Watanzania (na wanadamu wengine duniani kote) nyakati hizi; tunaishi kwenye zama zenye misongo mikubwa ya kimaisha; kubwa likiwa ni tatizo la kiuchumi.

Tunasikia kila kona habari za watu kuwa wajasiriamali na kujiajiri. Pamoja na mbiu ya ujasiriamali kuwa kubwa, kuna mambo tunatakiwa kuyaangalia kwa umakini.

 

Kabla ya mtu kufundishwa kanuni za ujasiriamali (utunzaji hesabu, masoko, utawala rasilimali watu n.k); kuna kitu kinatakiwa kutangulia kumwingia mtu na hicho ndicho ambacho Watanzania wengi tunakikosa.  Kitu hiki ni hamasa na nguvu ya kufanya mambo na kutimiza malengo. Kwa kimombo wanaita “motivational”.

 

Hamasa na nguvu hii haiji hivi hivi, inahitaji kufundishwa kupitia shuhuda za waliofanikiwa, uzoefu walioupata waliowahi kujaribu pamoja na kuthibitisha uwepo wa fursa. Mtu asipokuwa na hamasa na nguvu hii ni vigumu kufanikiwa hata kama akikopeshwa ama kupewa bure mtaji.

Kwa mujibu wa utafiti, imegundulika kuwa chanzo namba moja cha watu wengi kushindwa kumudu kurejesha mikopo (ama kufeli katika maeneo mbalimbali ya kimaisha) ni kukosekana kwa hamasa na nguvu niliyoisema. Watu wanahitaji kufundishwa kanuni za kiasili na kisaikolojia, wajue kujitambua, wapate kanuni za kiubongo zenye kuelekeza namna ya kufanikiwa.

Iko hivi; mtu akijiweza kutoka ndani (nafasi), ni rahisi kuyaweza maisha kwa sababu aonavyo mtu nafsini mwake (fikra, mtazamo na imani) ndivyo alivyo. Naweza kusema kuwa Watanzania tunaendelea kuwa maskini kwa sababu nafsini mwetu tunauona umaskini.

 

Ufisadi na uzembe serikalini ni matokeo ya maradhi tuliyo nayo kwenye nafsi zetu. Maradhi haya ni hatari sana, na tunahitaji tiba ya kuzifunza nafsi zetu kuyaona tunayoyataka.

 

Kimsingi ni kuwa suala la mtu kufanikiwa kibiashara; kiajira; kiuchumi ama katika eneo jingine lolote kimaisha kunahitajika maendeleo ya ndani ya nafsi yake. Kama ni matatizo binadamu wote tunapitia; lakini katika hayo matatizo kuna wengine watakata tamaa; wengine wanaweza hata kujinyonga.

 

Lakini wapo watakaosimama na kuendelea mbele kwa ushindi hata baada ya matatizo kuwapata. Kinachoamua utofauti wa uwezo wa wanadamu kukabiliana na changamoto ama matatizo ni namna tulivyojengeka nafsini, rohoni na kifikra.

 

Kwa jinsi hii, utabaini kuwa kama Taifa tunatakiwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa fikra chanya kwa Watanzania kabla hata ya kufikiria namna ya kupambana na ukosefu wa ajira, kuyumba kwa biashara na uchumi pamoja na kukabiliana na changamoto kali zinazotukabili kila kona.

Ninafahamu, na tena ninaamini kuwa hata Mungu huwasaidia kuwapa nguvu waovu katika fikra zao na huwabeba wenye unyoofu wa moyo katika mawazo yao yanayoelekea mafanikio na utajiri. Msingi mkubwa ni mawazo (yaani namna tunavyofikiria) ambayo kwa upande wa pili yanaamua namna tunavyotenda. Kufikiri sahihi kunahitaji taarifa sahihi na taarifa sahihi hupatikana kwa mtu kuwa na bidii katika kujisomea, kujifunza kwa wengine na kuwa mdadisi.

Fikra zetu ndizo zinazoweza kutuletea utajiri ama umaskini, mafanikio ama kushindwa. Nia yangu ni kusimama katika eneo litakalowezesha watu wengi kuishi maisha ya ushindi na ya utajiri. Nafahamu kuwa zipo njia nyingi zinazoweza kumpa mtu utajiri. Lakini mafanikio na utajiri halisi na wa kweli unaanza katika fikra zetu.

 

Kingine cha kufahamu ni kuwa inawezekana mtu ukawa tajiri lakini usiwe na uhuru wa kifedha, kutegemeana na njia uliyoitumia kuupata huo utajiri. Ingawa kuna nadharia nyingi, hapa nitasema nadharia moja yenye vipengele vitatu.

 

Unaweza kupata fedha kwa kutumia nguvu za shetani, unaweza kutajirika kwa nguvu za Mungu na upo uwezekano mtu akatajirika kwa kutumia nguvu na akili zako mwenyewe (wengi huita kama mtulinga).

Ninachoweza kukushauri  ni kufanya kile alichosema, aliyepata kuwa bilionea duniani (hajapata na huenda hatatokea mwingine zaidi yake), Mfalme Suleman. Yeye alisema mambo mawili; la kwanza ni hili; “Mafanikio/utajiri pamoja na kumcha Mungu ni uzima” na la pili akashauri hivi; “Usiwahusudu waovu (wezi, mafisadi, washirikina) wanapofanikiwa”.

 

Tunataka utajiri na uhuru wa kifedha ambao utaleta ustawi bora kwa jamii zetu; ndiyo maana nasisitiza tuwe na fikra chanya.

Ninaposema neno utajiri hakuna kufanana, ingawa kuna kurandana na dhana ya mafanikio. Mtu anaweza kufanikiwa katika jambo fulani lakini asiwe tajiri. Kwa mfano, inawezekana mtu anayehamasisha watu kulala katika vyandarau kijijini kwake akafanikiwa kuchangia kupungua kwa malaria lakini akabaki kuwa maskini wa kiuchumi.

Kutoka hapo tunaibukia kwenye dhana pana zaidi ambayo ni fikra sahihi kutuletea mafanikio pamoja na uhuru kamili wa kifedha na kiuchumi (real financial freedom). Uhuru wa kiuchumi na kifedha ni pale unapoweza kupata kipato pasipo kufanya kazi. Iwe ni mfanyakazi wa kuajiriwa, iwe umejiajiri au mwekezaji, unayo nafasi na tena ni muhimu kufikiria na kunuia kujipatia mafanikio yenye kukufaa wewe na wengine.

Huhitaji muujiza ili kupata mafanikio katika eneo lolote maishani; isipokuwa unachohitaji ni ufahamu, nia na kusudi la kujipatia mafanikio na uhuru wa kiuchumi na kifedha. Hapa ndipo ninaposema Watanzania tunahitaji hamasa kuliko hata kubadilisha katiba au chama kinachotawala!

Huu si muda wa kulalama kuhusu kuongezeka kwa pengo la wenye nacho na wasio nacho (pengo hilo litazidi kuongezeka hata watu waandamane na kulia machozi ya damu, anayebisha asome falsafa za Yesu Kristo kuhusu jambo hili). Kitu cha kuhangaika nacho kwa sasa ni kuchukua hatua kama Taifa na kama mtu mmoja mmoja kuangalia ni kwa namna gani tunaweza kujipatia uhuru wa kiuchumi na kifedha.

Kinachokosekana miongoni mwetu tulio wengi si mitaji, fursa wala elimu. Ugonjwa mkubwa wa Taifa hili upo katika ukosefu wa mawazo (ideas) na hamasiko (motivational, inspirational). Kwa wanaoona mbali na wenye nia ya kulisaidia Taifa hili (hata kama atasaidika Mtanzania mmoja) ninashauri wawekeze katika  ujenzi wa fikra. Utakapojengeka ufalme wa kifikra itakuwa rahisi kupata mafanikio ‘chanya’ katika harakati zozote zile (zikiwamo za kisiasa).

Naomba sasa niseme japo kwa ufupi hatua ambazo mtu anapaswa kuzipitia kuelekea katika uhuru wa kiuchumi na kifedha. Kwanza kuna mambo magumu lazima ukubaliane nayo hata kama hungependa kujua.

 

Lazima utambue kuwa hakuna yeyote atakayewezesha maisha yako mara baada ya kustaafu kwako, utambue kuwa Serikali haiwajibiki (japo inaweza kukusaidia) katika uhuru wako wa kiuchumi. Cha kuelewa ni kuwa unawajibika kwa maisha yako mwenyewe kwa asilimia 100.

Jambo la kupata utajiri ama niseme uhuru wa kifedha haliji kwa bahati nasibu, ni lazima upange. Watu wengi wanatamani kufanikiwa, lakini hawapangi kufanikiwa. Kutamani pekee hakutoshi (mamilioni waliishi na maghorofa na magari vichwani mwao wakafa bila kuonekana), kunahitajika mikakati na uamuzi.

Unapoamua kufanikiwa lazima sasa uanze kuishi maisha ya kimafanikio. Kama unataka kuwa tajiri ni lazima ujizoeshe kuwa na tabia za kitajiri. Zipo tabia za kimafanikio ambazo husababisha watu kuzidi kufanikiwa zaidi na zaidi. Kwa habari ya uhuru wa kifedha na kiuchumi, utalazimika kuwa na mfumo utakaoongeza kipato chako.

 

Fikiria kipato zaidi ya mshahara wako, zaidi ya faida unayopata katika biashara ya sasa, fikiria kuanzisha kampuni mpya na anza namna fulani za kufanikisha unavyovitafuta.

Katika hatua hizo kutakuwa na utajiri (ama uhuru wa kifedha) na ikiwa unapenda kustaafu kazi (kwa walioajiriwa), basi unaweza kuacha kazi lakini unaweza kuendelea kufanya kazi ikiwa unafanya kwa furaha.

 

Watanzania tunastahili ushindi wa kiuchumi

0719 127 901

stepwiseexpert@gmail.com

 

 

3828 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!