Mjadala wa ukosefu wa ajira unazidi kushamiri. Ndiyo, tatizo la ajira lipo na bila shaka litaendelea kuwapo; si kwa Tanzania tu, bali kwa mataifa mengi duniani.

Nchi kama ilivyokuwa Libya, kwao tatizo la ajira lilikuwa dogo. Hali hiyo ilitokana na umakini wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi. Wasiokuwa na ajira walilipwa mishahara. Vijana waliotaka kuoa walipewa mahari. Kwa ufupi, kila mwananchi aliweza kufaidi matunda ya nchi yake yaliyotokana na utajiri mkubwa wa mafuta.

Ndugu zetu hao wakaona waliyopata chini ya Gaddafi si lolote si chochote! Wakalilia demokrasia ya Magharibi. Wameipata. Sasa wanalia. Hawana wa kuwasaidia. Wanataka wakatubu kwenye kaburi la Gaddafi, hawajui liliko. Majuto ni mjukuu. Wanastahili kabisa wanachokipata sasa.

Nchini mwetu wapo wenye nadharia kama za raia kadhaa wa Libya. Tuna kundi la vijana wanaodhani utatuzi wa matatizo yetu ni suala la kudra za Mwenyezi Mungu. 

Huyu Mungu tumekuwa tukimsingizia mambo mengi mno. Mtu anapokosa mlo, hata kama yuko kando ya mto, jibu la mkato ni; “ni mapenzi ya Mungu hakunipa”. 

Katika safu hii, nimewahi kusema kuwa encyclopedia ya maendeleo yetu ni maandishi na hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katika kijitabu chake cha TUJISAHIHISHE alichokiandika Mei, 1962 (miaka 54 sasa), Mwalimu Nyerere anasema maneno haya:

“Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu. Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, na kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo.

“Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalaumu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k, lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchunguzi wa kweli, siyo sababu ya uvivu wa kutumia akili! Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si dawa hata kidogo. Nikienda kwa mganga anitibu maradhi yangu, namtazamia kuwa kazi yake ya kwanza ni kujua hasa, siyo kwa kubahatisha, naumwa nini; kazi yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu; kazi yake ya tatu ni kujua dawa ya ugonjwa wangu. Daktari asipojua ugonjwa wangu na sababu zake hawezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona, atakuwa kaniponya kwa bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo hawezi kumponya mgonjwa, na ni daktari wa hatari sana.”

Haya ni maneno muhimu mno kwa wakati huu pengine kuliko miaka hiyo ya 1960. Tunapozungumza tatizo la ajira, mchawi wetu amekuwa ni ‘Serikali’. Hili ni kosa kubwa. Na sidhani kama lawama kwa Serikali pekee zinaweza kuwa jawabu la tatizo hili.

Tatizo la ajira, kwa mtazamo wangu, jawabu lake lipo kwa mtu mmoja mmoja, jamii hadi Taifa zima. Hatuwezi kukaa tukabweteka kwa matarajio ya kulimaliza tatizo hili kwa kulalama tu.

Tatizo la ajira katika nchi yetu linaanzia kwenye mfumo wa elimu tunayowapa watoto wetu. Elimu yetu bado ni ya kumfanya mtoto aishi akitambua kuwa wajibu wa yeye kupata ajira uko mikononi kwa Serikali. Hili ni kosa kubwa. Sina hakika na kauli moja aliyonipa rafiki yangu Mkenya, lakini aliniambia haya; kwamba nchini Kenya, asilimia 80 ya wahitimu wa vyuo akili zao zinawatuma kujiajiri, na ile asilimia 20 inayobaki ndiyo wanaosubiri kuajiriwa serikalini. Tanzania, anasema ni kinyume chake. Asilimia 20 wanapata walau wazo la kujiajiri, ilhali asilimia 80 wao wanapotoka chuo hubaki wanasubiri lini wataitwa kufanya kazi katika serikali, kwenye taasisi za serikali au katika mashirika na asasi binafsi! 

Bila kupindua mtazamo huu, nchi hii itaendelea kuwa na genge kubwa mno la watu ambao kazi yao ni kulalamika tu.

Kwangu mimi, hii ‘sifa mbovu’ ya mtu kuonekana msomi lazima awe amehitimu shahada, inatuponza na kutukosesha stadi za maisha. Serikali inatumia mabilioni ya shilingi kuwapa vijana elimu ambayo haina msaada wowote kwao.

Mwaka juzi, Idara ya Uhamiaji ilitangaza nafasi 70 za ajira. Vijana walioomba ni zaidi ya 20,000. Baada ya kuchujwa, wakasalia vijana 15,000. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, wale vijana 15,000 wakaitwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ili kufanyiwa mchujo ambao ungebakiza vijana 70 pekee! Kama hatukushituka kwa tukio hilo, basi tutakuwa na matatizo ya uelewa.

Unapokuwa na vijana 15,000 wote wakisubiri kuajiriwa, hili ni janga. Lakini kwanini uwe na idadi hiyo? Kuna sababu nyingi. Mosi, hawa vijana wanapokwenda vyuoni kusoma, wanasoma kuhitimu! Hawasomi ili siku moja waweze kujiajiri. 

Pili, Serikali inapoona fahari kusomesha vijana kozi za sayansi ya siasa, itambue kuwa hatuwezi kuwa na shughuli za kisiasa za kuhimili idadi hiyo.

Tatu, Serikali inapokuwa radhi kuwakopesha vijana wanaosoma shahada, lakini ikapuuza kutoa mikopo kwa vijana wengi kusomea ufundi mchundo, matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona sasa.

Ni wajibu wa wazazi na Serikali kuwabadili fikra watoto wetu. Hapa, tunaona mifano kwa wale wanaohitimu shahada zinazohusu kilimo na ufugaji. Tujiulize, kila mwaka kuna vijana maelfu kwa maelfu wanahitimu masomo kwenye fani hizo, wangapi wako radhi kushika udongo au kinyesi cha ng’ombe? Kwa Tanzania, msomi maana yake ni ‘msafi’! Kushika kinyesi au udongo ni dalili ya mtu ambaye hakusoma! Huu ugoro ndiyo uliomo vichwani mwa vijana wetu wengi.

Tujiulize, kwanini vijana wetu wanaosoma vyuo vikuu, wenye sharubu na wanaotambua na kushiriki starehe zote, wawe tegemezi kwa wazazi na walezi wao kwa kila kitu? Wazazi wangapi wanawabana vijana wao wafuge kuku, walishe ng’ombe, au wafanye kazi yoyote nyepesi, isiyoathiri mwenendo wa masomo yao, yenye kuwasaidia kupata fedha kwa mahitaji madogo madogo? Je, ni busara kwa kijana mwenye masharubu kudeka kwa wazazi au walezi ili apate fedha za kwenda saluni?

Waliokwenda kusoma Ulaya na Marekani wanatambua namna vijana wetu wanaokwenda huko wanavyohangaika kusoma na wakati huo huo kufanya kazi za kuosha vyombo, kutunza vikongwe na ajuza, kusafisha mabanda ya mifugo, kusafisha barabara, na kadhalika. Kwanini iwe halali kufanya kazi hizo Ulaya, Marekani au Asia, lakini iwe nuksi hapa Tanzania?

Tufanye nini? Kitu cha awali kabisa naamini ni kubadili akili za watoto wetu watambue kuwa kusubiri kuajiriwa katika mazingira ya sasa ya ulimwengu uliotekwa na mashine nyingi za kisasa (teknolojia), ni kujidanganya. Kazi zilizofanywa na watu 20 leo zinafanywa na mtu mmoja au wawili! 

Pili, tuwashirikishe watoto wetu katika kuamua aina ya masomo wanayostahili kuyapata ili kuwasaidia kujenga ‘kesho’ yao. Kusoma tu kwa kufuata mkumbo, hakuna tija. 

Tatu, Serikali isione shida hata kidogo kuanzisha utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi katika vyuo vya ufundi vya VETA. Sanjari na hilo, zitengwe fedha za kutosha ili kuibua vipaji vya vijana wengi wanaofanya ubunifu wa hali ya juu katika nyanja mbalimbali. Hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na fedha za utafiti.

Tuwaombe marafiki zetu Korea Kusini watufunze namna walivyofanya mapinduzi makubwa kwenye elimu ya ufundi.

Nne, Watanzania tujifunze kutoka nje ya nchi. Twende ughaibuni ili tuweze kukamata fursa mbalimbali na faida zake zirejeshwe nyumbani. Wakenya wengi wamejikwamua kiuchumi kwa mbinu hiyo, ndiyo maana wapo wengi mno hapa nchini mwetu.

Tano, Serikali iache kuwaaminisha vijana kuwa kazi za uchuuzi au uendeshaji bodaboda zinaweza kubadili maisha yao. Kuwapa vijana pikipiki ni kuwaumiza. Vijana wanastahili wapewe matrekta, ardhi na zana mbalimbali za kuwawezesha kujiajiri. Vijana wakipata mashine za kuwawezesha kwenye useremala, watatengeneza samani nzuri zitakazouzwa katika soko la ndani hadi soko la kimataifa.

Mwisho, utajiri wa Tanzania, hasa katika ardhi, ndilo suluhisho la kweli la ajira kwa maelfu ya vijana nchini mwetu. Watu wanaohitaji chakula duniani inaongezeka. Tanzania tumejaaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, tuna mito mingi mizuri, kwanini tuamini ardhi na mito hii si kitu, lakini bodaboda ndizo zenye tija?

Vijana wetu kukosa ajira si adhabu kutoka kwa Mungu, isipokuwa ni matokeo ya kutotumia akili na rasilimali tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Wanaosubiri ajira serikalini sioni kama watafanikiwa. Tubadili akili za vijana wetu.

2427 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!