Mwaka huu pekee, Tanzania imepokea marais wa mataifa mawili makubwa yanayoongoza kwa uchumi imara duniani. Rais Xi Jinping wa China alikuwa wa kwanza, na baadaye amefuatiwa na Rais Barack Obama wa Marekani. Ujio wa viongozi hao, pamoja na kauli za kwamba wanataka kufungua milango ya kushirikiana kiuchumi, ni ukweli ulio wazi kwamba Tanzania imeendelea kurusha ndoana ya kuomba misaada. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, katika hotuba yake ya Februari 5, 1967 jijini Dar es Salaam, alieleza athari za nchi kuwa omba-omba. Sehemu hii ya hotuba inapatikana kwenye kitabu chake cha Ujamaa ni Imani (2). Endelea.

Kujitegemea

Sasa ningependa kuwaelezeni habari tuliyoizungumza juu ya siasa ya kujitegemea. Nayo si ngumu kueleza; nayo pia rahisi. Nimesema mara nyingi- na ni jambo la kweli, si la uongo- kwamba kujitawala kwa kweli maana yake ni kujitegemea. Hakuna kujitawala kwa kweli kama hakuna kujitegemea. Ni kujidanganya tu. Hili wote tunajua. Mimi najua, wote wananchi mlio hapa, na wananchi wa Tanzania wanaonisikiliza, wote wanajua. Hakuna maana nyingine ya kujitawala isipokuwa kujitegemea.

 

Bin omba-omba

Watu tunasema tunataka kuheshimika tuheshimiwe. Ndiyo tutaheshimiwaje? Tutaheshimiwa na dunia kwa kujitegemea; hakuna namna nyingine dunia inaweza kutuheshimu. Hii yote tunajua; mimi najua na wenzangu wananchi, na wana-TANU, wote mnajua vilevile.

 

Hatumheshimu Athumani bin Maganga kwa sababu anakula chakula cha kuomba; anavaa kilemba cha kuomba; kiatu chake cha kuomba; kitanda cha kuomba. Athumani bin Maganga mahari aliyoolea Binti Musa ni mahari ya kuomba. Binti Musa yuko nyumbani na kajaliwa, kazaa. Lakini kila siku yuko barabarani anatoka nyumba hata nyumba, hodi, karibu! Hapa kaja kuomba nini? Kaja kuomba vitumbua. Anaomba-omba. Mara anatoka hapo. Akishapata vitumbua hapo anakwenda nyumba ya tatu; huko anakwenda kuomba nini? Anakwenda kuomba kibiriti, nyumbani hakuna moto.

 

Nani dhahiri kwamba mtu huyu hawezi akaheshimiwa. Tena watu hawatamwita Athumani bin Maganga, watamwita Athumani bin Omba-omba, jina lake ni “Omba-omba” na wakimwona watu wanaanza kufunga milango wanasema, “Huyo tena anakuja”. Wanafunga milango. Hawamkaribishi, hawampokei, hana heshima; majirani zake wote wanamsema mtu wa namna hii, mtu balaa mtu yule. Mtu mzima, si kilema, si mgonjwa lakini omba-omba; hafanyi kazi, hataki kujitegemea. Anakula vya wengine; kupe mkubwa! Hawezi akaheshimiwa na mtu.

 

Taifa la omba-omba

Mtu anayeheshimiwa duniani anajitegemea. Anafanya kazi, anajitegemea; hategemei watu wengine. Anayetegemea watu wengine ni mmoja katika makundi ya wale wanyonyaji.

Kadhalika taifa. Taifa haliwezi likaheshimiwa duniani kama ni taifa la Bin Omba-omba, waombaji wakubwa. Iwe taifa la Tanzania namna yetu ya kulijenga taifa letu liheshimike sana duniani ni kuomba, kila siku kuomba, chakula cha kuomba, kila kitu chetu sisi ni cha kuomba.

 

Tukichagua viongozi ni viongozi wetu wa kuomba. Rais Nyerere anasifiwa na wananchi wa Tanzania. Wanasema, “Tuna President hodari sana”. Uhodari wake nini? “Ni mwombaji sana Rais wetu. Mara yuko Marekani, mara yuko China, mara yuko India, mara yuko wapi, anakwenda kuomba. Na akirudi ana mahindi mfukoni. Rais wetu mtu mkubwa sana. Na asipokwenda mwenyewe, huwapeleka mawaziri; wala hachelewi. Mara waziri mmoja yuko huku kusini, mara mwingine kaskazini; hawakai mawaziri, hawatulii hata kidogo. Wamo katika safari za kuomba- omba. Tuna nchi barabara sisi”. (vicheko)

 

Mnacheka wananchi kwa sababu mnajua hili ni jambo la kipumbavu. Nchi haijengwi namna hii; nchi hijengwi kwa omba-omba. Nchi inajengwa kwa watu wanaojitegemea wenyewe, chochote kile walichonacho wanajitegemea, siyo wanaomba. Sifa ya serikali yetu iwe ni sifa ya kuomba. Hatuwezi tukawa kitu. Na tulipokutana Arusha tuligundua kuwa tulifanya makosa.

 

Kuleta matumaini

Tumetilia mkazo mkubwa sana habari hii ya omba-omba. Magazeti, maredio, maelezo yetu: omba-omba, omba-omba. Mawaziri wetu wakienda nchi za nje nyinyi sasa mnatega sikio. Waziri wetu mmoja amekwisha kwenda Ulaya, sasa tutege masikio. Na yeye akirudi, hata kabla ya kurudi, huanzia huko huko analeta habari, “Jamaa, nimeanza mazungumzo ya neema huku.” Na akishafika pale Dar es Salaam, kiwanja cha ndege mara huita waandishi wa magazeti, huambiwa watu wa magazeti, “Njooni sasa, mnitangazie neema niliyoileta.”

 

Basi hukaa na watu wa magazeti akawasimulia habari ya mazungumzo yake yaliyokuwa ya kwenda kuleta neema, na magazeti hutangaza na redio hutangaza. Hawatangazi pesa, mara nyingi si pesa wanazotangaza, ila kazungumza mazungumzo, wakubwa wakafurahi. Anawaambia, “nimesema nao vizuri, nimekuja na matumaini”

 

Basi tutatangaza hiyo. Mara tutasikia mkubwa wa huko naye kaja, naye kafunga safari kafika. Mara tutatangaza vile vile, “Mkubwa mmoja kafika hapa kaja kuzungumza mazungumzo ya neema.” Tutamkaribisha kwa vishindo vikubwa. Halafu wakati wa kuondoka tutaita magazeti tuwaambie, “Tumezungumza na wenye neema.” Mazungumzo yamekwendaje? “Yamekwenda vizuri sana!” Ataondoka atakwenda huko alikotoka.

 

Basi ili mradi tukianza mazungumzo tutatangaza; akija mkubwa hapa tutatangaza; mkataba ule tukiutia sahihi tutatangaza; tukianza kuvipokea visenti vya kwanza tutatangaza; na kila tunavyopokea kidogo kidogo tutatangaza Tanzania ijue kwamba serikali inafanya kazi ya ujanadume, kazi ya kuomba-omba. Tunakuwa waombaji wakubwa, ndivyo tunavyojenga taifa, tunajenga taifa kwea kuomba-omba! Tumekubaliana kwamba, jambo hili ni chafu, baya, halifai. Halifai kwa nini? Kwa sababu mbili nzuri sana.

 

Njia hiyo haitufai

Kwanza, kwa sababu hatuwezi kuzipata hizo pesa, uwongo mtupu; tunajifedhehesha bure tu. Nani atatupa pesa zile? Hivi kuna mjomba huko, kuna nchi ina wajomba zetu huko? Basi wanachongojea ni kwamba twende na kofia ya kuombea? Iko wapi hiyo nchi? Haipo. Nchi zote na hasa nchi matajiri, zimo katika kupunguza misaada yao ya kuzipa nchi za nyuma, nchi zenye dhiki.

 

Marekani ambao ndio matajiri duniani kupita taifa jingine lo lote, juzi juzi wametangaza kwamba katika matumizai yao ya mwaka ya paundi milioni arobaini na nane elfu, watatumia paundi sitini na tano milioni kuipa Afrika. Sitini na tano milioni! Na kwa pasa hizo kila nchi ya Afrika ianze kuwa Bwana Omba-omba. Tanzania itapeleka watu, kila nchi ya Afrika itapeleka watu sasa, tukazigombanie hizo sitini na tano milioni. Haziwezi hata kujenga reli moja.

 

Waingereza pia wametangaza, kwamba wanapunguza fedha zao za misaada. Wanasema kuwa wao wenyewe ni maskini, wanakufa; kwa hiyo lazima wapunguze misaada. Ili mradi kila nchi tajiri inajitazama yenyewe, ndivyo ilivyo duniani. Dunia hii si dunia ya mawalii, hii ni dunia ya watu wachafu- chafu, wanapenda kunyonya wenzi wao. Hakuna dunia ya mawalii hapa, kwamba matajiri hawa mtu unawatazamia. Tutafanya jambo la kijinga sana kutazamia matajiri hawa, nchi hizi za kitajiri, eti watatupa pesa, mradi twende tuseme nao vizuri tu!

 

Hata kidogo; wananchi msijidanganye. Hata katika nchi moja kama yetu hii, hii ya Tanzania, kuna matajiri. Kama nilivyowaambieni kwamaba, kazi ya utajiri ni kuondoa dhiki, kazi ya mali ni kuondoa dhiki. Lakini serikali yetu inapotaka kupata fedha kidogo za kuondolea dhiki, na matajiri wa Tanzania ndiyo wenye fedha, Serikali yetu haiwaombi. Hivi huwaomba hawa? Hatuwaombi. Tunawatoza kodi. Uende uwaombe matajiri, unapita unawaomba matajiri, watakubali? Wanapigwa kodi; wapende wasipende wanatozwa kodi, asiyelipa tunamtia ndani.

 

Njia peke yake duniani ya kuvamia mali ya matajiri, isaidie kuondoa dhiki, ni kuwatoza kodi. Hakuna njia nyingine. Kama mali yenyewe mmewaachia mpaka wakawa nayo, wanatozwa kodi; hawaombwi. Kuomba unaomba zaka! Lakini unaweza kuendesha nchi kwa zaka ya Jumapili? Ile zaka ya Juampili ni ile ya makanisani ambako mtu anapitisha bakuli. Sasa, waheshimiwa, mwingine ataweka shilingi moja, mwingine senti hamsini. Tajiri, pengine jizi, hilo hutumbukiza arobaini, linafurahi lenyewe, linakwenda nyumbani linajitapa, “Leo nimeweka shilingi arobaini katika sahani kanisani!”

 

Yote hiyo anayafanya ili aseme vizuri na ma sheikh na mapadri, nao wataanza kumtetea kwa sababu kajenga msikiti au kanisa. Na umaskini bado upo, bado uko hapa na pote duniani. Na misikitini wanapokea zaka zao zile kila siku, haziishi. Jumapili, leo, tumetoa; na umaskini bado uko pale pale. Umaskini hauondoki kwa zaka za Jumapili; umaskini unatolewa kwa kodi, au kwa kila mtu kufanya kazi.

 

Lakini dunia haina Serikali, Serikali itakayowatoza matajiri; rafiki zangu Marekani watozwe kikodi kidogo, Waingereza, Wajerumani, Warusi na matajiri wengine duniani wapigwepigwe vikodi kidogo, nchi ambazo ni maskini zenye dhiki ziweze kusaidiwa. Eti tunategemea zaka, zaka; zaka za matajiri! Tunatengeneza mpango wetu, mpango wetu wa miaka mitano, kumbe ni mpango wa zaka!

 

Basi wananchi nasema kwa sababu hiyo tunafanya makosa. Tunafanya makosa kwa nini? Kwa sababu hatuwezi kuzipata fedha za matajiri. Tunajidanganya kwamba tutapata pesa za matajiri, kwa kudhani watakuja wanazitoa tu. Au tunapokuwa hatufikirii zaka za Serikali tunafikiria za wale matajiri, kwamba eti makampuni yatakuja yataanzisha viwanda, bora tuseme nao vizuri tu!

 

Sheria ya kulinda mirija

Na sheria tunapitisha; Bunge limepitisha sheria. Tumepitisha sheria; na sheria tuliyopitisha katika Bunge letu ni kuwathibitishia waheshimiwa hawa kwamba nchi hii ni salama, haina wasiwasi walete tu mali zao. Waheshimiwa, hivyo ndivyo lakini? Tusimame na misahafu, tuwaapie waheshimiwa hawa…Mimi nitashika Bibilia, Karume atashika Korani, na Rashid atashika Korani, wote tunawaapia waheshimiwa hawa walete mali yao katika nchi yetu, wasiwe na wasiwasi. “Msiogope hata kidogo!” Lakini hata tukiapa, wataleta? Mbona tumekwisha apa! Mbona tumekwisha kupitisha sheria za kuwahakikishia kuwa mali yao itakuwa salama? Itakuja? Nawaambieni haiwezi kuja. Hiyo sababu ya kwanza.

Sababu ya pili ninayowaambieni siasa ya omba-omba haifai ni ujinga wenyewe. Hata kama mapesa ya matajiri yangemiminika, hivyo ni sawa?

 

Mirija ya Wazanaki

Waheshimiwa, nitawaelezeni jinsi Wazanaki wanavyokunywa pombe. Kwanza mtulie kidogo, maana hadithi hii ndefu.

 

Wazee wa Kizanaki wanapokunywa pombe, wananchi, chungu kikubwa huchimbiwa chini, na wazee hukaa wamekizunguka kile chungu na kila mzee hapo alipokaa ana mrija wake unaingia mle mwenye chungu. Wote wamekizunguka, kila mtu na mrija wake, unaingia mle mwenye chungu. Na huko katika majumba kuna pombe; mitungi ya mapombe imejaa tele humo majumbani. Wazanaki pombe yao huchanganya na maji ya moto. Sasa hapa wazee wamekaa, kimya, kila mtu ana mrija wake.

 

Na hapo kuna watu wengine wanaoshughulika kwenda kuleta ile pombe na kuimimina humu mwenye chungu, na kumimina maji ya moto. Wao kazi yao ni kutazama tu. Kama pombe inapunguka wanaongeza; maji ya moto yakipunguka wanaongeza. Wengine wako kule kazi yao ni kuchochea kuni; maji ya moto yabaki moto wakati wote.

 

Wengine wako njiani na vibuyu, wanaleta maji yasiishe pale nyumbani, hasa wakina mama hawa ndio wanaoleta maji. Na humo majumbani, pombe nyingine iko tayari kuchotwa; nyingine inatayarishwa, ni ya kesho; nyingine ni ya kesho kutwa. Basi ili mradi wako watu wanaoshughulika kuona kwamba mitungi ina pombe wakati wote, na maji ya moto yako jikoni, na wengine wanakwenda kuleta maji mengine.

 

Na hawa wazee wa Kizanaki wamekaa wanakunywa pombe; tena ni watu jeuri, wazee wa Kizanaki. Mrija wake huushiki, ukiushika ugomvi, ugomvi mkubwa sana. Huushiki kwa mkono, wala huuruki mrija wake. Hawatoki hapo; wakikaa hapo hawatoki ovyo ovyo. Wazee hawa wamekaa tu, wanakunywa pombe kwa mirija, na wengine wanashughulika: wanamimina pombe, wanamimina maji.

 

Mirija mikubwa zaidi

Sasa wananchi nasema, hata vinchi vyetu hivi navyo tunapozungumza habari ya unyonyaji wa mtu na mtu, nchi hunyonywa vile vile. Katika kuzungumza ujamaa, nimezungumza habari za mtu anamnyonya mtu mwingine. Lakini ukichuukua mataifa, yako mataifa manyonyaji na mataifa manyonywaji. Yako mataifa yanayotakata hivi hivi, kwa majasho ya watu wengine. Yana mirija mirefu-mirefu, inatoka katika nchi zao inaingia katika nchi za watu wengine: inafyonza tu mali katika nchi zile!

 

Sisi hatuna mrija Uingereza, hatunyonyi chochote Uingereza. Tunanyonya nini Uingereza? Sisi hatuna mrija Marekani, sisi hatuna mrija Ujerumani, hatuna mrija katika nchi yoyote, hata nchi moja. Hakuna nchi tunayofyonza sisi, iwe mali inatoka kule inakuja huku; hata kidogo!

 

Nchi zingine zina mirija: mikubwa, si midogo. Sisi nchi yetu tumeandamwa na mirija. Na sisi tunapowaambia, “Waheshimiwa, msiwe na wasi wasi,” ni kama wale wanaomimina pombe wanawaambia wazee wanywaji, “msiwe na wasiwasi, vyungu tutajaza tu sisi!” Na wale wenye mirija yao huja, husafiri kutoka kwao wakaja huku. Watakuja, wataonana na President.

 

Siku hiyo watazungumza na Mr. President: “Mambo yanakwendaje hapa?” Na mimi nitamwambia, “Usiwe na wasi wasi, bwana, mambo safi tu” “Mirija ni safi” Namwambia “Safi tu” Naweza kuleta mirija zaidi?” Namwambia, “Lete tu bwana.” “Na kufyonza naweza kufyonza?” “Na kufyonza bwana, si lazima?” “ Watu hawawezi kufanya fujo hapa? Mrija wangu hauwezi ukashikwa?” Nitamwambia, “Haushikwi bwana, utashikwaje? Nchi hii tumeishika sisi; nani tena atashika mrija wako?”

 

Basi waheshimiwa hawa wanakuja mara kwa mara, kuja kutazama vyungu vyao huku: kama chungu kimejaa, na kama kazi yetu sisi ya kuchochea na kumimina inatimizwa! Julius anakuwa ni mnyapara mkubwa wa kujaza pombe katika mitungi ya wakubwa. Kazi yake ni kuona kwamba chungu kimejaa pombe wakati wote, na maji ya moto. Wakubwa wenyewe wanakaa kule kwao!

 

Sasa nasema, hata kama kweli matajiri hao wangeweza kuja, wananchi; hata kama baada ya kuapa katika misahafu tunabembeleza, “Njooni!” Kweli ni siasa safi hii? Hii si siasa ya kujipalia makaa vichwani? Ni siasa safi ya kusema leteni tu mirija yenu hapa, na sisi siku zote tutazidi kupanua chungu, msiwe na wasi wasi!” Wakiuliza, “Lakini matata ya NUTA je?” “NUTA tutawangalia sisi bwana, msiwe na wasi wasi, leteni tu.” Hiyo siasa, nasema, hata kama matajiri wangekuja, ndivyo sawa? Kweli ndiyo mnajenga Ujamaa hivyo na Kujitegemea.

 

Kupoteza uhuru

Leo hao rafiki zetu katika nchi zao, wakipenda kuamua jambo lao wanaweza kuamua wapendavyo kabisa. Hawana haja ya kuuliza –uliza, sijui Julius atafikiri nini? Sijui Kaunda atafikiri nini, au Kenyatta atafikiri nini. Wanafanya tu; kama jambo lina manufaa katika nchi yao wanafanya, hawaulizi Julius, hawaulizi Kaunda, hawaulizi Kenyatta; wanafanya wapendavyo.

 

Sisi leo huwezi. Japo jambo ni la manufaa katika nchi yetu wenyewe, Ukilifikiria kulitenda unaogopa! Unaogopa wakubwa; kuna mirija yao hapa. “Watapenda?” Tunajiuliza kama watapenda. Japo tunajua lina manufaa kwa nchi yetu wenyewe hatuthubutu kulifanya bila kujiulizauliza, “Wakubwa watasemaje, jama? Mirija yao iko hapa; kitendo hiki kitagusa mirija yao?—Huku ni kujitawala? Huko ni kujitawala kwa u-prefect, unyapara! Mnalinda mirija ya waheshimiwa wengine; huko ni kujitawala? Kwamba tunaposema tunataka kujitawala, tujitawale barabara, maana yake ni kulinda mirija ya watu wengine katika nchi yetu, na kuiita zaidi kuja? Hata kidogo!

 

Kujitawala ni kujitegemea. Tunataka kuijenga nchi yetu wenyewe. Kazi yetu ni kukata mirija, siyo kuijenga na kuitetea.

 

Kazi yetu ni kujenga, tufike katika hali ya dunia ambapo kila taifa linaishi kwa jasho lake. Tutakuwa na uhusiano wa biashara na mataifa mengine, lakini siyo uhusiano wa mirija na chungu. Sasa siasa yetu hii ni ya kutaka kuomba omba-omba, omba-omba! Kwanza haiwezi kufanikiwa, hawatakuja jamaa hawa kuleta mapesa yao. Hatuwezi kwa njia hiyo kupata pesa tunazohitaji katika maendeleo yetu. Pili nasema, hata kama wangekuja, hivyo ndivyo? Nchi yenu mnawakabidhi wenye mirija; itakuwa mali yenu, hiyo tena? Kama mnataka iwe mali yenu sehemu kubwa ya maendeleo ya nchi yetu, lazima itokane na juhudi yetu wenyewe. Natuzuie watu wengine kutunyonya-nyonya.

 

Hiyo lazima iwe maana ya kujitegemea. Na mifano iko duniani siwezi kuitaja. Hiyo ndiyo njia peke yake ya kuifanya nchi yetu ikaendelea. Lakini sijaonyeshwa duniani nchi moja ambayo imeinuka, inajiheshimu, imeendelea, kwa siasa ya omba-omba. Siijui. Waheshimiwa wale wanaoijua nchi hii, baada ya hotuba wataniambia, “Lakini Mwalimu unakosea; nchi fulani imeomba-omba, mpaka sasa inakaribia kusimama kuwa imara.”

 

Mtaniambia, mimi sijui hata nchi moja. Na ninazijua zinazodidimia, kwa sababu ya siasa ya omba-omba. Na ninazijua zinazosimama imara kwa sababu ya siasa ya kujitegemea. Nchi yetu haitakuwa kinyume, nchi yetu nayo itadidimia, ikiendelea na siasa ya omba-omba. Na nchi yetu itakuwa imara itakapoamua kwamba tunataka kujietegemea, basi!

 

Masharti ya maendeleo

Na tunataka nini ili tuweze kujitegemea? Tumesema kwamba tunataka vitu vinne tu ili tuweze kujitegemea. Kwanza, ardhi yetu  tunayo, nani anasema hatuna aradhi? Tuna aradhi safi, kubwa mara tano ya Uingereza. Na sisi tunafurahi, ardhi tunayo, kitu cha kwanza tunachotaka. Cha pili, watu. Tuna watu milioni 10 tunadhani; lakini inawezekana mwaka huu baada ya kuhesabu si ajabu watu wetu ni kati ya milioni 12 na 15. Si watu wachache tu wengi, tutaendelea.

 

Kweli tunataka Afrika iungane iwe kitu kimoja, lakini sisi si watu wachache, ni wengi. Watu milioni 10, ardhi kubwa. Si wenda wazimu sisi, watu wazima. Tuna akili safi; nini tunachotaka? Tunataka ardhi ambayo tunayo, watu ambao wapo. Cha tatu nini? Siasa safi; siyo siasa omba-omba. Siasa omba-omba siyo siasa ya kuleta maendeleo ya nchi.

 

Tunataka siasa safi, siasa nzuri, siasa kweli ya omba-omba siyo siasa nzuri, tunaikataa hiyo. Na sasa kitu cha nne ni uongozi bora. Uongozi bora, ardhi tunayo, watu wapo, siasa ndiyo hiyo tunatamka siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ndiyo siasa safi.

 

Sasa hiari ya TANU. Tunadhani TANU inaweza kutoa uongozi bora, msipotoa tutasumbuana. Tunadhani TANU watatoa uongozi bora na tutakuwa katika shughuli ya kutengeneza uongozi bora wa TANU. Vitu hivyo vine vipo, na kama vinataka msasa, kama uongozi unataka msasa tutaupiga msasa uongozi.

 

Sasa basi wananchi, ardhi tunayo, watu wapo, siasa ni hiyo, tusiweze kuendelea kwanini? Tuendelee na siasa ya omba-omba, tunategemea watu wengine; na kwanini tutegemee watu wengine? Hivyo wananchi ndivyo tulivyozungumza: Kwamba tuache siasa ya omba-omba, tuingie katika siasa ya kujitegemea. Hiyo nayo wananchi ni rahisi kuielezea.

 

Nayo inaeleweka vilevile, si ngumu kuielewa. Si ngumu kuelewa heshima ya Maganga inatokana na kujitegemea, haiwezi kutokana na omba-omba. Ni rahisi kuelewa kwamba heshima ya nchi yoyote, si yetu, sin chi gani, haitatokana na siasa ya omba-omba, itatokana na siasa ya kujitegemea. Si vigumu kuelewa kwamba tunajidanganya tukielewa kwamba kutegemea zaka za Jumapili kunaweza kusaidia nchi yetu kuendelea. Hata kidogo. Haya nasema ni mambo rahisi sana kuelewa.

 

Maana yake ni kazi

Kutimiza kuna masharti yake; kunataka jitihada, kunataka kazi. Na tunapojidanganya ni pale tunapodhani kwamba basi tutakwepa kazi halafu tutaendelea hivyo, tutaendelea kwa kuomba-omba. Hapana haja ya kufanya kazi, tutaendelea tu; tutaomba halafu tutaendelea. Tunajidanganya; kuendelea kunataka kazi.

 

Na kazi binadamu huwa hawapendi, hawapendi kufanya kazi; wanapenda kufanyiwa kazi. Lakini hayo ni mambo ya kujidanganya, ndipo hapo unapokuja uongozi wa TANU. Na nyinyi wananchi, tunataka kweli kujitegemea? Tunataka kweli nchi yetu iwe barabara? Kama tunataka nchi yetu iwe barabara, ijitegemee, lazima tukubali maana ya kujitegemea. Maana ya kujitegemea ni kwamba lazima tufanye kazi. Maana ya kujitegemea vilevile ni kwamba, lazima tufunge mikanda.

 

Ujamaa ni Imani (2), Mwalimu Julius Nyerere, Februari 5, 1967

 

Please follow and like us:
Pin Share