Jina la Regina Lowassa – Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa limo kwenye orodha ndefu ya makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) watakaoteuliwa kuwa wabunge wa Viti Maalumu kwa mujibu wa Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Regina ambaye awali hakuwa na rekodi ya siasa za majukwaani na kujitokeza hadharani alipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), safari hii alivunja mwiko kwa kumpigia debe mume wake, Lowassa aliyekuwa akiwania urais kupitia Chadema.

Lowassa alikuwa anawania urais kwa tiketi ya Chadema, lakini akiungwa mkono na vyama vinavyopigania katiba yenye mtazamo na maoni ya Wananchi. Umoja huo unaofahamika kwa jina la Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

Vyanzo vya habari kutoka Chadema vimedokeza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chadema kilichofanyika katika Hotel ya Bahari Beach Jijini Dar es Salaam kiliamua kwa pamoja kwa kupitisha jina la Regina Lowassa kutunukiwa nafasi ya ubunge wa viti maalum.

Imeelezwa kuwa uamuzi huo uliyofanywa na Halmashauri Kuu uliungwa mkono na wajumbe wote wa kikao hicho ambao walivutiwa na mchango mkubwa alioutoa Regina katika kipindi cha kampeni nchini.

Baada ya kufanyika kwa maamuzi hayo, wajumbe hao waliwasiliana na Regina ambaye anaelezwa kushtushwa na taarifa hizo ambazo hakuwa na mamlaka ya kuyapinga kutokana na msimamo wa wajumbe wa kikao hicho.

Hata hivyo vyanzo vyetu vimebainisha kuwa Regina mpaka sasa hajatoa msimamo wake kutokana na msisitizo alioupata kutokana na uamuzi huo wa kikao hivyo ameendelea kuwa kimya.

Katika kipindi cha miezi miwili ya kampeni za uchaguzi, Regina ameonekana katika majukwaa nchini ambapo amezunguka nchi nzima kumuombea kura mume wake Lowassa ambaye katika matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi alishika nafasi ya pili, nyuma ya Dk. John Magufuli wa CCM.

Wakati JAMHURI likiwa limethibitishia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge wa Chadema, John Mrema, alishindwa kulizungumzia suala hilo kwa undani akidai, “Wakati wake haujafika. Muda wa kutangaza majina ya Viti Maalumu ukifika, basi kila mmoja atajua.”.

By Jamhuri