anatumia kigezo cha means testing. Maelezo ni kwamba wanatafuta watoto kutoka familia masikini, lakini mwisho wa siku wanaishia kupata mikopo hii watoto wa vigogo. Serikali sasa inabagua walipakodi kwa kutumia madaraja ya kwanza na ya pili huku ikijua fika kuwa sifa za kuingia chuo kikuu ni hadi daraja la tatu.

 

Yapo mengi ila nihitimishe na moja. Kikwete aliingia madarakani akakuta kampeni za uchaguzi ndani ya chama zinaongozwa na Jumuiya ya Vijana (UVCCM) yeye anasema urais ni suala binafsi anamtumia mtoto wake si la kichama zaidi. Tulikuwa hatujawahi kumpata mke wa Rais kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, leo mke wake na mtoto ni wajumbe wa mkutano huo na NEC pia.

 

Haya yote nani anabishi kuwa Kikwete hajabadili sura ya nchi hii? Nani anabishi kuwa hajatutoa alipotukuta na kutufikisha alikokutaka? Hoja yangu na pengine nikuulize wewe msomaji, je, ametutoa kwenye karaa na kutuleta kwenye neema au kinyume chake? Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana. Heri ya Mwaka mpya 2013.

By Jamhuri