Katika “decentralization” kulitokea vituko katika utawala. Mtu kama daktari wa mifugo kasomea mifugo (shahada ya veterinary) eti anateuliwa kuwa Afisa Tawala Mkuu wa Mkoa (Regional Administrative Secretary). Mkuu wa shule ya sekondari anateuliwa kuwa Afisa Utumishi Mkoa (Regional Personnel Officer) na kadhalika, na kadhalika. Utawala wote ukavurugika mara moja.

Hapakuwa na mtaalamu wa kusimamia zile “General Orders”. Basi, mambo yakawa yanakwenda kwa tafsiri yangu, kienyeji. Ule msahafu wa matumizi ya fedha za Serikali (Financial Regulations) nao uliachiliwa mbali na kuanzia hapo utawala bora ulikufa kifo cha mende!


Kulikuwa na utaratibu wa kipaumbele serikalini tukiita “Staff List” kuanzia Gavana wa nchi hii, Chief Secretary hadi mtumishi wa chini. Walijulikana hivyo upandishaji cheo ulifuata hiyo “Staff List” kutoka utumishi. Vitabu hivyo ninavyovitaja vinaweza kuonekana kule Idara ya Utumishi na kwenye archives (mambo ya kale) kwenye maktaba zao.


Nini basi matokeo ya mvurugiko huo wa utawala bora wa sheria na wa haki? Kitu cha kwanza kilichojitokeza dhahiri ni NDUGUNAIZESHENI ikaingia katika Serikali. Watu wakaajiriwa kwa maombi ya vikaratasi (chits) na kujuana na wala si kwa sifa za nafasi ile ya kazi.


Pili, RUSHWA ikapenyapenya hapo hapo, watu wakawa wanavaa mashati ya mikono mirefu kila walipotafuta kazi maofisini au katika kupata stahili zao kama funguo za nyumba, sharti atoe kishikia funguo au azunguke mbuyu. Ni misemo ya kawaida mitaani wakati ule.

 

Hivyo, hapakuwa na utaratibu wa haki wa kupandisha vyeo serikalini wala utaratibu wa haki wa ajira. Hapo hakukuwa na utawala bora. Ulikuja kuzuka usemi kuwa hapa Tanzania kupata kazi kunategemea sana unajuana na nani na wala si unajua nini au utaalamu wako ni upi. Watu wengi wakisema, “In Tanzania what matters is know who BUT NOT know how! Ujuzi haukuthaminiwa tena. Huo basi si utawala bora, bali utawala holela.

 

Nimetaja machache yaliyotufikisha hapa tulipo kiutawala. Maofisa utawala wenye ile taaluma ya kiofisi waliwekwa pembeni, badala yake ndugu, marafiki au wafadhili walichomolewa huko waliko na kutua serikalini kuendesha ofisi za Serikali kiutawala.

 

Nakumbuka Katibu Mkuu mmoja mwaka 1975 kutoka wizara fulani alimokuwa na ujuzi nao, akateuliwa eti akawe Meneja Mkuu wa TAZARA! Yeye Makerere alisomea kilimo (Bsc Agric. Hon) anapelekwa TAZARA kuwa mtawala, kweli hatafanya madudu huyu?

 

Aliogopa sana akakimbilia kwenye shirika la Umoja wa Mataifa alikotumia ujuzi wake barabara kwa miaka mingi na kutupatia sifa nzuri tu.

 

Kuna mifano mingi ya matumizi mabaya ya nguvu kazi – wataalamu wale wasomi wenye shahada. Bwana shamba (afisa ugani mkuu) anateuliwa kuwa mkuu wa benki. Jamani kasomea wapi au ana ujuzi gani wa kibenki? Mparanganyiko ule wa kutumia vibaya wataalamu waliohitimu kutoka Makerere siku zile, ulichangia kuozesha utawala bora wa haki na wa sheria.

 

Ingawa kuna ukweli kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na wasomi wenye utaalamu wa fani mbalimbali wachache sana katika nchi yetu wakati ule, je, leo hii hali namna ile ya miaka ile kweli bado ipo katika nchi yetu? Mbona sasa wasomi wenye shahada wameshafurika hapa nchini?

 

Nilipokuwa mkoani Mara (1971-1972) Admin Secretary na RC hawakuiva katika chungu kimoja. Basi, yule Regional Administrative Secretary aliswekwa mahabusu kwa saa 24. Huyu mtu nilisoma naye St. Mary’s Tabora.

 

Basi, nilikwenda kumwona kule kituo cha Polisi alikoswekwa mahabusu. Alianiambia na kunilalamikia kutiwa ndani bila kupata nafasi ya kujieleza. Baada ya kutolewa mahabusu, Rais Nyerere asubuhi ile ile alimhamishia Mkoa wa Singida kwenda kuendelea na kazi yake ya Regional Administration kutoka kule Mara.  Kwa kweli wasingeweza kuhudumia wananchi katika hali ile ya uhasama (antagonistic situation).

 

Nimetoa baadhi ya mifano niliyoijua binafsi, kuthibitisha tu wapi wanasiasa walipindisha dhana nzima ya utawala bora katika nchi yetu kwa kisingizio cha chama kushika hatamu.


 

By Jamhuri