DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga

Uongozi ni mchakato wa kusimamia, kuelekeza na kutoa njia zinazotakiwa kufuatwa ili kutafuta suluhu ya changamoto katika kufikia shabaha inayojengwa.

Kiongozi ni mtu mwenye jukumu la kusimamia, kuelekeza na kutoa njia zinazotakiwa kufuatwa kufikiwa malengo.

Jamii huishi kwa umoja na mshikamano kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, ukanda na ulimwengu mzima.

Katika kutatua changamoto na kutumia fursa zilizopo kuyafikia malengo ya jamii, ni vigumu

ikiwa kila mtu atafanya anavyoona au kusubiri wengine wafanye kwa niaba ya jamii.

Mfumo huu unaifanya jamii kulazimika kuwa na viongozi au watu wanaopewa mamlaka ya kusimamia, kuelekeza njia zinazotakiwa kufuatwa.

Kwa majukumu hayo, anayepewa uongozi lazima awe na sifa bora na si mtu yeyote tu, kwa kuwa uongozi ni usimamizi na udhibiti wa masuala yote yahusuyo maisha ya watu ya kila siku. Si Kila mtu anaweza kuwa kiongozi.

Baadhi ya sifa muhimu kwa kiongozi ni kuwa na uwezo wa kuongoza na kufanya uamuzi sahihi ili kuwezesha upatikanaji wa suluhu za changamoto za jamii; asiyelewa madaraka au hata dawa za kulevya.

Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi kwa kuwa mlevi anaweza kutumia madaraka kuumiza wengine, kukashifu na hata kujilimbikizia mali kwa kutumia rasilimali za umma.

Sifa nyingine muhimu mtu kuwa kiongozi bora ni yule asiyekubali mapato ya aibu, yaani rushwa, ufisadi, ubinafsi, upendeleo, ubaguzi na fursa zisizo halali. 

Hii ni sifa nyingine muhimu kwa kiongozi bora. Kiongozi si mtu yeyote tu.

Sifa nyingine ni kutokuwa na ‘ndimi mbili’ (kigeugeu).

Mwenye ndimi mbili hutafsiriwa kama mtu asiye na msimamo kwa anachokisimamia, ni mtu anayebadilikabadilika, anakosa mwendelezo wa hoja zake, hivyo hupoteza mwelekeo wa jamii kwa kuwaweka watu katika wakati mgumu kufuata kila anakotaka waelekee kadiri anavyobadilika.

Kiongozi bora anapaswa kuwa mkweli, mtu asiye mnafiki, anayeweza kusimama katika misingi anayoiamini bila kununuliwa au kutumiwa na wenye nguvu kupitisha mambo kwa masilahi yao.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliamini kuwa viongozi bora huandaliwa na katika kipindi cha utawala wake, alihamasisha ujenzi wa vyuo vya utumishi wa umma na aliishi katika falsafa kuwa kiongozi lazima awe yule anayekerwa na ubaguzi wa aina yoyote.

Mwalimu alisisitiza kuwa kiongozi lazima awe na uwezo, awe anakerwa na mambo yote yanayokwaza masilahi ya jamii.

“Kiongozi ni lazima awe na uwezo, awe ni mtu anayekerwa na rushwa na aonekane hivyo kutoka ndani ya moyo wake,” anasema Mwalimu Nyerere alipokuwa akihutubia moja ya mikutano mikuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kukomesha ubaguzi, Mwalimu alifuta tawala za kikanda (uchifu) na kuanzisha mfumo wa kitaifa ambapo watu wote walikuwa na sifa ya kuteuliwa au kuchaguliwa kuwa viongozi mahali popote ndani ya nchi na akaanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kujenga jamii ya kidemokrasia, ambapo madaraka ya nchi yatakuwa mikononi mwa wananchi wenyewe.

Katika kuenzi tunu hizi, kiongozi bora anatakiwa apatikane kwa uwezo wake katika masuala ya uongozi na si vinginevyo.

Mtu hatakiwi kupata au kukosa uongozi kutokana na jinsia yake, kipato chake, kabila lake, dini yake, anakotoka au umaarufu alionao.

Mtu kuzaliwa mwanamume si sifa ya kuwa kiongozi bora, kuwa mwanamke si kigezo cha kuombea kura ya uongozi, kuwa maskini si mkosi wa kuondoa sifa ya kuwa kiongozi, kuwa wa dini fulani si sifa ya kuwa kiongozi bora wala kuwa kabila fulani si sifa ya kuwa kiongozi bora.

Ni mawazo mfu yanayoishi katika fikra za wabaguzi, wanasiasa waliofilisika hoja kuwa mtu anaomba kura kwa kujificha katika kundi fulani la jamii.

Kuomba kura kwa kujificha katika dini, jinsia, kabila, utajiri au kutumia umaarufu ni umaskini wa kidiplomasia.

Hata katika nafasi za uteuzi, mtu kuwa maarufu si sifa ya kuwa kiongozi bora.

Kumteua mtu kwenye uongozi kwa sababu ni mwanariadha anayejulikana sana; kwamba ana kasi sana uwanjani, au kwa kuwa ni mrembo anayepigiwa kura mitandaoni na kupata mashabiki, au ni mwimbaji wa nyimbo za aina fulani, kuiona kuwa hiyo ni sifa ya kuwa kiongozi bora ni umaskini wa kidiplomasia unaozorotesha maendeleo ya jamii kwa watu wasio na maarifa kupewa nafasi za kuwa waamuzi wa masuala ya jamii huku wenye sifa wakiachwa nje ya mifumo, wabaki kulalamika na kukosoa mambo yanayofanywa na watu wasio na uwezo waliopewa nafasi.

Hii imesababisha wimbi la uwepo wa viongozi wasio na maadili, viongozi wasio na unyenyekevu kwa wananchi, wababe, wenye kejeli na kauli za kihuni. 

Ni kwa sababu tunawachagua kwa kuangalia sifa za ajabu.

Mwalimu Nyerere aliamini kuwa ofisi ya umma (Ikulu) ni mahali patakatifu, si pango la wahuni kwenda kufanya mambo ya ajabu ajabu.

“Ikulu ni mahali patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza kuwa pango la walanguzi,” hii ni kauli ya Mwalimu Nyerere inayotoa maadili kwa kiongozi wa umma anayemiliki ofisi ya umma kuwa ni lazima awe mtu mwenye maadili na sifa zinazotakiwa.

Wapiga kura, wagombea wa nafasi za uongozi na wateuaji wa viongozi ni vema wakajikita katika kutathmini sifa za uongozi bora katika kufanya uamuzi wa kupata viongozi ili kuondokana na ombwe linalosababishwa na viongozi wa ajabu wanaodidimiza maendeleo ya jamii.

0689990248

[email protected].

By Jamhuri