Hali inaonesha kwamba wasanii wa Tanzania wamekuwa wadau wakubwa katika mzunguko wa biashara ya dawa za kulevya.

Hivi karibuni kumekuwa na habari mbalimbali kupitia vyombo vya habari zinazoonesha jinsi wasanii wa Tanzania wanavyoshiriki katika usafirishaji wa dawa za kulevya.

 

Mbali ya wanaoshiriki katika uuzaji na usafirishaji, kuna wale ambao wameamua kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo zenye athari kubwa.

 

Kuna waliokubali kuacha kutumia dawa hizo na wapo wanaoendelea kuzitumia kana kwamba hawajaona madhara yake.

 

Suala la matumizi ya dawa za kulevya halina kificho. Kwa wale waliozoea kujichanganya katika maeneo mbalimbali ni rahisi kumgundua mtu anayetumia dawa hizo.

 

Mtu anapoanza kutumia dawa hizo kuna dalili ambazo hazijifichi ili kumtambua. Kwa mfano, hivi karibuni msanii wa muziki kutoka Tanzania, Agnes Gerald ‘Masogange’ (25) akiwa na Melisa Edward (24) waliripotiwa kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8 za Tanzania.

 

Kukamatwa kwa Masogange kumeambatana na habari nyingine zilizowahusisha wasanii wengine wa muziki wa kizazi kipya ambao pia wamehusishwa na biashara hiyo.

 

Baadhi ya vyombo vya habari vimetoa habari kuhusu mwanamuziki Naseeb Abdul, maarufu kama ‘Diamond’ wa jijini Dar es Salaam kuhusishwa na biashara hiyo.

 

Ni kwa muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa za Diamond kujihusisha na biashara hiyo hasa kutokana na ukaribu wake na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini Afrika Kusini.

 

Taarifa kupitia mitandao mbalimbali zinasema ni wafanyabiashara hao ndiyo waliohusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa marehemu msanii Albert Mangwair, aliyefia nchini Afrika Kusini takriban miezi mitatu iliyopita.

 

Taarifa za kifo chake ziligubikwa na matumizi ya dawa za kulevya. Mangwair aliambatana na msanii mwenzake maarufu kwa jina la M2theP ambapo taarifa zilisema kwamba mpaka Mangwair anakata roho M2theP alikuwa hoi akiwa hajitambui.

 

Juni, mwaka huu msanii mwingine wa muziki wa Hip Hop Langa Kileo, maarufu kama ‘Langa’ aliaga dunia.

 

Katika uhai wake Langa alikiri kupitia baadhi ya vyombo vya habari ya kuwa alipata kutumia dawa za kulevya na kuahidi kuachana nazo.

 

Pamoja na kutangaza kuachana na matumizi ya dawa za kulevya, baada ya kifo chake kuna baadhi ya wadau wa muziki waliodiriki kusema kuwa dawa za kulevya zilichangia kusababisha kifo cha msanii huyo.

 

Wakati hayo yakiendelea, hivi karibuni msanii wa muziki wa kizazi kipya, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ameibuka na kusema kwamba kuna idadi kubwa ya wasanii wa Tanzania wanaotumia dawa za kulevya.

 

Ray C ambaye alipata kutumia dawa hizo kwa sasa ameacha na anapata tiba ya ushauri nasaha dhidi ya matumizi ya dawa hizo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

Ray C alidiriki kusema kuwa watu wengi wameathirika vibaya na dawa za kulevya akisema kuna idadi kubwa ya wasanii anaowafahamu kuwa wanatumia dawa hizo.

 

Inahitajika nguvu ya pamoja kwa wasanii wa Tanzania kutambua madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

 

Huu ni mlolongo wa baadhi ya matukio yanayowahusisha wasanii wa muziki wa Tanzania kuhusu suala zima la dawa za kulevya.

 

Kuna haja ya wasanii kuweka nguvu ya pamoja ya wasanii kupiga vita mtandao wa dawa za kulevya ambao unatia aibu nchi yetu.

 

By Jamhuri