ffRais Mteule wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, akiwa anasubiri kuapishwa keshokutwa, tayari ameshaanza kazi zenye mwelekeo wa kuandaa aina ya Serikali atakayoiunda.

Habari za uhakika kutoka kwa watu walio karibu na Dk. Magufuli, zinasema amekuwa akitumia muda mrefu kupanga safu ya wasaidizi wake akiamini hana muda wa kupoteza.

Wiki ijayo, amepanga kulizindua Bunge mjini Dodoma na wakati huo huo kulihutubia Taifa kwa hotuba inayotajwa kuwa ya kipekee na yenye kutoa matumaini mapya ya kuijenga Tanzania mpya.

Kwenye upangaji huo wa safu ya uongozi, amekusudia kuanza kutangaza mawaziri wa wizara chache, na kuna habari kwamba kuna wizara moja nyeti ambayo anaweza kuiongoza yeye mwenyewe.

Ingawa haijawekwa wazi, watoa habari wetu wanasema Wizara ya Fedha ni miongoni mwa wizara ambazo huenda zikawa chini ya uangalizi wake wa moja kwa moja.

Sababu kubwa inayotajwa ni kwamba anafanya hivyo ili kuhakikisha Serikali inaingiza mapato makubwa zaidi yatakayomwezesha kutekeleza ahadi lukuki alizotoa kwa Watanzania wakati wa kampeni.

Wizara ya Fedha anakusudia kuiweka chini ya uangalizi wake ili kuziba mianya ya rushwa, urasimu wa utoaji fedha za maendeleo na kukomesha misamaha ya kodi.

Januari mwaka huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilisema misamaha ya kodi imeongezeka kutoka Sh trilioni 1.4 mwaka 2012/2013 hadi Sh trilioni 1.8 mwaka 2013/2014.

Sababu mojawapo ya Tanzania kuwa na utegemezi mkubwa wa misaada ya wahisani na kushindwa kuwekeza kwa haraka katika maendeleo yake ni ukusanyaji mdogo wa mapato yatokanayo na kodi.

Misamaha ya kodi Tanzania ni mikubwa ikilinganishwa na Kenya na Uganda; na kwa kiasi kikubwa inawanufaisha zaidi wawekezaji wakubwa wenye vyeti kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Dk. Magufuli, amekusudia kuona utekelezaji wa mara moja wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika Julai, mwaka huu. Sheria hiyo inafuta misamaha ya kodi kwa maeneo mengi na kuhimiza matumizi ya mashine za EFD.

“Rais Mteule anaamini bila kuongeza makusanyo Serikali haiwezi kutekeleza ahadi zake kwa ufanisi. Fedha zinazopotea ni nyingi sana na kwa maana hiyo anataka asimamie kwa karibu sana masuala ya fedha,” amesema mmoja wa watumishi wanaomshauri Dk. Magufuli, masuala ya fedha.

Hatua nyingine za awali zilizopangwa kuchukuliwa na Dk. Magufuli ni kuanza kuwashughulikia kisheria wakwepa kodi waliokubuhu.

Kwenye orodha hiyo, chanzo chetu kimesema: “Kuna majina ya watu hamtaamini kama kweli kungetokea siku wakakamatwa na kushitakiwa kwa ukwepaji kodi. Tayari amepewa orodha yao na hao imepangwa aanze nao kama mfano ili wengine wasithubutu kukwepa kodi.”

Kwenye orodha hiyo wametajwa pia wafanyabiashara ambao kwa siku za karibuni wamekuwa, ama wakifuta, au wakibadili majina ya kampuni zao zinazotuhumiwa kukwepa kodi.

“Mtu muuaji hawezi kuachwa kushitakiwa eti kwa sababu amebadili jina. Unapoua unabaki yule yule hata kama umebadili jina. Mheshimiwa anaamini wote wanaofanya ujanja huo watakamatwa na kutakiwa walipe kodi ya Serikali. Hana ugomvi na mfanyabiashara, ugomvi wake ni kwa wakwepa kodi, basi. Tena anasisitiza asiwepo mtu wa kukimbia kwa sababu anaamini kama mtu hakwepi kodi ni kitu gani cha kumfanya akimbie nchi?” Amesema mtoa taarifa wetu.

Kwenye orodha hiyo, pia kuna kampuni za mafuta ambazo zimekuwa zikiihadaa Serikali kuwa zinasafirisha mafuta nje ya nchi, lakini mafuta hayo yamekuwa yakiuzwa hapa hapa nchini na hivyo kuikosesha Serikali mabilioni ya shilingi.

Sambamba na hilo, Dk. Magufuli, amekusudia kuwashughulikia mara moja watumishi wote wa Serikali wanaoshirikiana na wafanyabiashara kuhujumu mapato ya nchi.

Hao ni pamoja na wale waliohujumu mita zinazorekodi kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini kutoka kwenye meli. Mita hizo ambazo zipo katika Bandari ya Dar es Salaam, zimenunuliwa kwa fedha nyingi lakini zimehujumiwa na sasa hazifanyi kazi.

Kwa hujuma hiyo, mafuta yanayoingizwa nchini hayajulikani, na hivyo kutoa mwanya kwa waagizaji kuihaa na kuikosesha Serikali mapato.

Dozi nyingine inayoanza muda mfupi baada ya Dk. Magufuli kuapishwa ni kupunguzwa, na hatimaye kufutwa kwa safari nyingi za nje ya nchi kwa watumishi wa umma.

“Miongoni mwa mianya ya upotefu wa fedha za umma ni kwenye safari za vigogo na watumishi wengine nje ya nchi. Hilo Rais Mteule amesema halisubiri mwezi, ni la kuanza nalo mara moja ili watu wabaki nchini wafanye kazi za kuwatumikia Watanzania.

“Safari pekee za nje ni zile zenye tija kwa Taifa, na unawekwa utaratibu maalum wa kujua nani atasafiri kwenda wapi, kufanya nini na kwa minajili ipi. Idadi ya wasafiri kwenye misafara nje ya nchi nayo inatakiwa ijulikane. Wametoa mfano wa Rais wa Botswana ambaye safari yake ya nje huwa haizidi watu 12; lakini kwa Tanzania hufikia watu 100. Hayo ni matumizi mabaya ya fedha za umma, na sasa yatapunguzwa na hata kukomeshwa,” kimesema chanzo chetu.

Jambo jingine ambalo Rais Mteule anatajwa kuanza nalo kwa kasi ni la kupambana na wahamiaji haramu hasa katika miji mikubwa na maeneo mengine ya mipakani.

Kati ya maeneo yanayotajwa ni Ngorongoro ambako duru za kiintelejensia zinaonyesha kuwa raia kadhaa wa kigeni wameingiza mifugo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) na hivyo kuhatarisha uhai wake. Serikali ni moja ya Hifadhi za Taifa zinazoingiza fedha nyingi za kigeni na pia kuhudumia hifadhi nyingine zisizotembelewa na watalii wengi.

“Dk. Magufuli, anapenda sana wageni, lakini wanaoishi nchini kisheria kwa sababu anasema Tanzania imekuwa shamba la bibi. Wahamiaji haramu ni wengi na hivyo wanachangia hata kuifanya Serikali iwe na wakati mgumu kuwahudumia raia wake kwa sababu humo humo imejikuta inahudumia wageni.

“Anaamini kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki, lakini anataka watu waishi nchini kwa kufuata sheria. Anakasirishwa na migogoro ya mara kwa mara ambayo vyombo vya usalama vimebaini kuwa inasababishwa na raia wa kigeni na wahamiaji haramu. Hili amelipa umuhimu wa kipekee,” amesema.

Kwa wale waliovamia hifadhi za barabara na wanaozidisha mizigo kwenye malori, Dk. Magufuli, tayari anatajwa kuandaa dawa yao.

Mtoa taarifa wetu anasema tayari Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ametakiwa awape taarifa wavamizi wote wa maeneo ya hifadhi ya barabara ili miradi inayojengwa au inayotarajiwa kujengwa isikwame.

“Kuna fedha nyingi zinapotea kwa kuwalipa makandarasi kutokana na uzembe wa Serikali kuchelewa kuwaondoa watu waliojenga ndani ya hifadhi za barabara. TANROADS sasa wanatakiwa wawape taarifa wavamizi waondoke ili maendeleo yaanze mara moja,” kimesema chanzo chetu.

Jambo jingine ambalo tayari ameshawasiliana na viongozi wenye dhamana nalo ni la Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Imeelezwa kuwa ahadi hiyo ambayo alianza nayo siku ya ufunguzi wa kampeni Jangwani, Dar es Salaam, tayari amekuwa akiifuatilia kwa karibu hata kabla ya kuapishwa keshokutwa.

Ni kwa msukumo huo, habari za uhakika zinasema tayari majina ya wanafunzi wanaostahili kupata mikopo yameanza kutangazwa. Vyuo vingi vinafunguliwa wiki hii.

Dk. Magufuli, amenuia kuunda Baraza la Mawaziri lenye idadi ndogo ya mawaziri, tena wasiokuwa na “majina makubwa”.

By Jamhuri