Uwaziri Mkuu moto

Dk. John Magufuli akitarajiwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wiki hii, mjadala wa nani atakuwa Waziri Mkuu na nani atakuwa Spika wa Bunge la Jamhuri, umeshika kasi.

Kwa mujibu wa Katiba, mara baada ya kuapishwa Dk. Magufuli atatakiwa awe ameteua Waziri Mkuu ndani ya siku 14.

Sehemu ya tatu ya sura ya pili ya Katiba inayozungumzia Muundo wa Serikali, inamtaja Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri.

Inasema: “Kwa mujibu wa sheria ya 1992 Na.20 Ibara ya 9; “Ibara ya 51 ya Katiba ya Jamhuri; kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, atakayeteuliwa na Rais  kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge.”

“(2) Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku 14 baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni au kama hakuna chama cha siasachenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi, kuwa Waziri Mkuu.

“Naye hatashika madaraka hayo hadi kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wabunge wengi.

Nafasi ya Waziri Mkuu kwa sasa inashikiliwa na Mizengo Pinda, ambaye kuna dalili zote za Kikatiba yeye kuiachia nafasi hiyo keshokutwa baada ya Dk. Magufuli kuapishwa.

Wanaotajwa ni pamoja na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo; Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe; Mbunge wa Isimani, William Lukuvi; Mbunge wa Bumbuli, January Makamba; na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba. Hao ni miongoni mwa wana CCM wanaotajwa tajwa.

Hawa wote wameshakuwa viongozi katika Serikali iliyopita, hali inayowaweka kwenye kundi la sintofahamu, hasa kwa kuzingatia kuwa Dk. Magufuli, amenuia kwa dhati kuwa na sura mpya zenye mwamko mpya wa utendaji kazi.

Hata hivyo, kuna habari kuwa Dk. Magufuli, atapenda kumpata Waziri Mkuu, ambaye hatakuwa na “makeke” kama yake ili Serikali yake isiogopwe mno.

Profeaa Muhongo ameingia rasmi katika siasa za juu mwaka 2002 akiteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Chini ya uongozi wake aliweza kufanya mageuzi makubwa katika wizara hiyo pamoja na kupambana na tatizo la mgawo wa umeme. Aliweza kuzuia ufisadi wa bei za mafuta uliofanywa na watumishi wa TANESCO, Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara.

Anakumbukwa kwa kusimamia vema masuala ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA; na pia kwenye masuala ya gesi. Amepelea vijana wa Tanzania kwa mamia nje ya nchi kusomea masuala ya gesi na madini.

Kwa wanasiasa wasomi, wasifu wa Profesa Muhongo hauna mfano wake; na pengine kwa wabunge wote wa sasa ni yeye mwenye wasifu wa kisomi ulioshiba barabara.

Pamoja na uchapaji kazi, Profesa Muhongo, alijichumia maadui kutokana na kauli zake kali zenye majibu ya kisayansi badala ya kisiasa. Majibu hayo yalimfanya achukiwe na baadhi ya watu, hasa wale waliokuwa na maslahi yao binafsi; hata wakahakikisha anaondolewa katika Wizara ya Nishati na Madini wakati wa sakata la ESCROW. Kwenye sakata hilo, yeye na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi, hawakupatikana na hatia ya uchotaji fedha, jambo lililomwezesha kurejea katika siasa na pia Maswi kuteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Manyara.

Kwa uchapaji kazi, huyu ni kama Rais Magufuli. Hana simile, na wala hajui kumung’unya maneno. Sifa za kuwa Waziri Mkuu anazo, lakini wachunguzi wa mambo wanasema misimamo na ukali wake ukiwekwa pamoja na wa Rais Magufuli, unaweza kupitiliza, hivyo wanaona heri arejeshwe kwenye Wizara ya Nishati na Madini.

 

WASIFU

Profesa Dkt Sospeter Muhongo, mwanazuoni maarufu, mwanajiolojia mbobevu na Mbunge wa Kuteuliwa, amewahi kuwa Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (April 2012- Januari 2015).

Serikali ya Ufaransa ilimtunukia Cheo cha Afisa Mwenyetunu ya Kitaaluma Iliyotukuka – Ordre des Palmes Académiques (Iliyoanzishwa na Mfalme Napoléon Mwaka 1808) na ni mtu wa kwanza kupokea Tuzo (Mwaka 2004) inayoheshimika sana kwa Jamii ya Wanajiolojia wa Afrika ya Profesa Robert Shackleton (UK) (Geological Society of Africa’s prestigious Profesa Robert Shackleton Award), kwa ajili ya utafiti wa kipekee kuhusu Jiolojia ya Afrika ya miamba yenye umri wa zaidi ya miaka Milioni 500 (Precambrian Geology of Africa).

Kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kimataifa katika Sayansi na Ustawi wa Jamii ulimwenguni, Profesa Muhongo amepewa nafasi nyingi zenye kuheshimiwa na wasomi na wataalamu maarufu duniani, pamoja na kutambulika kwa ngazi za juu kabisa na Vyama na Taasisi zao za kitaaluma, kwa mfano: An Honorary Fellow of the Geological Society of London (Ilianzishwa mwaka 1807), Honorary Fellow of the Geological Society of America (Ilianzishwa Mwaka 1888), an Honorary Research Fellow of the Chinese Academy of Geological Sciences (Ilianzishwa Mwaka 1956).

Ni Mshiriki wa Ngazi ya Juu (Fellow) wa Akademia ya Sayansi ya Nchi Zinazoendelea (FTWAS), Mshiriki wa Ngazi ya Juu (Fellow) wa Chama cha Wanajiolojia wa Afrika (FGSAf) , Mshiriki wa Ngazi ya Juu (Fellow) wa Akademia ya Sayansi ya Afrika (FAAS) na Mshiriki wa Ngazi ya Juu (Fellow) wa Akademia ya Sayansi ya Tanzania (FTAAS) na nyingine kadhaa. Ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Tume ya Ramani ya Jiolojia ya Dunia (CGMW) na pia Mhariri Mkuu Mstaafu wa Jarida la Afrika la Sayansi za Miamba na Madini (The Journal of African Earth Sciences, Elsevier). Profesa Muhongo ni Mshindi wa Mwaka 2014 wa Tuzo ya Heshima ya Jamii ya Wanasayansi wa Jiolojia na Uchimbaji Petroli na Gesi Asilia ya Nigeria (NMGS)/AMNI ya Profesa M.O. Oyawaye.

Profesa Muhongo aliongoza na kusimamami mabadiliko endelevu ya ubunifu na ugunduzi katika Sekta za Nishati na Madini nchini mwetu kwa kuingiza sera mpya na kutengeneza nyaraka za kisheria, ameongeza idadi kwa wingi ya rasilimali watu iliyopata mafunzo mazuri ya kitaaluma katika Tasnia ya Mafuta na Gesi Asilia. Amesimima ongezeko la kasi kubwa ya kampeni ya usambazaji umeme vijijini, na amesimamia usambazaji wa haraka na wa uhakika wa umeme mijini. Amesimamia punguzo kubwa la gharama za kuunganishiwa umeme vijijini na mijini. Amesimamia ongezeko la mapato

katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kutokana na kodi na tozo mbalimbali kwenye madini yetu. Baadhi ya wachimbaji wadogo wamepatiwa mafunzo na ruzuku ya kuboresha uchimbaji wao. Tarehe 28.02.2015, Chama cha Wachimbaji Wadogo nchini (FEMATA) kilimteua, kwa kauli moja, Profesa

Muhongo kuwa Mshauri Mkuu wao.

Profesa Muhongo alisimamia utayarishaji wa mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Umeme nchini, ikiwemo TANESCO, na Juni 2014 Wizara ya Nishati na Madini ilitangaza mipango na miradi itakayotekelezwa kuhakikisha Taifa linapata umeme mwingi wa kutosha mahitaji yake, umeme unaopatikana kwa urahisi na kwa uhakika, umeme wa bei nafuu na umeme wa ziada (biashara) kwa manufaa ya uchumi wetu – Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap 2014-2025, Powering Vision 2025.

Profesa Muhongo amevutia uwekezaji mpya (kutoka ndani na nje ya nchi) wenye mitaji midogo namikubwa kwenye Sekta za Nishati, Madini, Mafuta na Gesi Asilia. Haya yote yamechangia ukuaji mzuri wa uchumi wetu.

Yeye ni Profesa Kamili (mstaafu) wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Profesa wa Heshima wa Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini. Ni mjumbe wa bodi kadhaa za uhariri wa majarida ya sayansi na vijarida vya sayansi, teknolojia na ubunifu. Yeye ni Mhariri Mwandamizi wa Kitabu cha Mwaka 2009 kiitwacho: Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii: Simulizi za Mafanikio kutoka Afrika (“Science, Technology and Innovation for Socio-Economic Development: Success Stories from Africa”).

Profesa Muhongo na watafiti wenzake wamechapisha ramani kwa kuzingatia dhana na maarifa ya kisasa ya Jiolojia, kama vile: Jiolojia na Mashapo Makubwa ya Madini ya Afrika, Jiolojia na Mashapo ya Vito vya Thamani vya Afrika Mashariki na Ramani ya Jiolojia na Madini ya Tanzania. Hakuna mikopo au misaada ya fedha ilitumika kutengeneza ramani hizi. Ramani hizi zinatumika kupanua na kukuza uwekezaji mpya katika Sekta ya Madini Barani Afrika.

Profesa Muhongo alikuwa Rais wa Chama cha Wanajiolojia wa Afrika (1995-2001). Alikuwa Mkurugenzi Mwanzilishi (2005-2010) wa ICSU Ofisi ya Sayansi ya Kanda ya Afrika, Pretoria, Afrika Kusini. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UNESCO-IUGS-IGCP Programu ya Kimataifa ya Sayansi ya Jiolojia (2004- 2008), na Mwenyekiti (2007-2010) wa Kamati ya Programu ya Kisayansi (SPC) ya Mwaka wa Kimataifa wa Sayari ya Dunia uliotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN-IYPE).

Profesa Muhongo aliteuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mgombea (2009) wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO.

Alikuwa Mwenyekiti (1999-2005) wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), Tanzania; na alikuwa Mkuu wa Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (1997-2000). Profesa Muhongo alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi ya Serikali ya Tanzania kuhusu ajali mbaya ya vifo katika migodi ya Mererani (2002). Profesa Muhongo alisimamia kwa umakini mkubwa uboreshaji wa raslimali watu, majukumu, miradi na utendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC).

Profesa Muhongo amechapisha zaidi ya makala (publications) 200 za sayansi ya hadhi ya juu zikiwa ni za kiutafiti zenye kukubaliwa na kurejelewa na watalaamu Duniani kote. Ametoa mihadhara ya kisayansi zaidi ya 500 akiwa ndiye Mzungumzaji Mkuu (Keynote Speaker) katika Mikutano ya

Kimataifa na Kitaifa. Kwa zaidi ya miongo miwili, Profesa. Muhongo ameandaa vikao zaidi ya 100 vya mikutano ya vikundi vya wataalamu wa Kitaifa na Kimataifa vya sera, teknolojia na sayansi za nishati, miamba, madini, maji, tabianchi na mazingira. Amekuwa Mwandishi Mkuu wa mikutano ya sera za sayansi ikiwa ni pamoja na “Sayansi na Afrika” ambayo inadhaminiwa na Kamisheni ya Umoja wa

Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), Kamisheni ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) na washirika wake.

Profesa Muhongo amepata tuzo mbalimbali za kiuanazuoni na kitaalamu, ametambuliwa na kupata hibafedha kwa kazi mbalimbali za kitaaluma pamoja na kutunukiwa fedha za utafiti. Ameshirikiana na wanasayansi mabingwa wa Mabara yote kwenye tafiti za kisayansi. Alisomea Jiolojia katika Chuo

Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania) na GÓ§ttingen (Ujerumani). Alihitimu na kutunukiwa shahada ya Dr.rer.nat. kutoka Technical University of Berlin, Ujerumani.

Profesa Muhongo anaongea, na kuandika kwa ufasaha na umahiri mkubwa Kiswahili, Kiingereza na Kijerumani, na kwa wastani kwa lugha ya Kifaransa.

Profesa Dkt. Sospeter MUHONGO (Officier, Ordre des Palmes Académiques) 20 March 2015 FGSAf, FAAS, FASI, FASSAf, FTAAS, FGIGE, FTWAS, HonFCAGS, HonFGSA, HonFGS, CGeol, EurGeol

 

Lukuvi

Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tangu Januari 14, mwaka huu alishika nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Anna Tibaijuka.

Kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge. Alishika ofisi hiyo kuanzia Novemba 28, 2010 kutoka kwa Philip Marmo.

Alipoteliwa nafasi ya Waziri wa Ardhi, Rais Jakaya Kikwete alimteua Jenista Mhagama kushika nafasi yake.

Mwanasiasa huyo kutoka Jimbo la Isimani Iringa, alizaliwa Agosti 15, 1955. Dk. Magufuli alizaliwa mwaka 1959.

Alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na hata alipoteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lukuvi amefanya kazi kubwa na ya kupigiwa mfano kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Anajulikana kama mchapakazi hodari ambaye nafasi ya uwaziri mkuu inaweza kumfaa.

 Lukuvi kitaaluma ni mwalimu aliyepata utaalamu huo ngazi ya cheti kutoka Chuo cha Ualimu Tabora mwaka 1975 na baadaye alijiunga mafunzo ya siasa Lindi mwaka 1976.

Mwaka 1980 alifanya kozi ya mafunzo ya ulinzi na usalama mkoani Iringa.

Mwaka 1983, Lukuvi alifanya stahashaha (Diploma) katika Chuo cha Siasa jijini Moscow, Russia na baadaye Kozi ya Uongozi mwaka 1985. Pia alifanya kozi ya kompyuta katika Chuo cha Kompyuta Dares Salaam mwaka 1998.

Kadhalika ana cheti kutoka Chuo cha Uchunguzi wa masuala ya siasa kutoka Afrika Kusini alikohitimu kozi hiyo mwaka 1994 na kuhitimu shahada ya ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Washington, Marekani.

Amepata kuwa Mkuu wa Wilaya Bukoba kati ya mwaka 1994 na 1995 kabla ya Rais Benjamin Mkapa kumteua kuwa Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana 1995 hadi 2000.

Mwaka 2000 hadi 2005, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera) kabla ya kupelekwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hadi 2006 na baadaye kurejeshwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge ambako alishika ofisi hiyo kuanzia Novemba 28, 2010. Pia amepata masomo ya juu katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Kitengo cha Oganaizesheni ya Vijana, Makamo Makuu ya Chama Cha Mapinduzi – CCM – (1992 1993).

Katibu wa Mkoa wa Chama Cha Mapinduzi –1989 1992 na kuanzia mwaka 1984 hadi 1989 alikuwa Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni na Katibu wa Umoja wa Vijana (1980 hadi 1984).

 

Dk. Mwakyembe

Dk. Harrison Mwakyembe ni Waziri wa tano wa Wizara ya Afrika Mashariki tangu Jumuiya hiyo irejee mwaka 1999.

Wengine waliopata kuwa mawaziri wa wizara hiyo ni Samwel Sitta, Andrew Chenge, Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Kadhalika alikuwa Waziri wa Uchukuzi kuanzia Mei 7, 2012 hadi Januari 24, 2015 akishika nafasi ya aliyewahi kuwa Mbunge wa Tanga Mjini, Omari Nundu.

Kabla ya kuwa Waziri Kamili, Dk. Mwakyembe alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, alikofanya kazi kuanzia Novemba 28, 2010 hadi Mei 7, 2012 chini ta Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

Dk. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela tangu Desemba 2005, alizaliwa Desemba 10, 1955.

Elimu zake za Sekondari alizipata Shule ya Wavulana Tabora na Milambo.

Shahada ya kwanza na uzalimili alizifanya Chuo Kikuu Dar es Salaam wakati ile ya uzamivu aliipata Chuo Kikuu cha Hamburg, Ujerumani. Pia amesoma Chuo Kikuu cha Turin, Italia.

Uzoefu wake wa kisiasa ni kuwa mbunge kuanzia mwaka 2005. Kitaaluma ni mwanasheria na Mwandishi wa habari. Alisoma uandishi wa habari katika Shule ya Waandishi wa Habari Tanzania (TSJ) mwaka 1975-1977 na kutunukiwa Stashahada.

Amewahi kutumikia taaluma hiyo katika Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) mwaka 1978-1980.

Anajulikana kwa misimamo na ujasiri wake. Mwaka 2007 aliongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond. Ripoti ya Tume hiyo ndiyo iliyosababishwa kung’oka madarakani kwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa.

Dk. Mwakyembe, mbele ya umma anaonekana mtu jasiri, lakini ndani ya wizara alizoongoza kumekuwapo uoungufu wa hapa na pale. Akiwa Uchukuzi, kukaibuka sakata ya ununuzi wa mabehewa mabovu yaliyoligharimu Taifa Sh zaidi ya milioni 400. Mara zote amejitetea kwamba hahusiki na kashfa hiyo.

Mkoa wa Mbeya haujawahi kumtoa kiongozi wa juu kitaifa zaidi na nafasi ya uwaziri. Safari hii anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu ili aweze kumsaidia Rais Magufuli katika uendeshaji Serikali ya Awamu ya Tano inayokabiliwa na changamoto nyingi.

 

Makamba, Mwigulu

Hawa ni vijana wasomi ambao wamekuwa naibu mawaziri katika uongozi wa Awamu ya Nne. Makamba amekuwa Msaidizi wa Rais Kikwete, kabla ya kuingia kwenye ubunge.

JANUARY MAKAMBA:

Makamba ni miongoni mwa  vijana machachari katika siasa za Tanzania akiwa na sifa kubwa ya kuendesha siasa za kisasa na zinazowavutia vijana wengi. Alizaliwa Januari 28, 1974 mkoani Singida akiwa ni mtoto mkubwa kati ya watoto wanne wa Mzee Yusuph Makamba.

January ambaye kwenye Serikali ya awamu ya nne anamaliza akiwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, ana shahada ya masuala ya amani aliyoanza kuisoma katika Chuo cha Quincy, Massachusetts, Marekani na kumalizia Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana kilichoko Minnesota, Marekani.

Shahada ya uzamili kuhusu Uchambuzi na Usuluhishi wa Migogoro aliifanya kwenye Chuo Kikuu cha George Mason – Marekani, mwaka 2004 kabla ya kurejea nchini na kuajiriwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwa Ofisa wa Daraja la Pili kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Msaidizi Binafsi wa Rais Katika Mambo Maalumu.

 

Mwaka huu aliomba ridhaa ya kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi kwenye urais, na kufanikiwa kuingia kwenye tano bora.

Kama ilivyo kwa Makamba, Nchemba naye aliomba ridhaa hiyo, lakini aliishia kwenye mchujo. Makamba ni miongoni mwa injini za mafanikio ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika, kama ilivyokuwa kwa Nchemba.

Kama Dk. Magufuli, anataka kuwa na Waziri Mkuu kijana, bila shaka majina haya mawili yatakuwa miongoni mwa majina atakayoyatazama kwa jicho la kipekee.

Hata hivyo, watu walio karibu na Dk. Magufuli wanasema kiongozi huyo anaweza kuteua jina la Waziri Mkuu na hivyo kuibua mshangao mkubwa miongoni mwa wananchi, kwani anaweza kumteua mwanasiasa asiyekuwa na jina.

 

‘Vita ya u-Spika’

Vuta nikuvute ipo kwenye kiti cha Spika. Habari za chini chini zinasema Spika wa sasa, Anne Makinda aliyemaliza muda wake baada ya kuongoza Bunge la 10; ameshaonyesha nia ya wazi ya kuwania nafasi hiyo.

Pamoja na Makinda, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Naibu Spika wa sasa, Job Ndugai (Kongwa) na waliopata kuwa wenyekiti wa Bunge hilo – Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama; na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.

Lakini katika hatua nyingine, aliyewahi kuwa Mbunge wa Bunge hilo, Samuel Sitta, naye anatajwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho. Sitta alijengea umaarufu mkubwa kati ya mwaka 2005-2010 kabla ya kushindwa kuwania tena nafasi hiyo kutokana na kutokidhi sharti la jinsi ya kike kama lilivyowekwa na CCM.

Baadaye wakati wa Bunge Maalum la Katiba, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wake. Anakumbukwa kwa msimamo wake wa “kuchakachua maoni ya wananchi”; hali iliyomsababishia maadui wengi, hasa kutoka kwa wale waliokuwa wakitaka maoni ya Kamati ya Jaji Warioba yaheshimiwe.

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrewe Chenge, naye anatajwa tajwa kuwamo kwenye orodha ya watu wanaotaka kuwania nafasi hiyo.

Nafasi kwa Sitta na Makinda, inaweza kuwa finyu pengine kutokana na umri wao. Viongozi hao wamekuwa kwenye safu za uongozi wa Taifa hili tangu uongozi wa Awamu ya Kwanza.

Ndugai, anaweza kuwa kwenye wakati mgumu kutokana na misimamo yake ambayo mara kadhaa imekuwa ikiwatatanisha, si wapinzani pekee, lakini hata upande wa CCM. Anatajwa kuwa mtu mwenye hasira na mtoa uamuzi kwa jazba.

Mhagama na Zungu wanaweza kufikiriwa kutokana na mara zote kuonekana wakikimudu vema kiti cha Spika.

Katika vikao vya Bunge vilivyoongozwa na Zungu, alisifiwa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kutokuwa na upendeleo. Kusifiwa na wapinzani kunaweza kuwa chanzo cha yeye kunyimwa nafasi hiyo na wabunge wenzake wa CCM au vikao vya uteuzi vya chama hicho.

Pamoja nao, wanatarajiwa kujitokeza wanachama wengine wa CCM na vyama vingine, wasio wabunge, lakini wenye sifa za kuwa wabunge; kuwania kuteueliwa kuwania nafasi hiyo.

 

Kinyang’anyiro cha uwaziri 

Wanaotajwa kwenye uwaziri na naibu waziri ni pamoja na Dk. Charles Tizeba      (Buchosa), Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini), Ridhiwani Kikwete (Chalinze), Anthony Mavunde (Dodoma), Janeth Mbene  (Ileje), Luhaga Mpina (Kisesa), Cosato Chumi (Mafinga Mjini) na Dk. Norman Sigala (Makete).

Wengine ni Charles Kitwanga (Misungwi), Ezekiel Maige (Msalala), Nape Nnauye (Mtama), Rajab Adadi (Muheza), Charles Mwijage       (Muleba Kaskazini), Dk. Diodorus Kamala (Nkenge) na Hussein Bashe (Nzega Mjini).

Pia wamo William Ngeleja (Sengerema), Steven Masele (Shinyanga Mjini), Leonidas Gama (Songea Mjini), Juma Nkamia (Chemba), na George Simbachawene (Kibakwe).