DODOMA

Na Javius Byarushengo

Chakula hata kiwe kitamu kiasi gani, kikiliwa kwa muda mrefu, tena mfululizo, hukinai na kuhitaji chakula kingine.

Wali ni chakula kikuu Tanzania na kinapendwa na wengi, lakini ajabu ni kwamba wali ukiliwa mfululizo asubuhi, mchana na usiku kwa siku saba, utajikuta unatamani kula chakula kingine kabisa.

Mfumo huu wa kimaumbile kwa binadamu ni sawa na ilivyo hata katika masuala mengine, ikiwamo siasa.

Ni ukweli usiopingika kwamba ukizungumzia miongoni mwa vyama bora, tena vyenye historia ndefu Afrika, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikosekani.

Ni chama chenye vimelea vya vyama vilivyopigania uhuru; TANU ikiwa upande wa Tanganyika (Tanzania Bara) na ASP upande wa Zanzibar.

Ni CCM chini ya viongozi mahiri; Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume wa ASP, imeweza kuunda taifa imara lenye umoja usio na chembechembe za ukabila, udini, urangi na ukanda.

CCM imefanikiwa kulifanya taifa kuendelea kuitwa kisiwa cha amani licha ya kupitia changamoto mbalimbali zikiwamo za kiuchumi.

Licha ya mafanikio yote haya yaliyofanywa na CCM, bado wananchi wenye mtazamo na fikra tofauti wakiwa tayari kutaka mabadiliko,  wamekuwa wakiongezeka kadiri miaka inavyosogea.

Hebu tuchungulie baadhi ya matishio ya wananchi kutaka vyama vingine vitawale badala ya CCM.

Tishio la kwanza lilikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, ambapo hali ya CCM ilikuwa tete hadi Mwalimu Nyerere kuacha shamba lake Butiama na kuingia mitaani kupiga kampeni kunusuru chama kisife akingali hai.

Ikumbukwe mwaka huo chama kikuu cha upinzani kilikuwa NCCR-Mageuzi chini ya mgombea wake, Augustine Mrema, ilhali CCM ikiwa na Benjamin Mkapa kama mgombea wake.

Ni dhahiri katika uchaguzi huo Mrema kwa kutumia kete ya kazi alizozifanya akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani; kupambana na ujambazi, rushwa na mambo mengine, alikuwa kivutio kwa wananchi waliokuwa wakilisukuma gari lake la kampeni kila alikokwenda.

Inasemekana kama si jitihada za Mwalimu kuwaaminisha wananchi kwamba CCM bado ndicho chama pekee kinachofaa kuongoza, huenda taifa lingekuwa na historia nyingine.

 Tishio la pili lilikuwa ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambapo mgombea wa chama tawala, Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa akigombea kumalizia awamu yake ya pili ya uongozi.

Katika uchaguzi huo upinzani mkubwa ulitoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya mgombea Dk. Wilbroad Slaa.

Dk. Slaa alitumia kete ya rushwa, ufisadi na kujilimbikizia mali ambavyo vilionekana kukithiri katika serikali ya Kikwete, hivyo kujiongezea imani kwa Watanzania waliotamani mabadiliko ya uongozi.

Ilifanyika nguvu ya ziada kutoka kwa viongozi waandamizi ndani ya chama na serikali kuzunguka nchi nzima kujenga matumaini mapya kwa wananchi kwamba bado CCM inahitajika kuliongoza na kulisimamia taifa.

Dk. Kikwete akashinda kwa asilimia zilizoshuka ukilinganisha na mwaka 2005.

Tishio la nne lilikuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wa uongozi, CCM ikakumbwa na matukio kadhaa yakiwamo ya ubadhirifu na uzembe kwa watumishi wa umma hivyo kujiweka njia panda.

Si tu kujiweka njia panda, bali pia kutokana na baadhi ya wanachama  waandamizi kukumbwa na ulafi wa madaraka, chama kilijikuta kikiangukia katika makundi.

CHADEMA chini ya mgombea wake, Edward Lowassa akitokea CCM baada ya kubwagwa katika mchakato ndani ya chama, alitoa upinzani mzito kwa mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli licha ya kubebwa na historia ya uchapakazi kutokuwa na makundi ndani ya chama.

Ilitumika nguvu ya ziada kumnadi kwa wananchi; kazi kubwa ikifanywa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wakati huo, Nape Nnauye.

Tishio la tano ni katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo mgombea wa CCM Dk. Magufuli aligombea awamu yake ya mwisho.

Licha ya Dk. Magufuli kuonekana amefanya mambo makubwa ndani ya miaka mitano ya uongozi, ikiwamo ujenzi wa miundombinu na mapambano dhidi ya uzembe kwa watumishi wa umma bila kusahau vitendo vya ubadhirifu, bado alipata upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.

Upinzani huo ulitokana na wananchi waliokuwa wakidai  kuchoshwa na kukosa uhuru wa kujieleza, huku watumishi wa umma wakilia kutokana na kutopandishiwa mishahara kwa muda mrefu.

Hata hivyo, mgombea wa CCM aliibuka kidedea kwa kura nyingi, kitendo kilichoacha watu vinywa wazi. 

Yote kwa yote, matishio haya hakuna hata moja limeweza kuiondoa CCM. Hii ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kimfumo na migogoro isiyokwisha ndani ya vyama vyenyewe vya upinzani.

Vyama hivi licha ya uwepo wake kwa takriban miaka 29 sasa huku zikifanyika chaguzi kuu zipatazo sita, bado vimeshindwa kuungana na kuwa chama kimoja chenye nguvu, tena chenye kumsimamisha mgombea mmoja.

Kugombania mkate ndani ya vyama na baadhi ya viongozi wakuu kuendelea kuwa wafalme kwa kuzikanyaga katiba zao ni miongoni mwa mambo ambayo yameendelea kuvitafuna vyama.

Nani hakumbuki mgogoro uliojitokeza ndani ya NCCR-Mageuzi na kusababisha Mrema kutimkia TLP?

Nani hakumbuki Zitto Kabwe alivyoanzisha ACT- Wazalendo baada ya kutimuliwa Chadema kwa kilichoitwa usaliti kwa kitendo chake cha kukinyemelea ‘kiti cha ufalme’?

Je, ni nini kilisababisha Maalim Seif Sharif Hamad aitose CUF aliyosaidia kuiasisi mwenyewe?

Yuko wapi mwanasiasa na mpinzani mkubwa mwenye haiba ya pekee, Dk. Slaa?

Je, vipi kuhusu mgogoro unaoendelea kuyatafuna masalia ndani ya CUF inayochechemea?

Katika muktadha huo, ninathubutu kusema itakuwa vigumu kwa vyama vya upinzani vyenye upinzani na ulafi ndani yake kukiangusha chama tawala kilichokaa madarakani kwa muda mrefu huku kikiwa na mbinu na mikakati mikubwa bila kusahau nguvu ya rasilimali fedha.

[email protected], 0756521119

By Jamhuri