*Wagombe urais watarajiwa Pinda, Lowassa, Membe njia panda
*Marando, Lissu, Dk. Slaa wataka wananchi wapige kura ya maoni
* Kikwete, Prof. Lumumba, Jaji Mtungi wawataka warejee bungeni
Na Mwandishi Wetu

Kuna kila dalili kuwa Tanzania sasa iko njia panda baada ya msimamo usioyumba wa wabunge waliojinasibu kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuwa hawarejei kwenye Bunge la Katiba linaloanza leo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaeleza kuwa yameibuka makundi mawili ndani ya chama hicho, wakiwamo wanaotaka Bunge Maalum la Katiba liendelee, huku wengine wakisema Katiba itakayotungwa bila upinzani halisi kuwa bungeni itakosa uhalali.
Wanachama wa CCM pia wenye nia ya kugombea urais mwakani, akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Bernard Membe, Edward Lowassa na John Magufuli, imeelezwa kuwa wako njia panda. “Hadi sasa hawajui iwapo waanze kampeni za chini kwa chini kwa ajili ya kugombea urais wa Tanzania au Tanganyika,” kilisema chanzo chetu.
Tamko la Waziri Mkuu Pinda kuwa Katiba Mpya isipopitishwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa hautafanyika mwaka huu, vyanzo vya habari kutoka ndani ya CCM vinasema Pinda anapigia chapuo Katiba mpya kwa matumaini kuwa ikipita yeye atagombea urais wa Tanganyika na kushinda.
“Amezungumza na marafiki zake akasema anajua hawezi kupata urais wa Tanzania kwa kuwa Zanzibar wanamchukia kuliko maelezo. Amekwenda mbali akaonyesha wasiwasi kuwa huenda Zanzibar baada ya kauli yake kuwa Zanzibar siyo nchi, hawezi kupata hata wadhamini 20, hivyo kugombea urais wa Tanzania kwake ni ndoto.
“Pinda sasa anatumia nguvu kubwa kupitisha Katiba mpya, ili apate fursa ya kugombea urais wa Tanganyika na ndio maana muda wote anasema yeye ni mtoto wa mkulima, anafuga nyuki kwa nia ya kuwarubuni watu wa Tanganyika wamuone ni mkulima mwenzao,” kimesema chanzo chetu.
Midahalo mitatu iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kati ya UKAWA na CCM na ule Chama cha Wanasheria Tanganyika, umeawaacha wananchi njia panda hasa baada ya msimamo uliotangazwa na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, aliyejitangaza kuwa ni mjumbe wa Ukawa, Tundu Lissu.
Lissu amesema mazungumzo yote yaliyokuwa yanaendelea yamevunjika na hakuna uwezekano tena wa UKAWA kurejea kwenye Bunge Maalum la Katiba kwani tayari CCM wamekwishabadili kanuni baada ya UKAWA kuondoka bungeni na tayari sasa wanaweza kubadili kifungu chochote cha rasimu ya Katiba.
Katika mkutano uliofanyika Jumamosi Agosti 2, 2014 Lissu alisema CCM walibadili kanuni Aprili 9, baada ya Ukawa kutoka bungeni. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Ukawa walitoka bungeni Aprili 16, hivyo Aprili 9 walikuwamo ukumbini.
Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo, Profesa Patrick Otieno Lumumba kutoka Kenya aliwasihi UKAWA kurejea bungeni kwa maelezo kuwa kutokuwapo kwao kunatoa fursa pana kwa CCM kufanya watakalo akiwapa mfano wa Kenya kuwa waliposusa wakatoka bungeni chama tawala kiliteka mchakato mzima wa Katiba.
Profesa Lumumba alitumia maneneo ya kifalsafa akisema katika Afrika, Tanzania pekee ndio nchi yenye utulivu na amani, lakini akaonya kuwa anaona malaika wa vita wanaiita Tanzania itumbukie katika vurugu kisha baada ya machafuko wanasiasa watarejea kwenye meza ya mazungumzo kurudi hapa nchi ilipokuwa kabla ya mapigano.
David Kagulila, ambaye ni mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, alisema mkwamo uliotokea ni jambo la afya, kwani umewafanya Watanzania kufuatilia kwa karibu mchakato wa Katiba unavyokwenda nchini.
Pamoja na kwamba imependekezwa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika kwenda Mahakamani kutafuta tafsiri cha Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inaelezwa kuwa kengele nyingi zinazopigwa sasa ni za kusitishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.
Lissu na wanasiasa wengine kama Dk. Wilbrod Slaa, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema wanasema sasa hali ilipofikia hakuna sababu ya kuendelea na mchakato wa Katiba kwani unaweza kuzaa zahama badala ya neema.
Katika hatua nyingine, Lissu anasema bunge la Katiba limetekwa na wanasiasa. Anasema mchakato huu ulipaswa kuwahusisha wananchi wenye mawazo huru na akawashangaa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika kwa kushindwa kujiingiza katika mchakato huu na kuingia sasa “wakati mambo yamekwishahabarika.”
Rais Jakaya Kikwete ambaye awali ametoa msimamo kuwa Wajumbe wa  Bunge Maalum la Katiba wakishindwa kuelewana ndani ya siku 60 zijazo atasitisha mchakato huu, katika hotuba ya mwisho wa mwezi Julai amesema yeye hakuwa na kosa kutoa maoni yake wakati wa kuzindua Bunge Maalum la Katiba Machi 21.
Kikwete amewataka UKAWA kurejea bungeni akisema malalamiko waliyonayo ni vyema wakayatolea bungeni badala ya kuyasema mitaani, na akasema hakufanya kosa kueleza kuwa chama chake kinaamini katika mfumo wa serikali mbili.
Katika mdahalo wa Jumamosi, Profesa Lumumba alisema ingawa Bunge lina mamlaka ya kuboresha rasimu iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba halina mamlaka ya kubadili mambo ya msingi. Mgogoro mkubwa umekuwa iwapo Bunge hilo libadili misingi ya rasimu na kupendekeza Serikali mbili au tatu. CCM wanataka serikali mbili na upinzani unataka serikali tatu.
Mwanasheria wa Chadema, Mabere Marando amesema yeye anachoona ni ama CCM waanzishe mchakato wa kwenda kwa wananchi kupiga kura za iwapo wananchi wanautaka Muungano au la na kama wanautaka uwe wa Serikali ngapi.
Marando ameshauri kuwa ikiwa hilo litakuwa gumu, mchakato usitishwe sasa na iwe ajenda ya uchaguzi mkuu ujao mwakani. “Twenda kwenye kura na ajenda hii, tuwambie wananchi kuwa anayekataa Katiba mpya wasimpe kura, alafu wananchi wachague kati ya anayetaka kuwapa Katiba mpya na asiyetaka.”
Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mtungi ameliambia JAMHURI kuwa yeye kama mlezi wa vyama vya siasa ana wajibu wa kuhakikisha mgogoro uliopo kati ya UKAWA na CCM unakwisha kwani hauna masilahi yoyote kwa taifa.
“Mimi ni Msajili na Mlezi wa vyama vya siasa nchini. Kwa kawaida huwa tunakutana na sasa tuna vyama vinavyovutana, hivyo nawajibika kuvikutanisha,” ameliambia JAMHURI, ingawa amesisitiza kuwa yeye hasuluhishi UKAWA, bali anakutana na vyama vya siasa vyenye usajili.
Amesema wamekutana mara tatu ndani ya mwezi Julai na lengo ilikuwa ni kumaliza tatizo lililopo, na bado anaamini katika mazungumzo kila tatizo linamalizwa.
Jaji Mtungi amesema Katiba mpya ni suala lenye masilahi ya taifa kwa Watanzania wote, hivyo kusitisha mchakato wake ni kutowatendea haki Watanzania.
Alipoulizwa yeye kama Msajili atawezaje kumaliza mgogoro wa idadi ya serikali iwapo ziwe mbili au tatu, alisema suluhisho ni UKAWA kurejea bungeni ambako watajadili hoja hizo na kupata suluhisho.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, ameliambia JAMHURI kuwa chama tawala kimefanya mbinu nyingi ikiwamo ahadi ya kuongeza posho kwa wajumbe waweze kurejea bungeni.
“Ingawa kuna msimamo kuwa UKAWA hawatarudi bungeni, lakini kuna dalali kuwa posho huenda zikawarudisha ndani ya Bunge. Sisi tumepata taarifa kuwa posho zimeongezwa hadi Sh 700,000 kwa siku kutoka Sh 300,000 za sasa,” amesema Kibamba na kuongeza: “Kiasi hiki kinashawishi wengi kurejea bungeni.”
Amesema ukitaka kufahamu kuwa fedha zina ushawishi, baada ya Jukwaa la Katiba kukutana na CCM Julai 14, walipanga kukutana na UKAWA Julai 16, lakini UKAWA walisita kuhudhuria mkutano huo wakaenda kushauriana na Serikali, hali inayomtia wasiwasi kuwa si muda watarejea bungeni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, amekanusha vikali tuhuma kwamba posho ya vikao kwa wabunge imeongezwa. “Hakuna kitu cha namna hiyo. Hakuna nyongeza,” alisema Lukuvi na kuongeza; “Ningekuwa mtu wa kwanza kupata taarifa hizi. Mimi ndiye nawajibika kusimamia taratibu za Bunge hili kwa upande wa Serikali, ningejua tu.”
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, ambaye katika Bunge Maalum la Katiba ni Naibu Katibu wa Bunge alipoulizwa juu ya ongezeko la posho, kwa mshangao alisema: “Nani kasema? Hakujakuwapo mabadiliko tangu bunge lilipoahirishwa mwezi Aprili.”
Kwa upande wake Dk. Slaa, ameliambia JAMHURI kuwa zimekuwapo juhudi nyingi za kuwarejesha bungeni UKAWA lakini zote zimegonga mwamba na akawaonya wajumbe wa UKAWA kuwa posho zisiwapofushe hata kama zimeongezwa.
“Ni jambo baya, na tumewaonya wajumbe wetu kuwa macho na hela. Hatukutoka nje ya bunge kwa sababu ya fedha, lakini tulitoka kwa sababu ya misingi tunayoiamini kukiukwa,” amesema na kuongeza: “Ukipiga hesabu ya kiasi kinachotajwa inakaribika Sh milioni 42 kwa kila mjumbe, lakini wanachopaswa kufahamu hata Yesu Kristo alisulubiwa kwa ajili ya fedha. Wawakilishi wetu wasikubali kuwa sehemu ya dhambi hii.”
Kuhusu UKAWA kurejea bungeni, alisema ikiwa CCM wanataka serikali mbili sheria iko wazi kuwa warejee kwa wananchi wawahoji juu ya hilo. “Wananchi ndio wenye mamlaka ya kubadili rasimu ya Katiba, bali kuibadili kwenye Bunge Maalum la Katiba itakuwa ni kutoheshimu mawazo yao.”
Wajumbe wa UKAWA wanakadiriwa kufikia 200 na kati ya wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete imetajwa na Lissu kuwa 166 wanatoka CCM baada ya kuwa wamejipachika vyeo bandia ikiwamo wanaojitambulisha kama waganga wa kienyeji.
Wajumbe 438 ni wabunge na wajumbe wa Baraza la wawakilishi kati ya idadi kuu ya wajumbe 629 wanaounda Bunge Maalum la Katiba la sasa.
Baadhi ya wajumbe wa UKAWA wanaotambulika rasimi ni: Mwanamrisho Taratibu Abama (CHADEMA), Rashid Ali Abdallah (CUF), Abdalla Haji Ali (CUF), Amina Amour Abdulla (CUF), Chiku Abwao (CHADEMA), Rukia Kassim Ahmed (CUF), Mustapha Akunaay (CHADEMA), Salum Barwany (CUF), Mbarouk Salim Ali (CUF) na Abdalla Haji Ali        (CUF).
Wengine ni Said Arfi (CHADEMA), Selemani Saidi Ally Bungara (CUF), Agripina Buyogera (NCCR-MAGEUZI), Haji Makame Faki (CUF), Pauline Gekul (CHADEMA),  Khatib Said Haji (CUF), Zahra Ali Hamad          (CUF), Hamad Ali Hamad (CUF) na Assa Othman Hamad          (CUF), Riziki Omar Juma (CUF) na  David Kafulila (NCCR-MAGEUZI).
Wengine ni Haji Khatib Kai (CUF), Naomi Kaihula  (CHADEMA),,Prof. Kulikoyela Kahigi (CHADEMA), Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA), Yussuf Haji Khamis (CUF), Raya Ibrahim Khamis (CHADEMA), Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), Mkiwa Kimwanga (CUF), Susan Kiwanga (CHADEMA) na  Grace Kiwelu (CHADEMA).
Wajumbe wengine wa UKAWA ni Highness Kiwia (CHADEMA), Kombo Khamis Kombo (CUF), Anna Komu  (CHADEMA), Godbless Lema (CHADEMA), Tundu Lissu (CHADEMA), Susan Lyimo (CHADEMA), Moses Machali (NCCR-MAGEUZI),  Salvatory Machemli (CHADEMA) na AnnaMaryStella Mallac (CHADEMA).
Wengine ni Esther Matiko (CHADEMA), Antony Mbassa (CHADEMA),  James Mbatia (NCCR-MAGEUZI), Joseph Mbilinyi (CHADEMA), Freeman Mbowe (CHADEMA) , Kuruthum Mchuchuli (CUF), Halima Mdee  (CHADEMA), Felix Mkosamali (NCCR-MAGEUZI) na  Rebecca Mngodo (CHADEMA).
Wengine ni pamoja na Eng. Mohamed Habib Mnyaa (CUF), John Mnyika  (CHADEMA), Hamad Rashid Mohamed (CUF), Rajab Mbarouk Mohammed (CUF), Maryam Salum Msabaha (CHADEMA), Rev. Peter Msigwa (CHADEMA), Christowaja Mtinda (CHADEMA), Philipa Mturano (CHADEMA) na  Christina Mughwai Lissu (CHADEMA).
Wengine Thuwayba Idrisa Muhammed (CUF),  Haji Kombo Mussa (CUF), Joyce Mukya (CHADEMA), Clara Mwatuka (CUF), Amina Mohamed Mwidau (CUF), Joshua Nassari (CHADEMA), Rev. Israel Natse (CHADEMA), Philemon Ndesamburo (CHADEMA), Ahmed Juma Ngwali (CUF) na  Vincent Nyerere (CHADEMA). Wengine ni Leticia Nyerere (CHADEMA), Rashid Ali Omar (CUF), Rashid Ali Omar (CUF), Meshack Opulukwa (CHADEMA) , Lucy Owenya (CHADEMA), Cecilia Paresso (CHADEMA), Rachel Mashishanga (CHADEMA), Mhonga Ruhwanya CHADEMA), Conchesta Rwamlaza (CHADEMA) na Said Suleiman Said (CUF).
Moza Abedi Saidy (CUF), Magdalena Sakaya (CUF), Masoud Abdallah Salim (CUF), Muhammad Ibrahim Sanya (CUF), Ali Khamis Seif (CUF), Joseph Selasini (CHADEMA), Haroub Shamis Mohamed (CUF), John Shibuda (CHADEMA), David Silinde (CHADEMA), Rose Kamili (CHADEMA), Sabreena Sungura (CHADEMA) na  Ezekia Wenje (CHADEMA).

By Jamhuri