Ndugu Rais, salaam.

Utii wangu kwako hauna shaka yoyote tangu nilipokufahamu ukiwa mwanasiasa chipukizi, nami nikiwa mwandishi mchanga wa habari.

Mapenzi yako kwa Watanzania yananishawishi nivutiwe kukuita ‘Ndugu Rais’.

Ushujaa na misimamo yako si tu kwamba vilinishawishi nivutiwe na uongozi wako, bali pia vimekuwa mihimili ya imani yangu kwako kutokana na hulka uliyonayo ya kuweka maslahi ya nchi yetu mbele.

Ndugu Rais, uamuzi ulioutoa wiki iliyopita, wa kuwaruhusu wamachinga na wachimbaji wadogo kuendelea na shughuli zao, si tu kwamba ni wa kiutu, bali pia ni wa kuonesha namna unavyoguswa na maisha ya wanyonge katika Taifa unaloliongoza.

Wamachinga hawapo Tanzania pekee. Wapo Asia, Ulaya na hata katika mitaa ya Washington DC, ingawa staili yao ya uchuuzi ni tofauti kabisa na hii ya hapa kwetu.

Ndugu Rais, uamuzi wako wa kuwatetea wachimbaji wadogo, umetia fora! Kwa miaka mingi hawa wachimbaji wamekuwa ‘wanusaji’ wa yalipo madini, lakini wenye ukwasi walipobaini, waliwafurusha kama fisi wanavyofurushwa wanapozengea mawindo ya simba!

Mwishoni mwa miaka ya 1990 nilishiriki kuandika makala za makabwela wa Mirerani kunakochimbwa tanzanite! Hoja yangu ilikuwa na itaendelea kuwa tanzanite ichimbwe na makabwela Watanzania wenyewe kwa sululu. Wakati tanzanite ikiwa mikononi mwa waswahili tuliona miji ya Arusha, Moshi na mingine ya jirani ilivyostawi! Mzunguko wa fedha ulikuwa wa hali ya juu. Vijana wengi waliboresha maisha. Walipokaribishwa wageni wa Afrika Kusini, tanzanite ikawa si neema kwa wenye nayo. 

Sheria imebadilishwa. Madini ya vito kama tanzanite yanapaswa yachimbwe na Watanzania wenyewe. Hili lisimamiwe na wenye mamlaka.

Ndugu Rais, tatizo letu kubwa kwenye madini lipo katika usimamizi wa mamlaka za kodi! Pale Mirerani kunahitajika uzio ili kila wakia ya tanzanite inayochimbwa ilipiwe kodi! Hilo halifanyiki kwa sababu waliopewa kazi hiyo bado wanaamini wa kuifanya hawajazaliwa.

Wachimbaji wadogo wa madini si walipa kodi, kwa hiyo kunahitajika juhudi za makusudi za kuwafanya walipe. Mamlaka zinazohusika kuweka vituo vya kukusanya kodi, viwepo. Wachimbaji walazimishwe kulipa kodi.

Ndugu Rais, pamoja na kupongeza uamuzi wa kuwaruhusu wamachinga kuendesha biashara katika maeneo ya miji yetu, naomba utaratibu huu uwe wa mpito. Ukiachwa udumu unaweza kuwa na athari kubwa pengine kuliko faida ulizokusudia. Unaweza kuwavuta vijana wengi zaidi mijini na kuwaacha ajuza na vikongwe wakihangaika kwenye uzalishaji mali.

Kuna hatari ya kushuka mapato yatokanayo na kodi kwa sababu hata wenye maduka sasa wameamua kuwa ama wamachinga, au kuwaajiri wamachinga kuuza bidhaa zao! Hawana mpango tena wa kutumia mashine za EFD. Hawana sababu ya kulipa ushuru unaotozwa na miji, manispaa au majiji. Hii ni hatari kubwa.

Pili, utaratibu mzima wa kuishi kwa ustaarabu umevurugwa. Sehemu za waenda kwa miguu zimevamiwa na wachuuzi walioamua kupanga bidhaa kila palipo na upenyo. Juzi tu, watu wenye magari waliofika kupata mahitaji Kariakoo walinusurika kupigwa na magenge ya wachuuzi kwa sababu maeneo ya maegesho ya magari wanayahodhi. Ikumbukwe kuwa miezi kadhaa iliyopita dereva aliyepita katika barabara iliyozibwa na wachuuzi pale Kariakoo, alishushwa, akapigwa hadi akauawa. Kisa, alikanyaga fungu la bamia lililowekwa barabarani!

Ndugu Rais, kabla hujatangaza ruhusa yako kwa wamachinga, tayari Jiji la Dar es Salaam lilishakuwa uwanja wa vurugu. Kila mahali kulionekana wauza miwa, wauza karanga, wauza mahindi, wauza machungwa, wauza madafu, wauza wali na ugali, wauza mitumba, wauza mihogo na viazi, wauza sharubati, wauza saa, wauza viatu, wauza maembe na kadhalika! 

Ruhusa yako imeongeza idadi ya wachuuzi. Sasa kila mahali ni wachuuzi tu. Wachuuzi hawa wa vyakula sidhani kama wanapimwa kama kanuni za afya zinavyoagiza. Nani anaweza kuwa na hakika kama maji yaliyotumiwa kwenye sharubati yalichemshwa? Nani ana hakika miongoni mwao hawamo wagonjwa wa TB? Tunajua kustaarabika si majengo au ukwasi wa watu pekee. 

Kustaarabika kunajumuisha namna watu wa jamii husika wanavyoishi. Mgeni anapokuja nyumbani kwangu, akakuta nguo za ndani zimeanikwa sebuleni, atanitilia shaka! Mgeni anapozuru nyumba yangu, akafungua jokofu; badala ya kuona vinywaji au vyakula akakutana na soksi, atakuwa na haki ya kuhoji utimilifu wa akili yangu.

Mgeni anapofika nyumbani kwangu, akakuta wanangu wanajisaidia sakafuni barazani kwa sababu tu kuna mfanyakazi wa ndani anayelipwa kufanya usafi, atakuwa sahihi akitilia shaka akili yangu.

Tunaporuhusu kuuzwa kwa mitumba, vyakula na vitu vingine katika mazingira yasiyo sahihi, tunakuwa tunavunja moja ya misingi ya ustaarabu katika jamii yetu.

Jamii iliyostaarabika ni ile inayotenga maeneo kulingana na mahitaji. Haiwezekani shule ya awali, ya msingi au sekondari ikawa na baa au duka la kuuza vileo ndani ya eneo lake! Lakini baa au hilo duka si ajabu hata kidogo vikiwa ndani ya chuo kikuu. Tumefundishwa, tena shule ya msingi, ya kwamba kitu chochote kinachokuwa mahali ambako si pake, ni uchafu! 

Serikali inaweza kuwa na nia nzuri sana kwa ndugu zetu wamachinga, lakini matokeo ya nia hiyo yanaweza kuwa na athari kubwa zaidi.

Wananchi sharti wazoezwe kuwa wastaarabu. Hilo lilizingatiwa kwa miongo mingi na ndiyo maana moja ya kazi kuu za Serikali za Mitaa ni kutunga na kusimamia sheria ndogo ndogo zinazolenga, pamoja na mambo mengine, kulinda ustaarabu katika jamii yetu. 

Sheria ndogo ndogo zisipotiliwa maanani, hizo sheria nyingine za nchi zitapuuzwa. Sidhani kama mwananchi asiyeheshimu sheria ya kutotupa taka ovyo anaweza kuwa na uungwana wa kuheshimu sheria zinazomtaka alipe kodi.

Athari za kuruhusu wamachinga waendeshe biashara holela zinaweza kusambaa hadi kwenye makundi mengine. Waendesha bodaboda watahoji, kama wamachinga wanaachwa watambe, kitu gani cha kuwazuia wao kuendesha vyombo vyao katika upande wa barabara wanaoutaka.

Ndugu Rais, kuyasema haya si kwamba napinga huruma uliyoionesha kwa wamachinga, isipokuwa ninachosisitiza hapa ni kuwa na mpango endelevu wa kuhakikisha kundi hili la wachuuzi linakuwa na sehemu ya kudumu ya kuendeshea shughuli zake.

Tufanye nini? Mosi, tufanye kila linalowezekana kuwaaminisha vijana wa Tanzania kuwa uchuuzi si suluhisho la maisha yao. Tuwaaminishe kuwa uchuuzi na uendeshaji bodaboda ni ‘dawa ya kutuliza maumivu’, na kamwe ‘si tiba’ ya kuyaponya maisha. Na hili viongozi wetu sharti walitambue na kulisema wazi wazi kuwa nchi hii haiwezi kujengwa na vijana wauza mitumba ambayo nayo kwa bahati mbaya inazalishwa ughaibuni. 

Nguvu kazi kubwa inayotumika kwenye uchuuzi, ielekezwe kwenye uzalishaji katika kilimo na viwanda. Vijana wetu wapewe elimu ya kuwa wazalishaji badala ya wachuuzi.

Wapo waliompongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kuwezesha vijana kupata bodaboda 200. Huu si mpango wa kupongezwa. Ni ulemavu tu wa akili na kimwili kwa vijana wetu.

Tanzania tuna ardhi kubwa, nzuri na ya kutosha kwa kilimo na ufugaji. Tuna vijito, mito, maziwa na bahari vinavyoweza kutoa ajira kubwa sana kwa vijana wa Taifa hili. Tujitahidi kubadili akili za vijana wetu kuanzia kwenye aina ya elimu tunayowapa. Huu ‘ugonjwa’ wa kuamini elimu ni ya shahada, na kuamua kupuuza elimu ya vyuo vya ufundi, ni mbaya na kwa hakika unaliumiza Taifa.

Pili, alimradi wamachinga wapo na hakuna namna ya kuwapatia ajira mbadala kwa sasa, Rais achukue uamuzi madhubuti wa kutwaa maeneo fulani fulani katika miji yetu ili kujengwe majengo makubwa, ya kisasa yenye huduma zote muhimu kwa ajili yao. Rais amwagize balozi wetu aliyeko Cairo, Misri, aingie kwenye majengo ya wamachinga ili achote maarifa. Amshauri na hatimaye mradi kama huo utekelezwe hapa nchini mwetu.

Lengo la Serikali yetu liwe kuhakikisha kila mtu analipa kodi – kuanzia kwa wachuuzi hadi kwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa.

Mpango huo ulenge kuhakikisha sekta isiyokuwa rasmi inafikia hatua ya kuwa sekta rasmi. Kupigia debe informal sector maana yake ni kuwaambia Watanzania waliokuwa wameanza kupata mwamko wa kulipa kodi, wasilipe kodi. Haya yameanza kuonekana Kariakoo.

Ndugu Rais, hizi mali unazoona zikiuzwa na wamachinga, zote si za wamachinga. Zimo mali za wakubwa. Nafuu uliyowapa inaweza kuwa yenye faida kubwa zaidi kwa wale waliokuwa wakibanwa kulipa kodi awali, na sasa wakawa wanapumua kwa kujificha nyuma au ndani ya umachinga. 

Hili lipo hata kwenye bodaboda, kwani Arusha kuna mtuhumiwa wa ujangili aliyebainika kuwa na pikipiki zaidi ya 300. Kwenye mwonekano, vijana wamejiajiri; kwenye uhalisia, hao ni watumishi wa tajiri! Ukitoa unafuu, huwapi vijana 300, bali unakuwa umempa tajiri mmoja! 

Tatu, maeneo ya maegesho ya magari na ya waenda kwa miguu yaliyovamiwa na wamachinga yaachwe kwa ajili ya waenda kwa miguu na kwa maegesho ya magari.

Ndugu Rais, nimeyasema haya na kutoa ushauri kwa nia njema nikiamini ninao wajibu halali wa kufanya hivyo ili kuboresha huruma yako uliyoionesha kwa wanyonge na makabwela katika nchi yetu.

Kwa kuwa umewataka wakuu wa wilaya na mikoa watenge maeneo kwa ajili ya wamachinga, wahimize wafanye haraka. Wakichelewa, siku watakapoamua kuwahamisha, wamachinga wataona wanaonewa, na hapo huenda mitumba ikawa imeshasambazwa hadi kwenye uzio wa Ikulu. 

Mungu azidi kukupa nguvu za kukuwezesha kuwatumikia Watanzania.

By Jamhuri