seifKatibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amekuwa mwiba mchungu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar hasa baada ya kutangaza kuwa anasubiri kuitwa na Tume ya Uchaguzi visiwani  humo (ZEC) kumtangaza.

JAMHURI lilipowasiliana na Maalim Seif ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa SMZ, akasema kwa ufupi: “Sijui wanasubiri nini kunitangaza?”

Seif ambaye juzi alizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu ngazi za Wilaya na Majimbo katika Ukumbi wa Majid Kiembesamaki Zanzibar kisha kuzungumza na JAMHURI, anasema: “Leo nilikuwa nazungumza na wajumbe wa CUF, nimewaambia kabisa kwamba hawana sababu ya kukimbia.”

Badala yake, kiongozi huyo wa CUF, anawataka wafuasi na wapenzi wa chama hicho kutembea kifua mbele kutokana na ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.

Maalim Seif anasema ushindi wa CUF visiwani humo umeleta matumaini mapya kwa Wazanzibari ambao wameitumia vyema haki yao ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Ninachoweza kusema kwamba hapa Zanzibar kuna hila. Kuna njama za kupindua uamuzi wa wananchi kwa nguvu. Wananachi walikwisha kuamua kupitia masanduku ya kura, nasema safari hii haiwezekani,” anasema.

Anairushia tuhuma hizo ZEC, akidai kwamba inachelewesha kukamilisha uhakiki wa kura kwa majimbo 14 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa Urais.

“Ningependa kuishauri ZEC kukamilisha zoezi hilo ili serikali mpya ianze kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi. Kama nilivyowaambia wajumbe wale wa CUF kwamba mimi sina wasi wasi.

“Ninajihesabu kama Rais ninayesubiri kuitwa na kuapishwa, na sasa nimo katika matayarisho ya kuunda serikali ili nikiapishwa tu nisipoteze tena muda wa kufikiria kuunda serikali.”

Anasema suala la yeye kuwa Rais halifahamiki Zanzibar pekee, bali dunia nzima wanamfahamu yeye ndiye aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu uliopita.

Anasisitiza kuwa hakuna sababu za kurudia uchaguzi huo kwani ulifanyika kwa amani na hakukuwa na dosari ya kuusitisha kwani washindi wa uwakilishi na udiwani walikwisha kutangazwa.

Maalim Seif anasema hakuna ukweli juu ya madai kwamba kuna ongezeko la kura katika kisiwa cha Pemba. “Kule Pemba hakuna kituturi hata kimoja kilichozidishwa wapiga kura 350 kiliopangiwa na kwamba vituturi vingi vilikuwa na wapikura chini ya idadi hiyo.”

CUF imeishauri ZEC kutengua uamuzi wa Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, kwa vile hana mamlaka ya kikatiba na sheria ya uchaguzi haimruhusu kufuta uchaguzi huo.

Mmoja wa makada mahiri wa CCM Zanzibar anasema Seif anazidi kuwachanganya kwani ameng’ang’ania kutaka kutangazwa mshindi ilihali uchaguzi umefutwa na utafanyika Januari, mwakani.

Kada huyo anasema kuna idadi kubwa ya wakazi wa visiwani humo walioamua kukimbilia Tanganyika (Tanzania Bara) wakihofu machafuko ya kisiasa.

“Wazanzibar hawajui hatma ya malumbano ya kisiasa Zanzibar. Tume imetangaza kufuta yale matokeo na bila shaka kuna taratibu zinafanyika, lakini Seif anang’ang’ania tu, sijui,” anasema kada huyo.

Mwana-CCM huyo kutoka Pemba, anasema hali ya Zanzibar kwa sasa imetulia, lakini bado kuna mambo yanawaumiza Wazanzibari kichwa kujua hasa nani ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

2647 Total Views 4 Views Today
||||| 5 I Like It! |||||
Sambaza!