DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita kulifanyika hafla ya utoaji wa tuzo mbalimbali kwa wanasoka na wadau wengine wa michezo waliofanya vizuri katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/2021.

Hafla hiyo ya kuvutia ilifanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Wadau wa michezo kutoka kona mbalimbali za Tanzania wametofautiana kimaoni na hata kimtazamo kuhusu uandaaji wa sherehe, utoaji tuzo na hata uvaaji wa baadhi ya washindi wa tuzo hizo.

Wapo waliokosoa wakihoji sababu za kipa bora wa msimu huo, Aishi Manula, kupewa tuzo na mtu asiyeendana naye.

“Kipa bora angezawadiwa na mmoja wa makipa wakongwe kama Mohamed Mwameja, Idi Pazi au Juma Pondamali,” anasema mfuatiliaji mmoja wa soka kutoka mkoani Kigoma.

Wakosoaji wengine wanasema tuzo ya mhamasishaji bora haikupaswa kumshirikisha shabiki mkuu wa Taifa Stars, Bongo Zozo, kwa kuwa yeye hajihusishi na Ligi Kuu Tanzania Bara au Kombe la Shirikisho (ASFC).

Bongo Zozo, raia wa Uingereza mwenye mapenzi makubwa na Taifa Stars, ametwaa tuzo ya mhamasishaji bora akiwashinda watu kama Haji Manara wa Yanga aliyefanya kazi hiyo kwa kiwango kinachoonekana kama ni cha juu alipokuwa na Simba’ pamoja na Antonio Nugaz aliyekuwa Yanga.

Mitandaoni nako kukachafuka kwa vichekesho vya hapa na pale vikihusisha uvaaji wa suti wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga.

Lakini kwa ujumla mashabiki na wadau wengi wa soka wameridhishwa na kazi pamoja na maandalizi ya utoaji tuzo huo na hata kwa washindi kadhaa, isipokuwa tu kukosekana kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Louis Miquissone, aliyeng’ara msimu huo lakini hakuambulia chochote.

Mchezaji huyo raia wa Msumbiji kwa sasa anachezea Klabu ya Al Ahly ya nchini Misri.

Katika hafla ya wiki iliyopita Simba walipewa mfano wa hundi ya Sh milioni 100 kama zawadi ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo, huku nyota wake kadhaa wakiondoka na tuzo katika nyanja mbalimbali.

John Bocco, Nahodha wa Simba, ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita huku Fei Toto wa Yanga akishinda tuzo kama hiyo upande wa ASFC.

Katika sherehe za utoaji tuzo hizo zilizofanyika JNICC, Bocco amewashinda aliyekuwa mchezaji mwenzake katika Klabu ya Simba, kiungo raia wa Zambia, Clatous Chota Chama ambaye kwa sasa anachezea Klabu ya RS Berkane ya Morocco, pamoja na kiungo wa Yanga, Tonombe Mukoko raia wa DRC.

Kwa upande wa Fei Toto kwenye mashindano ya ASFC, amewashinda Bocco na kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Miquissone aliyekuwa Simba kabla ya kuhamia Al Ahly ya Misri.

Golikipa anayeaminika kuwa katika kiwango cha juu zaidi kwa sasa nchini, Aishi Manula wa Simba, amebeba tuzo zote mbili; yaani Kipa Bora wa Ligi Kuu na Kipa Bora wa ASFC, akiwashinda Jeremiah Kisubi aliyekuwa Tanzania Prisons kabla ya kuhamia Simba na Haroun Mandanda wa Mbeya City kwenye Ligi Kuu.

Katika ASFC Aishi amewashinda Faroukh Shikhalo, raia wa Kenya aliyekuwa akiichezea Yanga kabla ya kuhamia KMC na Cleo James Ssetuba, raia wa Uganda anayechezea Biashara United.

Mlinzi wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameshinda Tuzo ya Beki Bora wa Ligi Kuu mbele ya mchezaji mwenzake wa Simba, Shomary Kapombe na Dickson Job wa Yanga.

Mshambuliaji Abdul Suleiman ‘Sopu’ wa Coastal Union ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi dhidi ya Job wa Yanga, Lusajo Mwaikenda wa KMC na Deogratius Mafie wa Biashara United.

Simba, mabingwa mara nne mfululizo, wametoa pia Kocha Bora wa Ligi Kuu ambaye ni Mfaransa Didier Gomes, akiwaangusha George Lwandamina raia wa Zambia anayeifundisha Azam FC na raia wa Kenya, Francis Baraza, aliyekuwa akiifundisha Biashara United kabla ya kuhamia Kagera Sugar.

Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Soka kwa upande wa wanawake ni Amina Bilal aliyewashinda mchezaji mwenzake wa Yanga Princess, Aisha Masaka na Oppah Clement wa Simba Queens.

251 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!