Mbunge wa Afrika Mashariki, Adam Kimbisa na wenzake wanatuhumiwa kujitwalia na kujimilikisha Chama cha Masalaba Mwekundu (TRCS) na kukitumia kwa manufaa yao binafsi.

Wengine wanaotuhumiwa ni wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu Kimbisa, Naibu Katibu Mkuu Peter Mlebusi, Mkurugenzi wa Fedha, Ally Rajabu, Mkurugenzi wa Maafa Joseph Kimario, Mkuu wa Hesabu, Gideon Balangwa na Sixbert Shimbe.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa miezi sita sasa umebaini kuwa kufanikisha mambo yao sekretarieti hiyo imekuwa ikipanga safu ya uongozi kwa kufuata maslahi yao binafsi. Sekretarieti hiyo inatuhumiwa kupitisha viongozi mbalimbali wa mikoa kwa kufuata matakwa ya uongozi huo.


Tayari uongozi wa chama hicho umeingia katika kashfa ya kupitisha majina ya watu wasio na sifa kuongoza mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma. Waliopitishwa kwa kufuata masharti ya sekreteriti hiyo na si kanuni za uchaguzi na sheria ya chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni Leonard Masono kwa nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ni Haidari Riko na Mweka Hazina, Heri Kalungwana.

 

Waliotemwa ni Laurian Rugambwa aliyegombea nafasi ya Mwenyekiti, Sufiani Juma (Makamu Mwenyekiti), Muhsin Tusa (Mipango na Maendeleo), Zahara Hassan na Amina Mwalimu (Kitengo cha Mfunzo).


Pamoja na wanachama wa chama hicho kuandika barua ya kuweka pingamizi juu ya viongozi waliogombea nafasi mbalimbali kwa madai ya kutokuwa na sifa za kugombea nafasi hizo, malalamiko yalifumbiwa macho na uongozi.


Katika barua yao ya Oktoba 16, mwaka jana, wanachama hao walieleza kuwa kwa miaka 15 uchaguzi huo kwa mara tatu umeendeshwa kibabe, hususani katika mchujo wa mjina ya wagombea.


Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa mwaka 2000, Naibu Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Ajira, Makongoro Mahanga alipitishwa kugombea nafasi ya uhazini wakati si mwanachma wa chama hicho.


“Isitoshe mwaka 2006 kulikuwa na wagombea waliopitishwa bila kuwa na sifa mfano, Bw. Yakubu aliteuliwa kuwa mtunza hazina wakati hakuwa mwanachama. Alichukuliwa kutoka Lions Club na ndo sababu iliyomfanya Yakubu  kutowahi kuonekna ofisini tangu alipochaguliwa,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.


Barua hiyo ilieleza kuwa katika uchaguzi wa mwaka jana majina ya wagombea wengine yalikatwa bila kufuata taratibu zozote za kikatiba au kanuni husika.


Hata hivyo, jinamizi la kukata majina ya wagombea wanaonekana kuwa mwiba katika sekretairiti hiyo limezidi kushika kasi baada ya kukata majina mengine katika ngazi ya Mwenyekiti wa taifa

Kuna taarifa kuwa bodi imekata majina ya wagombea walioomba kugombea nafasi ya mwenyekiti na kuweka mazingira ya kumpitisha, Dk. George Nangale.


Inaelezwa kuwa pamoja na Dk. Nangale, wengine waliopitishwa kwa nafasi hiyo ni Dk. Gotlieb Mpangile na Mama Makoye, huku majina ya Laurien Rugambwa na Dk. Shoo yakikatwa. Taarifa nyingine zinaeleza kuwa kuna mkakati utakaohakikisha, Dk. Nangale anashinda kiti hicho kwani hadi sasa bodi hiyo imemtaka Dk. Mpangile kuondoa jina lake siku ya uchaguzi utakaofanyika Januari 28 hadi 29 mwaka huu huko Mwanza.

 

Mmoja wa wafanyakazi wa chama hicho ameliambia Jamhuri kuwa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, ambaye ni mlezi wa chama hicho hashirikishwi katika uamuzi wa bodi hiyo na hapelekewi taarifa.

“Unajua chama kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 71 ya Desemba 31, 1962 na Mlezi wake na Rais Jakaya Kikwete  lakini hadi sasa hashirikishwi. “Hata leo kama kuna wabunge katika mkutano wa bunge anayetaka kujua ni jinsi gani Red Cross inafanya kazi hakuna waziri yeyote anayeweza kujibu kuhusu hilo.

 

“Kisheria inatakiwa kuwa chini ya wizara kama ya Afya au wizara inayosimamia Ustawi wa Jamii, lakini wamekuwa wakifichaficha mambo tu kwa kuogopa kuulizwa maswali ambayo yataibua mambo mazito. “Na sidhani kama hata kama rais anajua kuwa yeye ndiye mlezi wa chama hicho,” amesema.

 

Amesema Katibu Mkuu wa TRCS, Adamu Kimbisa na Naibu Katibu Mkuu Peter Mlebusi wao ndio wanaotajwa kukifanya chama hicho kuwa mali yao. Amesema Mlebusi anatuhumiwa kutumia mali za ofisi kwa manufaa binafsi.

 

Amezitaja mali ambazo Mlebusi anatumia kinyume na matakwa ya ofisi kuwa ni magari, Toyota Land Cruiser namba T 327 ALW analotumia kwa kazi za nyumbani. Gari nyingine ni Nissan Patrol namba T 729 BEV ambalo linatumiwa na familia yake.

 

Uchunguzi wa JAMHURI, pia umebaini kuwa mara kadhaa Mlebusi amekuwa akitumia lori aina ya Marcedes Benzi namba T 479 AEL  kwa ajili shughuli za ujenzi na shamba bila ruhusa ya ofisi. Mwaka jana  gari hilo  mali ya TRCS  lilijazwa mafuta  kwa gharama za ofisi likatumika kubeba migomba kutoka Moshi kwenda shambani kwake Tegeta Dar es Salaam bila idhini ya ofisi.

 

Tuhuma nyingine zinazomkabili Mlebusi ni kutoa ajira bila kufuata utaratibu kwa mtoto (jina linahifadhiwa) wake, ambaye ameajiriwa kama Ofisa katika Kitengo cha Damu Salama cha chama hicho. Kuna taarifa kuwa mtoto huyo amekuwa akifanya kazi kwa kudeka kwa kudai chochote anachotaka hata kama ni nje ya mkataba wake wa kazi.

 

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Desemba 12 hadi 14 mwaka jana, TRCS ilipeleka wafanyakazi wake Arusha kwa ajili ya kupata mafunzo ambapo walilipiwa gharama zote ikiwemo nauli na malazi kwa kila mfanyakazi akimwemo mtoto huyo.


Hata hivyo, ingawa mtoto huyo alikubali kwenda kwa basi baada ya kumaliza mafunzo aligoma kurudi kwa kutumia usafiri huo kwa madai kuwa yeye ni mtoto wa bosi, hapaswi kupanda basi.

Hivyo alitaka kutumiwa gari la ofisi kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, jambo lililotekelezwa na baba yake.

 

Uchunguzi umebaini kuwa mzizi wa matatizo katika chama ni viongozi kukaa muda mrefu madarakani licha ya kufikisha umri wa kustaafu. Taarifa zilizopatikana katika ofisi za TCRS zinaonesha kuwa wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho wanapaswa kuwa wamestaafu tangu mwaka jana na wengine mwaka juzi.

 

Katibu Mkuu Kimbisa alizaliwa Agosti 2, 1952 na kuajiliwa na chama hicho 1986 hivyo alipaswa kustaafu mwaka jana. Licha ya umri, pia Kimbisa anatakiwa kuachia ngazi ya ukatibu mkuu wa chama hicho kwa kwani anabanwa na kanuni  za uchaguzi za 2011 na sheria za nchi kwa kuwa chama hicho kilipitishwa kwa sheria ya bunge.

 

Kanuni hiyo inaeleza kuwa kiongozi anatakiwa awe mwanachama wa kawaida kwa nafasi ya mwenyekiti au katibu na wagombea wa nafasi za juu za TRCS kama Mwenyekiti na Katibu wasiwe viongozi wa vyama vya siasa.

 

Kimbisa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki hivyo hastahili kuwa kiongozi wa chama hicho. Naibu Katibu Mkuu, Peter Mlebusi alizaliwa mwaka 1952 na kuajiliwa katika chama hicho mwaka 1976 hivyo alitakiwa kuachia ngazi mwaka jana.

 

Wengine ni Mkurugenzi wa Fedha, Ally Rajab (1949) alitakiwa kustaafu mwaka 2009 Mkurugenzi wa Maafa, Joseph Kimario 1953  anapaswa kustaafu mwaka huu.

Wengine ni Sixberty Shimbe (1947) alipaswa kustaafu 2007 lakini hadi sasa bado anaendelea na kazi.


Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti viongozi hao walikanusha madai hayo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Msafiri Ramadhani Msafiri ameliambia JAMHURI kuwa viongozi hao watang’oka baada ya uchaguzi huo.


“Ndugu mwandishi hayo unayoniuliza tusubiri uchaguzi ufanyike ndio tutapata majibu kama wanatangoka ua la ndio tuzungumze,” amesema. Naye Kimbisa amesema kuwa madai hayo si ya kweli bali yanalaenga kukichafua chama hicho.

 

“Duniani kote ikitokea uchaguzi lakini mmoja akashindwa basi ataleta sababu ya kuwa kaonewa, hebu achana na hizo habari ndugu. Hayo ni majungu wanataka kukichafua chama kwa kukipaka matope hakuna kitu kama hicho,” amesema Kimbisa.


Naye Mlebusi amesema kuwa shutuma hizo si za kweli kwa kuwa zinatolewa na watu walioshindwa katika uchaguzi. “Kaka hao wanakutumia vibaya usiwasikilize waambie wakasome Katiba na kanuni za uchaguzi hakuna kitu hicho” amesema.

By Jamhuri