Mfululizo huu wa makala kuhusu Loliondo ulianza wiki mbili zilizopita. Kwenye toleo la mwisho, tuliishia kwenye kipengele kinachopingana na propaganda za uongo kwamba Serikali imechukua ardhi ya vijiji. Mwandishi anasema baadhi ya madiwani na NGOs zimetumiwa kueneza uongo huo kwa maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi. Endelea.

Waziri Kagasheki  alisema kuna Waziri mmoja wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi  aliyejikoroga (hakumtaja), kwa kuwapa wananchi hati bandia za kumiliki eneo la Pori Tengefu, huku akijua kwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za ardhi.

 

Maswali ya kujiuliza; ni nani aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati vijiji hivyo vinasajiliwa na kupewa hati bandia miaka ya 1990? Kwanini vijiji vingi katika Tarafa ya Loliondo vilisajiliwa wakati huo huku kwenye tarafa nyingine vikigomewa kusajiliwa kwa vigezo vya migogoro ya mipaka? Tarafa ya Loliondo hakukuwa na migogoro ya mipaka? Huu wa sasa umetoka wapi? Je, ni sahihi kisheria kutoa hati juu ya hati kabla ya kutengua kwanza hati ya awali?

 

Je, kisheria ni nani mwenye mamlaka ya kubadilisha matumizi ya ardhi [custodian] kati ya waziri na rais kwa manufaa ya umma? Taratibu zote za kusajili vijiji zinajulikana je, vijiji hivi vilivyopewa hati bandia vilifuata taratibu hizo, ikiwa ni pamoja na kijiji husika kuitisha Mkutano Mkuu wa Kijiji tarajiwa na baadaye kumbukumbu zake kujadiliwa na kata [WADC], vikao vya ushauri vya wilaya [DCC] na hatimaye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kujiridhisha na kutoa hati?

 

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema kwamba utaratibu wa kupora ardhi Pori Tengefu Loliondo kimkakati uliratibiwa na kusimamiwa na baadhi ya NGOs na wanasiasa, sambamba na usajili wa vijiji hivyo na vingine kama Naan na Masusu, ambako taratibu za kuvisajili hazikufuatwa, bali zilifanyika mbinu ikiwamo za kujenga miundombinu kama shule, zahanati, kuingiza wahamiaji kutoka nchi jirani nk.

 

Hiyo ilikuwa mbinu ya kutwaa ardhi kwa nguvu na baadaye ukabila ukachukua mkondo wake. Katika mazingira hayo ya taratibu, kanuni na sheria kukiukwa na wahusika kwa maksudi, hapo kuna kijiji chenye hati halali? Je, waliohusika na mchezo huo wamechukuliwa hatua gani?

 

Hivyo, kusema Pori Tengefu Loliondo ni ardhi ya mababu na mali ya vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria Namba 7 ya Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ya 1982 ni upotoshaji, maana ukisoma Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999, Sheria ya Wanyamapori Namba 23 ya 1974, Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009 pamoja na sera zilizopo, waziri kwa niaba ya rais ana mamlaka ya kuboresha mapori tengefu nchini.

 

Nashauri kwamba Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999 ifanyiwe marejeo kwa kuzipunguzia madaraka halmashauri za vijiji maana ndizo chanzo cha migogoro mingi ya ardhi nchini. Hii inatokana na uelewa  wao mdogo. Ni vigumu kuingia mikataba yenye tija na wawekezaji weledi.

 

Malango yote yafutwe

Nimuombe Balozi Kagasheki kuyafuta mara moja malango yote nchini yaliyowekwa kinyume cha sheria kwenye barabara zipitazo kwenye mapori ya akiba, mapori tengefu na kwenye vivutio mbalimbali vya utalii nchini kama barabara ya Babati-Orkasmet-Kiruani-Msitu wa Tembo, Barabara ya Mto wa Mbu-Engaruka-Ngarasero-Loliondo kwa kisingizio cha kudhibiti mapato na rasilimali za maliasili maana mageti haya yamegeuka kuwa kero kwa wananchi na watalii; tena huongeza gharama na usumbufu bila sababu za msingi. Zaidi, mapato yatokanayo na ushuru wa mageti haya huingia kwenye mifuko ya wezi maana hata risiti ya malipo hazitolewi.

 

Tishio la kujiuzulu madiwani

Baadhi ya madiwani wilayani Ngorongoro katikati ya Machi 2013 walitishia kujiuzulu nyadhifa zao zote kwenye halmashauri hiyo, iwapo Serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii itaendelea na azma yake ya kumiliki eneo la kilomita za mraba 1,500 kutoka Pori Tengefu la Loliondo.

 

Sababu nyingine ni kwamba Serikali haina eneo ndani ya Pori Tengefu Loliondo, bali kisheria eneo hilo ni ardhi halali inayomilikiwa na wananchi kwa mfumo wa vijiji vya Soitsambu chenye hati namba 7275 ya Oktoba 13,1990, Arash hati namba 7264 ya Oktoba 13,1990, Ololosokwan chenye hati iliyotolewa Januari 25, 1996, Engusore Sambu, Oloirian Magaiduru, Loosoito, na Oloipiril; kwamba eneo linalomegwa na Serikali si mazalia ya wanyamapori, vyanzo vya maji wala ushoroba; bali inawahadaa wananchi kwa lengo la kuwaondoa wafugaji wa kabila la Kimaasai ndani ya Loliondo ili kupisha biashara ya uwindaji na utalii kwa kampuni ya Otterlo Business Corporation Ltd [OBC]ambayo haina eneo.

 

Mbali na hoja hizo, kuna lugha za vitisho zilizokosa ladha na zenye ukakasi masikioni, ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya madiwani wanaojifanya wana uchungu na wananchi wa Loliondo eti “wananchi tupo tayari kufa na kuzikwa kwenye kaburi moja, wananchi hawako tayari kuhama labda wapigwe risasi na kuwapoteza wote, kwamba waziri wa maliasili na utalii ni mwongo na afute kauli yake ya kumega eneo la Loliondo, kwani hana mamlaka wala nia ya kutatua mgogoro huo, bali anataka kuipatia eneo hilo kampuni ya OBC Limited.

 

Binafsi, sikuamini maneno niliyoyasikia yakitoka vinywani mwa watu ninaowaheshimu na kuwafahamu kama madiwani. Nilidhani kuwa ni watu makini. Hii ni kuthibitisha kuwa wanasiasa wetu ndiyo wachochezi wa migogoro Loliondo. Badala ya madiwani kutuambia ni kwanini hadi karne ya 21 bado tumezama kwenye lindi la umaskini wa kutupwa pamoja na rasilimali tulizonazo, au watueleze tunavyonufaika na mapato yatokanayo na rasilimani zetu kiuhalisia badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na tija.

 

Diwani anapokosa weledi huiharibu kata yake kwa mikono yake mwenyewe, maana migogoro hii wanaoathirika ni akina mama na watoto tena baadhi ya madiwani wetu hakuna wanachopoteza, kwani vurugu zinapotokea wao huvuka mpaka na kurudi kwao na kutuachia wazawa matatizo [Loliondo si sehemu salama].

 

Pia tunasubiri watekeleze kusudio lao la kujiuzulu nyadhifa zao zote ili turudi kwenye uchaguzi, maana kazi tulizowapa zimewashinda ndiyo maana hawawashirikishi waliowachagua kutoka kwenye kata zao.

 

Kimsingi, mayowe haya ni dili na yameasisiwa na baadhi ya madiwani, wanasiasa na NGOs kwa lengo la kupata ‘mshiko’ na wameamua kuipotosha jamii ya Watanzania na dunia kwa jumla kwa malengo yao binafsi, na si kwa faida ya wananchi wa Loliondo. Kwa uhalisia wananchi ndiyo tuliovamia pori tengefu.

 

Mwenye kumbukumbu nzuri atakumbuka mwaka 1964 Dk. Ochinga kutoka Austria alianzisha Hospitali ya Wasso kwa lengo la kuhudumia wagonjwa wa kifua kikuu (TB) na baadaye mwaka 1974 alianzisha kituo cha kulelea watoto wenye utapiamlo Mondorosi na kuweka pampu ya kuvuta maji katika eneo hilo. Mwaka 1976 eneo hilo lilijengwa shule na kuanzishwa Kijiji kikongwe cha Soitsambu, hivyo eneo la pori tengefu halikuwa na boma hata moja.

 

Wanasiasa wetu wanajua kwamba Kenya kuna uhaba mkubwa wa ardhi na ukoo wa Loita na Boroko ni wahamiaji kutoka huko, baada ya kufukuzwa wakati wa kuanzishwa mbuga za Maasai Mara [Narok], Samburu [Kajiado] na kwa sababu ya uhaba wa malisho [ukame] walijipenyeza kwenye maeneo ya Tarafa za Loliondo na Sale na kuhodhi ardhi kinyume cha sheria.

 

Kuna kisa cha kweli kilichoandikwa na mwandishi Henry ole Kulet katika kitabu chake cha ‘Is it possible?’, akielezea maisha halisi ya kijana wa Kimaasai aitwaye Lerionka wakati akisoma Shule ya Kati Arusha [sasa Arusha Sekondari] akitokea kwao Narok kwenda shule Arusha kupitia Loliondo.

 

Lakini pia kuna simulizi kutoka kwa mababu wa Kiiraq, Wakurya, Wamaasai ukoo wa Letayok, Kisongo na Wasonjo zinazothibitisha kwamba Pori Tengefu Loliondo ni mpaka kati ya Wasonjo na Wakurya baada ya Wairaq kuondolewa kwa nguvu na Wamaasai katika Milima ya Ngorongoro, hivyo kuthibitisha uhamiaji wa Boroko na Loita Loliondo.

 

Itaendelea

 

1763 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!