*Vikumbo vyaanza uchaguzi NEC-CCM

*Matayarisho ya mitandao yapamba moto

*Sura mpya, waliopotea waanza kuibuka

*Kipimo cha kukubalika ni kwenye NEC

Harakati za kuwania nafasi mbalimbali, hasa ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimetafsiriwa kwamba ni maandalizi ya kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Rais Jakaya Kikwete hataruhusiwa tena kuwania kiti hicho baada ya kuwa ametumikia mihula miwili ambayo ndiyo ukomo kikatiba. Mwaka huu ndiyo wa uchaguzi wa ngazi zote – Shina hadi Taifa – ndani ya CCM. Kujitokeza kwa wanasiasa walioonekana kupumzika kwa miaka kadhaa sasa, kunazidi kuibua mikakati ya kuandaliwa kwa mitandao ya kuwania urais kwa mwaka huo.

 

 

Wanasiasa wafanyabiashara matajiri kama Nazir Karamagi na Anthony Diallo kujitokeza kuwania nafasi za juu ndani ya chama hicho, kunatajwa kama mwanzo wa harakati za kujipanga upya kisiasa kuelekea mwaka 2015. Ingawa wenyewe wanaweza wasiwe na nia ya kuwania urais, ushawishi wao bado ni muhimu kwa yeyote atakayetaka kupata kura za kutosha kutoka kwa wajumbe wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa.

 

Diallo anakumbukwa ndani ya CCM kwa mchango wake mkubwa mwaka 2005 alipoamua kutumia vyombo vyake vya habari kufanikisha kampeni za chama hicho. Pamoja naye, kuna wafanyabiashara wengine maarufu kama Mwita Gachuma, Lameck Airo na wengine ambao ni makada wa chama hicho.

 

Kumekuwa na taarifa kwamba kwa mara ya kwanza uchaguzi wa NEC wa mwaka huu utaweza kupata sura mpya ambazo “hazikutarajiwa”. Imani iliyojengeka ni kwamba ili mwanachama aweze kufanikiwa kuteuliwa kuiwakilisha CCM au aweze kuhakikisha ushindi kwa mgombea urais anayemtaka, ni vema akawa mjumbe wa NEC.

 

Kuwa mjumbe wa NEC kunasaidia mgombea au wapambe wa mwanachama anayeomba ridhaa ya kukiwakilisha chama katika nafasi ya urais, kuwa karibu na waamuzi muhimu ambao ni wajumbe wa NEC. Katika NEC ndimo mnamopatikana pia wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ambayo ndiyo chujio la awali.

 

Wanaotajwa kuwania urais

Wanachama wengi wa CCM wanatajwa kuwa na nia ya kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa rais mwaka 2015. Miongoni mwao ni wale walioshindwa na Kikwete mwaka 2005 na wengine ni wapya kabisa.

 

Mbunge wa Mtama, Bernard Membe, ametangaza kwamba hatagombea ubunge mwaka 2015. Membe ameithibitishia JAMHURI katika mahojiano maalumu, akisema kutogombea kwake ubunge ni utekelezaji wa ahadi yake ya muda mrefu, kwani alisema baada ya vipindi vitatu, hataendelea. Hata hivyo, uamuzi huo unaweza kutafsiriwa na wengi kuwa ni maandalizi yake ya kuwania nafasi ya juu zaidi, yaani urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Lakini mwenyewe anasema amelitumikia taifa kwa muda mrefu katika nafasi mbalimbali, hivyo kutogombea kwake ubunge kumelenga kumpa nafasi ya kukaa na familia, na ikiwezekana kuanza kuandika masuala aliyofanya kitaifa na kimataifa.

 

Alipoulizwa kama lengo lake ni kujiandaa kuwania urais, alisema, “Kwa sasa ni mapema, ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba nilishatoa ahadi ya kuwatumikia wananchi wa Mtama kwa vipindi vitatu, sasa vimetimia, na lazima niheshimu ahadi yangu.”

 

Anasema kwa sasa nguvu zake amezielekeza katika kumsaidia Rais Jakaya Kikwete, ili aweze kumaliza vema ngwe yake ya uongozi. “Sipo tayari kulizungumza jambo hilo (kuwania urais) kwa sasa…kwa kweli nipo bize sana kumsaidia Mheshimiwa Rais Kikwete amalize ngwe yake ya uongozi.

 

“Hiyo ndiyo ‘priority’ (kipaumbele) yangu ya kwanza, hiyo ndiyo ‘priority’ yangu ya pili na kwa kweli hiyo ndiyo ‘priority’ yangu ya tatu…kumsaidia amalize ngwe yake salama,” alisema.

 

Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta (CCM), naye ameweka bayana kwamba hatagombea urais mwaka 2015. Lakini watu walio karibu naye wanasema bado anamini ana sifa na uwezo vinavyomwezesha kushika nafasi hiyo. Wanasiasa wengine ndani ya CCM wanaotajwa kujiweka tayari kuwania urais mwaka 2015 ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anayetajwa kuwa na mtandao mpana na wenye nguvu.

 

Lowassa aliyejizulu nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 kwa kashfa ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, hajataja waziwazi nia yake ya kuwania kiti hicho, lakini anatajwa kama mmoja wa watu wanaoitaka nafasi hiyo.

 

Hata hivyo, fursa ya kuiwakilisha CCM inakabiliwa na mtihani mgumu, hasa kutokana na mambo yanayoendelea ndani ya CCM yanayoonekana dhahiri “kudhibiti watu”, badala ya kukabiliana na changamoto. Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa walengwa wakuu.

 

Hakuna shaka kwamba kuna wanachama na wafuasi wengi ndani na nje ya CCM wanaomuunga mkono Lowassa kichinichini, na hao ni wale wanaoamini kuwa akiwa rais anaweza kuleta mabadiliko makubwa, hasa katika uwajibikaji. Swali lililopo ni je, walioongoza mpango wa kumwengua mwenye uwaziri mkuu watamwacha apite?

 

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, anatajwa kama miongoni mwa wanaofaa kuiwakislisha CCM kwenye kinyang’anyiro cha urais. Anajulikana kama mmoja wa mawaziri wachapaji kazi ambao CCM imepata kuwa nao. Hana mtandao mpana ndani ya CCM pengine kutokana na msimamo wake wa kutotaka kuwania nafasi yoyote.

 

Kwa dhana ya “maamuzi magumu”, Dk. Magufuli anaonekana kufaa hasa wakati huu ambao Serikali inalalamikiwa kwa kuacha mambo mengi yajiendeshe na kujimaliza yenyewe. Walio karibu naye wanahofu kuwa huenda asiwe rais mzuri kutokana na ukali uliopindukia, na kufuata sheria.

 

Mbunge wa Rungwe Mashariki ambaye ni Waziri Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, ni miongoni mwa wanaotajwa kuwania urais. Anajivunia rekodi yake ya mwaka 2005 alipoweza kuwa miongoni mwa wana-CCM watatu walioingia fainali na hatimaye wakashindwa na Jakaya Kikwete.

 

Pamoja na afya yake kutetereka, bado hajatangaza hadharani kama hana mpango wa kuwania kiti hicho, hasa baada ya kuona ameanza kutengemaa. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, naye yumo kwenye kundi la wanaotajwatajwa kuwania urais.

 

Kwa kutumia kigezo cha jinsi, anaelezwa kama mmoja wa watu wanaotakiwa na Rais Kikwete wawe warithi wake.  Safari zake za mara kwa mara hapa nchini na ushiriki wake kwenye masuala mengi ya kijamii (wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), vinachukuliwa kama viashiria vya kuitaka nafasi hiyo.

 

Pamoja na ‘mtaji’ wa jinsi, anajivunia rekodi nzuri ya kuwa na weledi wa hali ya juu kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa kabla ya wadhifa huo mkubwa, amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ni miongoni mwa wanaowekwa kwenye orodha ya wanaoweza kuwania na hata kushinda kiti hicho. Anabebwa na historia yake njema ya uongozi, na kwa sasa anaonekana kukomaa zaidi. Dk. Shein, aliyepata kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka mingi, anao uzoefu wa kutosha wa kuweza kuhimili siasa za Tanzania.

 

Nafasi yake ya kuwania kiti hicho inapaliliwa zaidi na nadharia isiyo ya kikatiba ya kuona kuwa pande zote mbili za Muungano zinakuwa na utaratibu wa kutoa rais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kigezo hicho, hata Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, naye anaingizwa kwenye orodha ya wanaoweza kujitokeza kuwania kiti hicho. Licha ya kuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka 10 kwa mujibu wa Katiba, bado hafungwi kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, si wa kubeza hasa kutokana na uzoefu wake kama Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadaye waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Amethubutu kuwania urais wa Zanzibar, ingawa “kura hazikutosha”. Kwa kigezo cha kuwa na rais anayetoka Zanzibar, kama Muungano utaendelea kuwa imara, nafasi yake si haba. Kutoka Visiwani, washindani wengine wanaweza kuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, na Dk. Hussein Mwinyi.

 

Ukiacha suala la umri kwa Dk. Bilal, Dk. Mwinyi anaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwania urais. Kwenye orodha hii wapo wana-CCM wengine ambao ingawa wanaonekana kuwa kimya, bado wanaweza kuleta ushindani mkali.

 

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, anayeshikilia rekodi ya kushika nafasi hiyo kwa muda mrefu zaidi – miaka 10 – anatajwa na walio karibu naye kwamba anataka kuwania kiti cha urais mwaka 2015. Uamuzi wake wa kwenda Hanang’ kuwania ujumbe wa NEC kunaelezwa kwamba ni mpango wake wa kumweka karibu na wana-CCM ili mwaka 2015 aweze kufanikiwa. Pia, kauli zake za kukosoa baadhi ya mambo ndani ya chama kunachukuliwa kama uthibitisho wa mpango huo.

 

Mwingine anayetajwa ni Dk. Abdallah Kigoda ambaye mwaka 2005 alishiriki na kukawapo maneno kwamba alikuwa chaguo maridhawa la Rais na Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo, Mzee Benjamin Mkapa. Kurejeshwa kwake katika Baraza la Mawaziri kunaelezwa kama ni kumsaidia kusafisha njia ya kuwania nafasi hiyo ya uongozi kubwa kabisa katika Taifa letu.

 

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ingawa mara zote amesema kazi ya urais ni ngumu na asingependa kubebeshwa mzigo huo, anaweza kubadili mawazo na kuamua kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, upole wake na kutokuwa na jeuri ya kuchukua “maamuzi magumu” kunaweza kumfanya aonekane kuwa mwepesi mbele ya wagombea wengine, hasa wa upinzani.

 

Lakini kundi jingine la “hawavumi lakini wamo” ni la wana-CCM vijana. Miongoni mwao ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na wengine kadhaa.

 

 

1266 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!