EDITHA MAJURA

Imebuka sintofahamu kubwa kutokana na uvunjaji wa jengo la Chako ni Chako mjini Dodoma, baada ya kuwapo harufu ya eneo hilo kuviziwa na “wakubwa”, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imevunja jengo lililokuwa maarufu kwa jina la Chako ni Chako, ambalo kwa miaka mingi limekuwa likitumiwa kwa biashara ya kuuza nyama ya kuku waliochomwa – ‘Kuku choma’.

Uchunguzi unaonyesha kuwa taratibu za kuvunja jengo hilo zilikiukwa kwa kiasi kikubwa. Ilani iliyotolewa ya kuvunja jengo ilikuwa na jina tofuati na mmiliki halisi wa kiwanja. Manispaa inadai kuna viwanja viwili eneo moja vyote vikiwa na Na. 116.

Manispaa imevunja jengo bila kufuata matakwa ya kisheria ya kutimiza siku 30 za notisi na 45 za mwenye jengo kupata fursa ya kupinga ilani hiyo, lakini yote hayo wanajitetea wakisema Manispaa imefanya makosa ya kibinadamu kuchanganya majina ya mwenye nyumba iliyovunjwa na mtu mwingine.

Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa mwenye nyumba ya Chako ni Chako aliomba kibali cha kukarabati jengo kwa kuezeka paa, ila alipotoa mabati akakuta nyumba haina hata renta. Baada ya kubaini hilo aliamua kufunga renta na kuezeka upya, lakini hilo Manispaa ikaliona ni kosa linalostahili kuvunja hiyo nyumba.

Mdhibiti wa Majengo wa Manispaa ya Dodoma, Mhandisi Ally Bellah, kwa kibali cha Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hidaya Maeda, amelieleza JAMHURI kuwa wamevunja jengo hilo kwasababu aliyepewa kibali cha kukarabati paa lake, Charles Edwin Mamuya, amekiuka masharti ya kibali hicho.

“Badala ya kukarabati paa kwa maana ya kubadilisha bati tu, yeye alibomoa na kujenga kuta za jengo ili kuliimarisha kabla ya kupaua jambo ambalo haliruhusiwi, kwasasa nyumba zote zilizo katikati ya mji zinapochakaa kiasi cha kukosa sifa ya kutumika inatakiwa zijengwe upya tena ujenzi wa gorofa,” amesema Mhandisi Bella.

Amesema walipobaini anakiuka masharti walimpelekea hati ya kumzuia kuendelea na ujenzi huo, akakaidi. Wakapelekea hati ya kumtaka abomoe jengo hilo ndani ya siku thelathini, hakuisaini, ikawabidi waibandike ukutani na kwamba bado aliendelea na ujenzi, hali iliyotafsiriwa kuwa ameidharau serikali.

“Mkuu wa Mkoa akasema hatuwezi kuendelea kudharaulika, lazima tuoneshe kuwa serikali ina mamlaka, akaagiza jengo livunjwe,” amesema Mhandisi Bella.

Ilani iliyobandikwa ukutani inaonesha iliandikwa Desemba 05, mwaka jana na inamtaka Mamuya, avunje jengo hilo ndani ya ya siku thelathini tangu Februali 5, mwaka huu.

Pia ameelekezwa kuhuisha umiliki wa ardhi hiyo na kuwakilisha michoro ya jengo la kudumu kwa mujibu wa masharti atakayopewa na kwamba ujenzi unaotakiwa hapo ni ghorofa.

Hata hivyo, JAMHURI limebaini kuwa hati aliyopewa ikimzuia kuendelea na ujenzi, iliyoandikwa Januari 23, mwaka huu, imeandikwa jina la Sleyum Alli, Kiwanja Na. 116 Kitalu V eneo la Airport tofauti na taarifa zilizo kwenye kibali cha ujenzi huo, zinazomtaja Charles Edwin Mamuya, Kiwanja Na. 116 eneo la Airport (bila kitalu).

Manispaa kupitia ilani iliyoibandika ukutani, ilitoa maelekezo. Siku tisa baadaye Manispaa ikabomoa jengo bila kibali cha Mahakama kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya Mwaka 2007, kifungu cha 74(3)(4)na (5).

Alipoombwa na JAMHURI kuzungumzia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge, amesema hahusiki na kutoa kibali cha ujenzi, kuzuia ujenzi, wala uvunjaji wa majengo yanayojengwa kinyume cha sheria na taratibu, bali anayehusika ni Manispaa hivyo mazungumzo hayo yafanywe na Mkurugenzi, Godwin Kunambi.

Kunambi hakupatikana hivyo Kaimu Mkurungezi Maeda, alimpa kibali cha kuzungumza Mhandisi Ally Bellah kutoa ufafanuzi kuhusu sintofahamu hiyo.

Mhandisi Bellah, amesema kiwanja Na. 116 kitalu V kinachomilikiwa na Aleyum Alli, kipo maeneo jirani na kilipo kiwanja kingine Na. 116 kisicho na Na. kitalu eneo la Airport, hivyo kumpatia Mamuya ilani yenye utambulisho huo usio jina lake, lakini ni makosa ya kibinadamu ingawa ‘contents’ (maudhui) kwenye ilani hiyo ndiyo yalikusudiwa kuelezwa kwake (Mamuya).

Amesema pamoja na kusaini ilani hiyo, Mamuya, hakuacha kujenga na wao walipobaini makosa yaliyofanyika, walimpelekea ilani nyingine ambayo ilimtaka kubomoa jengo hilo ndani ya siku thelathini, lakini hakuisaini hivyo wakalazimika kuibandika ukutani.

Ilani hiyo ambayo JAMHURI limeishuhudia, imeandikwa tarehe 5 Desemba 2017.

Mhandisi amesema wamebomoa jengo hilo bila kibali cha Mahakama kwasababu sheria hiyo haiwalazimishi kuomba kibali mahakamani; “Ukisoma vizuri pale limetumika neno ‘may’ siyo ‘shall’.”

Na kwa upande wa kutosubiri muda wa siku thelathini uliotolewa kwa Mamuya kubomoa jengo lake ufike, amesema “Uzoefu umetuonesha tunaposubili siku thelathini, wengi wanatumia muda huo kukamilisha ujenzi na tunakuta jengo limeishaanza kutumiwa hali inayosababisha mambo kuwa magumu zaidi,” ameeleza Mhandisi Bellah.

Kwa upande wake Mamuya, amelieleza JAMHURI kuwa ana masikitiko makubwa kwa kiwango cha kutoweza kuzungumzia tukio hilo kwa kina kwasababu ni uamuzi uliotolewa na mamlaka halali, yenye dhamana ya kusimamia ujenzi katika eneo hilo hivyo hana budi kutii na kuzingatia maelekezo yanayotolewa ila akaomba vyombo vyenye kutoa haki viliangalie suala hili kwani wamemtia hasara.

Amesema jengo hilo lilijengwa tangu Mwaka 1961 na marehemu baba yake ambaye amefariki miaka ya 1980 na hivyo jengo kubaki kwa warithi wake ambao ni yeye na ndugu zake chini ya msimamizi wa mirathi ambaye ni dada yao mkubwa.

“Mimi niliagizwa tu na familia kuja kufanya ukarabati kwasababu paa lilichakaa sana kiasi cha kuvuja mvua zilipokuwa zikinyesha, lakini kwa bahati mbaya, sikufanikiwa na kwakweli sina cha kusema zaidi ya hiki,” amesema Mamuya huku akilengwa na machozi.

 

Wananchi wanena

Harrison George, mkazi wa Uzunguni amepongeza hatua ya serikali mkoani humo kusimamia nidhamu katika ujenzi mjini hapo, lakini akashauri kuwa uchunguzi wa kina ufanywe ndani ya mamlaka zinazohusika na uratibu wa Mipangomiji kwani inaashiria kuwepo watumishi wasiyokuwa waadilifu.

Amesema wananchi wanaharibiwa mali zao kwasababu moja au nyingine watumishi wanaotakiwa kuwaelekeza cha kufanya na kutofanya hawatekelezi majukumu yao ipasavyo, hivyo kuna haja ya kuwajibisha watumishi hao sawa na wanavyowajibishwa wananchi.

“Haiingii akilini, mtu afanye ukarabati kuanzia kubomoa jengo na kulijenga upya hadi kufikia hatua ya kupaua, ndipo mamlaka inajitokeza kuzuia na kumbomolea kwa nguvu ni dhahiri kuna waliokuwa wanamlinda, pengine wameshindwa kuelewana mwishoni,” ameeleza George.

Maria Shao, mkazi wa Maili Mbili amesema ikiwa serikali imedhamiria kuhakikisha sheria za Mipango Miji zinazingatiwa katika ujenzi, iboreshe na kuongeza kasi katika kushughulikia hatua zote zinazoendana na ujenzi wenye kuzingatia sheria hizo.

“Hati za kumiliki ardhi yake zipatikane bila ukilitimba, kupitisha michoro ya majengo na kutoa vibali vya ujenzi vipatikane kwa urahisi na mtu aelezwe hasara na faida za kujenga au kutojenga kwa kuzingatia sheria za Mipangomiji, bila shaka kila mtu atajenga kwa taratibu sahihi,” amesema Shao.

Kwa takriban wiki mbili sasa serikali inakagua na kubomoa majengo yote yaliyojengwa bila vibali au bila kuzingatia Sheria za Mipango Miji mkoani hapa.

Dk. Mahenge, alipoombwa kuelezea agizo lake kwa Manispaa kuhusu kubomoa jengo la Chako ni Chako, akasema hawezi kuzungumza chochote kwa wakati huo.

Akasema angewaelekeza Manispaa wafanye mkutano na vyombo vya habari, Jumatatu (jana) ili waeleze kinagaubaga kuhusu kuvunjwa kwa jengo hilo na operesheni hiyo kwa ujumla, ili kuweka kumbukumbu sahihi.

By Jamhuri