Mara nyingi nimesema kwamba kuna watu wanaofanya siasa wakijiita wanasiasa wakati hawaelewi chochote kwenye siasa! Hawa wanaonyesha kuwa hawapo mahali sahihi. Inawezekanaje mtu ajiite mwanasiasa wakati haelewi siasa ni kitu gani?

Wanachofanya hao ni kutafuta masilahi kwa ajili ya kuendesha maisha binafsi lakini siyo siasa. Kwa mfano, kipindi hiki kuna wimbi la baadhi ya watu kuhama vyama vya siasa, hususan vya upinzani kwenda Chama tawala, CCM. Ni mtindo ambao umeota mizizi, huku watu, hasa Wana CCM, wakishangilia wakiona kuwa wameukomoa upinzani.

Kwa upande wangu ninaona kwamba wote pande mbili, wanaohama upinzani kwenda chama tawala na wale walio upande wa chama tawala wanaoshangilia jambo hilo, ni vigumu kujiita wanasiasa! Ndiyo, watasema ni wanasiasa lakini nikiwatazama kiumakini ninaona kuwa hawawezi kuwa wanasiasa.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, amesema kuwa Wana CCM hawapaswi kushangilia Bernard Membe kufukuzwa uanachama kwa sababu hilo ni jambo baya. Kwa kumfukuza Membe CCM inakuwa imepungukiwa na si tu mwanachama, bali mwanachama nguli ambaye aliwahi hata kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais na akaibuka kuwa mmoja wa wagombea watatu ambao majina yao yalipigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM. Sasa unashangiliaje kufukuzwa kwa mwanachama kama huyo?

Mwanasiasa anapaswa awe yule anayesimamia anachokiamini, kilichopo kisiasa na kitakachokuja kisiasa baadaye. Mfano, Tanzania ni nchi ya vyama vingi vya siasa, katiba ya nchi inatambua jambo hilo. Anayeshangilia wanasiasa wa upinzani kuhama kwa sababu huko ni kuubomoa upinzani, anaweza kuwa hajui kuwa Katiba ya nchi inataka kuwepo kwa vyama vingi vya saisa nchini. Ukiwa kinyume cha hilo, ina maana kuwa unaipinga Katiba.

Anayefurahia upinzani kubomoka anatakiwa kuhesabika kama msaliti kwa taifa zima. Kwa hiyo msaliti atajiitaje mwanasiasa na wewe umuone ni mtu aliyekamilika anayefaa kuwa katika nchi anayoisaliti?

Kama katiba ya nchi inaeleza kuwa nchi inaendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, inatakiwa ieleweke kuwa huo ndio mfumo rasmi. Kinyume chake ni ubatili mtupu. Kwa maana hiyo anayehama upinzani kuingia chama tawala, uhamaji huo unatakiwa ufanyike kwa siri bila kujulikana.

Lakini kuushikia bango na kuanza kuushangilia uhamaji huo ni sawa na kumsifia mtu anayekuchafua kwa tope ukimuita msafi na mtanashati! Atakuwaje hivyo huku anashika matope ili akuchafue wewe? Ni dhahiri kuwa kabla hajakuchafua wewe, ataanza kuchafuka yeye na kamwe hawezi kuwa msafi.

Kwa nini ninasema hivyo? Ni kwamba mtu mwenye akili timamu aliamua kuingia upinzani ili kuijenga nchi akiwa upande huo wa upinzani. Sasa anapobadilisha mawazo kurudi chama tawala si kwamba anatafuta kuibomoa nchi badala ya kuijenga? Na bado tuendelee kumuona kama mwenye akili timamu?

Sababu inaonekana wazi kuwa kila anayejaribu kuuboa upinzani anakuwa amepania kuiboa Katiba ya nchi na taifa kwa ujumla wake. Tutamuonaje mtu wa aina hiyo kuwa ana utimamu wa akili?

Lakini kwa upande mwingine, hata kile chama kinachompokea nacho inabidi tukihoji. Unawezaje kumpokea mtu ambaye anakotoka anaonekana kama msaliti kwa sababu ameshindwa kutekeleza kile alichokiamini? Una uhakika gani kama na huku unakompokea hawezi kusaliti na kurudi kule alikotoka au kwenda kwingine?

Zipo sababu zinazotufanya tumuone mtu wa aina hiyo na kuutilia shaka utimamu wa akili yake. Ni kwamba chama tawala kimekuwepo muda wote na ndicho kilichochangia kwa kiasi kikubwa kujitawala kwetu, kwa hiyo anayeamua kukikimbilia kwa muda huu tumueleweje?

Sababu mpinzani kaamua kuijenga nchi, akisahihisha na kurekebisha pale ambako chama tawala kilisahau, na yapo mengi yamerebishwa kwa mtindo huo.

Kama anaamua kujiunga na chama tawala ina maana hatayaona tena yale ambayo alikuwa anayaona akiwa upinzani. hapo atajenga nchi kweli?

Na wale wanaoshangilia kitendo hicho tokea chama tawala tuwaeleje? Ina maana muda wote walikuwa hawaoni ni watu gani wanafaa kukijenga chama chao tawala? Kweli hao ni watu makini?

Au niulize hao ni wanasiasa wa kweli? Tulishangilia tulipopata uhuru wa nchi yetu kwa vile ni kitu tulichokitafuta muda wote na ilikuwa haki yetu, lakini kweli tunahitaji kushangilia kwa mtu kuhama upinzani kujiunga chama tawala?

Ina maana waliokuwemo ndani ya chama tawala walikuwa hawafai, hivyo kukuona kuhama uko kwa wapinzani kuingia chama tawala kama baraka kwao? Kama ni hivyo, kwa nini waendelee kujiita wanasiasa wakiendelea kukikalia chama hicho badala ya kukihama na kuwaachia wanaoweza kazi?

Kwa upande wa wapinzani wanaohamia chama tawala, ni kitu gani kinawashawishi kufanya hivyo? Ni uzuri wa chama tawala au ni masilahi ya ziada? Kwa nini wanafanya hivyo leo na muda wote wamekiona chama hicho tawala bila kujishughulisha nacho?

Inachoshangaza kuna baadhi ambao walitoka hukohuko chama tawala wakakimbilia upinzani baada ya kuona mambo ndani ya chama tawala si mazuri. Leo kimetokea nini hadi wageuke tena na kuona kile kilichokuwa kibaya kimekuwa kizuri?

Labda wapo ambao wameanzia kwenye upinzani ili kupata uzoefu wa siasa, kama ni hivyo kwa nini tusione kuwa upinzani ndio unaofaa katika siasa, kwa sababu unatumika kama shule ya siasa? Kwa nini wasionyeshe huo uzoefu wao wakiwa upinzani?

Kama ni masilahi ndiyo yanayowafanya watu wahame kutoka upinzani kwenda chama tawala, tunawezaje kuwaona hao kama wajenga nchi badala ya kuwaona kama wahujumu nchi kutokana na kuhama walikokuwa wamekaa katika ujenzi wa  nchi kwenda upande mwingine, tena uliokuwepo muda wote, wakidai wanakwenda kuendeleza ujenzi wa nchi uliowashinda wakiwa upande wa upinzani?

Basi, watu kama Julius Nyerere, Nelson Mandela na wengine nao wangehamia upande wa utawala wakiwa wameusaliti upande wa upinzani.

Hiyo ndiyo inaonyesha wazi kwamba kinachofuatwa upande wa chama tawala ni tofauti kabisa na kinachojionyesha. Huwezi kukitamani chama tawala leo hii kana kwamba kimeanzishwa jana wakati hiki ni chama kikongwe na kilicholeta uhuru wa nchi!

[email protected]

0654 031 701

By Jamhuri