Sehemu iliyopita, Mwandishi Wetu alieleza Kamati iliyoundwa na CCM kuchunguza mgogoro wa Loliondo. Sehemu hii ya nne na ya mwisho, anaeleza ubatili wa Kamati ya Nchemba. Endelea…

Badala ya timu hiyo kukusanya maoni na kurudisha majibu, ushauri na mapendekezo ya walichokibaini Loliondo kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, wao wakiwa katika Kijiji cha Olerian Maigaduru, Nchemba aliwaambia wananchi kuwa Serikali ya CCM ilikosea kutangaza kumega eneo la Pori Tengefu Loliondo.

 

Akasema kwamba uamuzi huo unakiuka Sheria ya Wanyamapori na una athari kubwa kwa wananchi, hivyo aliwaomba wananchi hao kuvuta subira na kumpa muda wa siku saba ili aweze kufikisha mgogoro huo kwa viongozi wa juu [Waziri Mkuu] ili upatiwe ufumbuzi, yaani atengue uamuzi wa Waziri.

 

Mheshimiwa huyu alitoa uamuzi huo baada ya Kamati yake kupokea maelezo ya utetezi kutoka kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya, wana-CCM, viongozi wa mila [malaigwanan], watendaji wa Serikali wa ngazi mbalimbali, na pia baada ya kina mama kumkabidhi kapu lililojaa kadi, bendera na sare za CCM!

 

Hayo yakamfanya ajiridhishe bila kuacha shaka kuwa hoja za wananchi kupinga uamuzi wa Serikali ni sahihi! Nchemba bila kutafuna maneno alisema, “Mwenye duka anapomwachia mtu kuuza duka na yeye akapandisha bei ya bidhaa na kufanya wateja waanze kuhama ni lazima mwenye duka arudi kulinusuru ili lisifungwe, hivyo hatutakubali kukosa wateja, ni lazima tumdhibiti muuza duka.” Hapa mwenye duka ni CCM na muuza duka ni Balozi Kagasheki!

 

Pamoja na Kamati hiyo kusheheni wanasiasa nguli na makada wa CCM, ilishindwa kazi yake baada tu ya kuteuliwa  hata kabla ya kufika Loliondo; achilia mbali wengi wa wajumbe wake kuwa na vinasaba na wafugaji wa Kimaasai. Sikustaajabu sana kwa uamuzi wa Kamati hiyo maana tuliutarajia.

 

Miongoni mwa maswali tuliyojiuliza, ni kwanini migogoro ya ardhi Loliondo haimaliziki? Kwanini migogoro ni Loliondo na si Maasai Mara? Kwanini Kamati hii ikiwa kwenye mkutano wa hadhara iligeuka na kuwa wapinzani wa Serikali yao wenyewe tena wakiwa kwenye ziara ya kichama?

 

Kwanini wageni wetu hawa baada ya kufika Loliondo hawakupelekwa maeneo hasa anayozungumzia na kutolea uamuzi Balozi Kagasheki katika vijiji vya Soitsambu, Ololosokwan, Loosoito, Oloipir [maeneo yenye vyanzo vya maji, mazalia na mapito ya wanyamapori], badala yake wakapelekwa Kijiji cha Maigaduru?

 

Wenyeji walikuwa wanaficha nini? Je, kwa kushindwa kufika eneo la tukio, Kamati hii itakuwa na uhalali wa kumshauri Katibu Mkuu wa CCM Taifa au Waziri Mkuu juu ya mgogoro wa ardhi Loliondo?

 

Loliondo yote ni CCM na wananchi wanayo haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa. Je, Nchemba yuko tayari kuvunja sheria za wanyamapori ili wana-Loliondo wasijiunge na vyama vingine vya siasa? Je, wana-CCM sehemu nyingine nchini wakitishia kurudisha kadi za CCM Serikali itakuwa tayari kupindisha sheria kama Loliondo ili wasihame chama?

 

Kwanini Kamati ya Nchemba iliikana sera yao ya ubinafsishaji na uwekezaji? Kwanini sera ya ubinafsishaji na uwekezaji imekuwa shubiri badala ya kuwa neema kwa wananchi? Ni kweli CCM walidaka sera hii bila kujua madhara yake kwa jamii masikini?

 

Napenda kuifahamisha Kamati ya Nchemba kuwa kampuni hizi za uwindaji za Kizungu na NGOs zao ndizo pekee hupanga safu ya uongozi wilayani Ngorongoro kwa manufaa yao. Zaidi ya asilimia 90 ya madiwani wa sasa [wa kuchaguliwa/kuteuliwa], ama walishafanya kazi, au ni wafanyakazi/waajiriwa wa NGOs hizo zaidi ya 30.

 

Au wengine ni waajiriwa kwenye kampuni za uwekezaji za Kizungu zilizopo Loliondo, hivyo si rahisi kuwatetea wananchi wa Loliondo wala CCM kama wanavyojinasibu zaidi ya kampuni za Kizungu kwa maana ya kulipa fadhila na kuipiga vita vya wazi kampuni ya OBC Limited.

 

Kwa sababu hiyo, ushauri wa Kamati hii si wa kuuamini, maana si wa kitaalamu. Msingi wake utakuwa ni wa kisiasa zaidi baada ya wananchi wa Loliondo kutishia kurudisha kadi za CCM na kujiunga vyama vya upinzani.

 

Iwapo huu ndiyo utakuwa ushauri wa Kamati ya Nchemba kwa Waziri Mkuu, utakuwa na madhara makubwa  maana ni heri wana-Loliondo ambao wengi wao ni wana-CCM wahame na kujiunga vyama vingine vya siasa kuliko kuvunja sheria ili eti wasihame.

 

Maana leo ukifanya hivyo Loliondo kesho itakuwa hivyo Serengeti, Tarangire na sasa kama inavyodaiwa kilimo cha kujikimu NCAA. Lakini kibaya zaidi itakuwa ni kumdhalilisha Waziri mwenye dhamana na wizara hii. Ikumbukwe kuwa yanayotokea leo Loliondo yalishatokea mwaka 2000 na msingi wake si wananchi wa Loliondo, bali wawekezaji kupitia NGOs.

 

Mwisho, Balozi Kagasheki anastahili pongezi kwa kuwa na moyo wa huruma kwa kuwatengea wananchi wa Loliondo ardhi kwa matumizi yao. Kagasheki songa mbele. Sasa mgogoro huu unasubiri uamuzi wa “Mtoto wa Mkulima” baada ya kushauriana na Rais baada ya kuahirisha shughuli za Bunge. Kagasheki Aluta Continua

Please follow and like us:
Pin Share