TABORA

Na Moshy Kiyungi

Baadhi ya wanamuziki wa Orchestra Baba Nationale ‘walichomoka’ baada ya kutokea kutoelewana kati yao na uongozi, wakaunda kikosi cha Les Mangelepa.

Hiyo ilikuwa ni Julai 1976, wakiongozwa na Bwammy Walumona ‘La Capitale’, wakimuacha Ilunga Omer Ilunga ‘Kamanda wa Kamanda’ maarufu kwa jina la Baba Gaston, akiendelea kuiongoza Orchestra Baba Nationale.

Baba Gaston ndiye mwanamuziki wa kwanza kutoka DRC kuweka makazi Afrika Mashariki mwanzoni mwa miaka ya 1970, akiweka makazi yake Dar es Salaam kwa miaka minne.

Baadaye yeye na bendi yake wakahamia Nairobi, Kenya ambako walipiga muziku mkubwa uliokidhi kiu ya wapenzi na mashabiki wa muziki wa rhumba.

Pamoja na sifa alizojizolea, ni ubovu wa uongozi wake ndio ulisababisha wanamuziki kadhaa kumkimbia na kuunda Les Mangelepa.

Muziki wa kundi hili jipya uliwakuna na kuwagusa vijana wengi wa wakati huo waliokuwa wakihudhuria maonyesho yao kwenye kumbi za Nairobi Park, Garden Square, Tents Club na Park Inn jijini Nairobi.

Les Mangelepa ilisheheni wanamuziki kutoka DRC, mbali na kiongozi wao, Le Capitale, walikuwamo akina Kabila Kabanze ‘Evani’ aliyeongoza safu ya uimbaji iliyoundwa na Kalenga Nzaazi ‘Vivi’, Lutulu Kaniki ‘Macky’ na Babibanga Watshilumba ‘Kai’.

Tarumbeta ilipulizwa na Mwepe Mutshi ‘Cavalou’ huku Kai akimsaidia mara kadhaa kwenye tarumbeta na ‘trombone’.

Gitaa la besi lilikuwa likiungurumishwa na Kasongo Fundi ‘Petit Jean’; Lukangika Maindusa ‘Moustano’ akicharaza magitaa ya solo na rhythm, wakati Lumwanga Mayombo ‘Ambassador’
akishikilia mipini ya besi na rhythm pia.

Drums zilichanganywa na Mukala wa Mulumba ‘Bebe’; Tabu Ngongo Ildephonce ‘Super Sax’ na Tshimanga Zadios walikuwa wakipuliza saksafoni.

Kinanda kilikuwa kikipapaswa na na akina Twikale wa Twikale na Kabe Kimambe ‘Elombe’. 

Wanamuziki wengine wa kundi hilo ni akina Kabebe Mukangwa ‘Picolo’, Tambwe Lokasa, Mukala Kanyinda ‘Coco’ na Padd ‘Mawauwau’.

Bendi ya Les Mangelepa ilijipatia umaarufu mkubwa miaka ya 1970 hadi 1980 baada ya kufyatua nyimbo zilizowakuna wapenzi wa muziki wa dansi Afrika ya Mashariki na Kati.

Baadhi ya nyimbo hizo ni Embakasi, Maindusa, Walter, Safari ya Mangelepa, Odesia, Dracula, Saad, Maboko Pamba na nyingine nyingi.

Juhudi zao ziliibua ushindani mkubwa dhidi ya bendi kubwa zilizokuwapo Nairobi, huku mashabiki wakidiriki kutamka kwamba Les Mangelepa hawana mpinzani miongoni mwa bendi zilizokuwa zikipiga muziki nchini Kenya.

Bendi zilizoonekana kuzimishwa na Les Mangelepa ni Les Knoirs, Les Wanyika, Orchestra Shikashika, Orchestra Virunga, Super Mazembe na Baba Gaston mwenyewe na bendi mama ya Mangelepa; Baba Nationale.

Baada ya ‘kulewa’ sifa na umaarufu, Les Mangelepa ikaingia kwenye mtafaruku mkubwa wa uongozi, wanamuziki wakaamua kubadili uongozi, ambapo Kabila Kabanze akawa kiongozi wa bendi.

Chini ya uongozi wa Kabanze, bendi ikafanikiwa kurejea kwenye umaarufu iliokuwa nao awali. 

Mwaka 1986, Bammy Walumona aliondoka katika bendi hiyo na kuokoka, akiicha Mangelepa ikiwa imesheheni
wanamuziki wengi wenye vipaji vikubwa waliotunga na kuimba nyimbo nyingi zenye mvuto, hivyo kushika chati katika kumbi za burudani na maeneo ya starehe ya miji mingi ya Kenya na Afrika Mashariki.

Wimbo wa ‘Embakasi’ na ‘Kanemo’ zilitungwa na mwanamuziki Kalenga Nzaazi ‘Vivi’; nyimbo za ‘Mimba’ na ‘Nyako Konya’ zilitungwa na Badi wa Tshilumba na hadi leo bado zinatamba.

Wimbo wa ‘Maindusa’ ni utunzi wa Lukangila Maindusa, wakati wimbo wa ‘Malawi’ ulitungwa na mwanamuziki Kabila Kabanze ‘Evani’ na ‘Walter’ uliotungwa na Badi Banga wa Tshilumba. 

Baadaye wakafyatua albamu nyingine yenye nembo ya Madina, ikiwa na nyimbo za Madina, N’kimba, Lolo Mukena na Kawala.

Les Mangelepa itakumbukwa na mashabiki wa muziki wa Zambia ambako ilifanya ziara na kutoa burudani ya kihistoria. Waliporudi nyumbani Kenya, wakatunga wimbo ‘wa shukrani’ ulioitwa Safari ya Zambia, ukipigwa kwa ala tupu.

Ikiwa na mtindo wa ‘Chafua Chafua’ mwaka 1978, bendi hiyo ilirekodi santuri zenye sehemu ya kwanza na ya pili za ‘Pambana pambana’ pamoja na ‘Haleluya’. 

Nyingine zilikuwa ni Dracula, Mangelepa Kamili, Kizunguzungu, Suzanne na Trouble.Kwa sasa bendi hiyo haipo tena katika taswira ya muziki na baadhi ya wanamuziki wake wamekwisha kutangulia mbele ya haki, huku wengine wakiokoka na kuachana na muziki wa kidunia.

Mwisho.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali na mwandishi wake akipatikana kwa namba za simu: 0784 331 200, 0767 331 200, 0713 331 200 na 0736 331 200.

320 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!