Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Dar es Salaam, wamekuwa na kibarua kigumu baada ya kuendelea kulinda nyumba ya diwani mteule wa CCM Kata ya Sandali, Abel Tarimo.

Tarimo anaelezwa kuwa hapendwi na wananchi, kitendo kinachowafanya watake kuvamia nyumba yake na kuichoma moto licha ya msimamizi msaidizi wa kata hiyo, kumtangaza kushinda.

Ulinzi wa jeshi hilo uliodumu kwa saa 72 (siku tatu) umefanyika siku chache baada ya wananchi kuchoma Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Sandali baada ya kusuasua kumtangaza mshindi wa nafasi hiyo.

Hata hivyo, kazi hiyo ilihitimishwa Ijumaa asubuhi kwa amri ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Temeke, ambaye aliwataka askari hao kuendelea na doria za kawaida mitaani pamoja na kupitiapitia kwenye nyumba ya Tarimo na si kuilinda kwa saa 24 kama walivyokuwa wakifanya awali.  

Kuchomwa ofisi ya kata

Ofisi za Afisa Mtendaji Kata ya Sandali zilichomwa moto Jumanne iliyopita, baada ya upigaji kura kuhitimishwa ya saa 1.00 asubuhi ingawa kulikuwa na askari polisi.

Chanzo cha habari kimeidokeza JAMHURI kwamba ofisi hiyo imechomwa moto na vijana waliokuwa kwenye usafiri wa pikipiki ambao walifika eneo hilo bila kugundulika.

Kwa mujibu wa habari hizo, vijana hao walitumia mafuta ya petroli kuchoma ofisi hiyo baada ya kuiloweka shuka na walipofika eneo hilo waliiwasha na kuitupia kisha kutokomea kusikojulikana.

“Ilikuwa ni muda mfupi baada ya askari polisi waliokuwa katika kituo hicho kujisahau kidogo kwa kudhani kwamba eneo hilo liko salama kwani kitendo cha askari waliokuwa waliimarisha usalama kuzunguka nyuma ya ofisi hiyo tu kiliwapa mwanya vijana hao kurusha shuka lililokuwa na petroli kisha kuliwasha moto.

“Na wakati ofisi hizo zinachomwa, gari la polisi la washawasha lilikuwa limeegeshwa kituoni hapo,” kimesema chanzo hicho.

Muda mfupi baada ya ofisi hiyo kuchomwa moto, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisikika kwenye ‘radio call’ akiita askari polisi wakadhibiti hali hiyo.

“Nakumbuka ilikuwa asubuhi wakati huo tupo kwenye majukumu ya kupeana kazi, ndipo viongozi walipotutaka twende tukaongeze nguvu katika ofisi za kata ya Sandali.

“Baada ya kufika eneo hilo kuongeza nguvu, tulipata taarifa kwa wasiri kwamba vijana hao wamehamishia nguvu zao nyumbani kwa diwani mteule ndipo tulipojipanga kuweka ulinzi nyumbani kwake,” kimeeleza chanzo hicho.

Habari zinapasha kwamba tangu siku hiyo askari wamekuwa wakilinda nyumba ya diwani huyo mteule usiku na mchana, kwa kupokezana na kuna wakati nyumba ya diwani huyo imekuwa ikirushiwa mawe na watu ambao hawaonekani kutokana na kufanya uhalifu huo na kujificha.

Wananchi wang’aka

Kutokana na hatua ya askari polisi kulinda nyumba ya Tarimo, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Temeke wamesema hatua ya upigaji kura na utangazwaji wa matokeo yaliyompitisha Tarimo kutetea nafasi yake si ya busara.

Joel Mpesya ameiambia JAMHURI kwamba ingekuwa busara kwa diwani huyo mteule ambaye hakubaliki na wananchi wa kata yake kukubali yaishe kwa kuiacha nafasi hiyo kwenda kwa mpinzani wake, kuliko kile alichokifanya.

“Binafsi namshangaa diwani huyo mteule kwani anasababisha polisi wasifanye shughuli nyingine zaidi ya kumlinda yeye nyumbani kwa saa 24 ilhali askari wana shughuli nyingi za kufanya na wapo wachache,” anasema Mpesya.

Mwananchi mwingine wa Kata ya Sandali, Hawa Omary, amesema ingekuwa vyema kwa Tarimo ambaye ameongoza kwenye kata hiyo kwa zaidi ya miaka 10 kisha mwaka huu kukatawali na wananchi kuachia ngazi.

“Najiuliza moyoni mwangu; hivi mheshimiwa Tarimo anajisikiaje anapoona vurugu zinatokea kwa sababu yake? Anajisikia raha gani, anajisikia fahari gani anapoona uvunjifu wa amani unatokea kwa ajili yake?” Anahoji Hawa.

Naye Baraka Sylvester ameshangaa hatua ya diwani huyo mteule kung’ang’ania madaraka wakati wananchi hawamuhitaji.

Tukio kama hilo limetokea Manispaa ya Moshi baada ya kundi la wananchi kuvamia ofisi ya Serikali ya Kata ya Njoro, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi mgombea udiwani wa Chadema, Jomba Koyi.

Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika magari matano, walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao na pia kufanikiwa kuwakamata wananchi 106 wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo, katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wananchi hao walionekana wakishangilia kwa kupeperusha bendera za CCM na vitambaa vyenye rangi ya njano na kijani wakati wakipelekwa polisi.

Katika uchaguzi huo, Koyi aliibuka mshindi kwa kupata kura 3,181 akifuatiwa na mgombea wa CCM, Zuberi Kidumo, aliyepata kura 2,467 na Hamad Nkya wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 106.

Polisi wa FFU na askari kanzu walionekana wakipita barabara mbalimbali za mji wa Moshi kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi wakiwa na watuhumiwa hao huku magari yao yakishinikizwa kwa ving’ora.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, alisema tukio hilo limetokea baada ya wananchi hao kuandamana na kwenda kuchoma ofisi hiyo wakipinga ushindi wa mgombea wa Chadema.

Kamanda Ngonyani amesema polisi walilazimika kutumia nguvu ikiwamo kupiga mabomu ya machozi, baada ya wananchi hao kuanza kuwarushia mawe polisi waliokwenda eneo hilo kudhibiti vurugu.

Koyi alipoulizwa hivi karibuni aliwalaumu polisi kwa kile alichodai kulea uovu wa baadhi ya wafuasi wa CCM, ambao walianza kujichukulia sheria mkono hata kabla ya yeye kutangazwa mshindi wa udiwani.

“Hayo ni matokeo ya polisi wenyewe kuwalea. Walivunja ofisi wakaiba sanduku la kura za urais hawakuchukuliwa hatua. Wakapiga wasimamizi polisi wakakaa kimya na sasa wamechoma ofisi,” ameeleza.

Koyi alidai taarifa za uovu wa wafuasi hao ziko polisi, lakini hawakuchukuliwa hatua, akisema zipo njia za kisheria za kupinga matokeo ya uchaguzi kama hukuridhika badala ya kuchukua sheria mkononi.

By Jamhuri