A

Samuel Sitta
Samuel Sitta
liyekuwa Spika wa Bunge la 9 Samuel Sitta wiki iliyopita alipoonyesha nia ya kugombea uspika wa bunge, sasa ameanza kushughulikiwa, JAMHURI limebaini.

Duru za uhakika zinasema Sitta anaunda upya mtandao wake ndani ya CCM baada ya mtandao wa awali kusambaratika katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mtandao uliokuwa wa Edward Lowassa, Bernard Membe, Rostam Aziz na Jakaya Kikwete, umechanwa rasmi katika uchaguzi uliopita hadi Lowassa akahamia CHADEMA, huku Membe akibwagwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama.

Kutokana na hali hiyo, vyanzo vya uhakika vinasema Sitta anataka kuwa Spika wa Bunge atumie fursa hiyo kujijengea umaarufu na ikibidi kumtisha Rais John Magufuli kuwa iwapo hatatenda atakavyo basi atamuundia Kamati Teule ya Bunge na kuisambaratisha serikali yake ndani ya miaka miwili kama ilivyokuwa mwaka 2008.

“Mzee Sitta bado ana matumaini kuwa ipo siku atakuwa Rais wa Tanzania. Na amefika mahala anaona kama si yeye, basi aandae mtu wake. Uspika anautaka kwa nia ya kujijenga na si kutumikia taifa, ndiyo maana wanaolijua wameanza kumshughulikia. Wanasema huyu sasa ni Agano la Kale. Wanataka kuona Agano Jipya,” alisema mtoa habari wetu.

Awali, Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, alitajwa kuwa na nafasi kubwa ya  kumshinda Samwel Sitta ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alitangaza kuona dalili za ‘mizengwe’ ya jina lake kukatwa.

Bunge la 11 likitarajiwa kuanza vikao vyake Novemba 17, mwaka huu mjini Dodoma ambako pamoja na shughuli nyingine litamchagua Spika wa Bunge.

Spika na Naibu Spika wakipatikana, Bunge litakabidhiwa jina la Waziri Mkuu na kulithibitisha au kulikataa kisha Dk. Magufuli ataanza kazi ya kuunda Baraza la Mawaziri kwa kushirikiana na Waziri Mkuu atakayekuwa amemteua kwa mujibu wa sheria. Waziri Mkuu atatangazwa Novemba 19, mwaka huu.

Kwa kuwa Dk. Magufuli aliapishwa Novemba 5, kwa vyovyote vile Ibara ya 51(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inamtaka ndani ya siku 14 awe amemteua Waziri Mkuu na ukomo huu unagota Novemba 19.

Sitta amedaiwa kutaka nafasi hiyo tena kwa udi na uvumba kwani imefikia hatua ya kutaka kwenda mahakamani iwapo itatokea akafanyiwa ‘mizengwe’ kama ilivyotokea mwaka 2010.

Mwaka 2010 alipohitaji nafasi hiyo, mamlaka ya juu CCM ilitangaza kuwa sifa ya mtu kuombea uspika alipaswa kuwa jinsi ya kike. Tangazo hili lilimpa fursa Anne Makinda, na Sitta akanung’unika kuwa sharti hilo lilikuwa gumu kwake kulitekeleza.

Alisema hasingewezi kubadili jinsia kuwa na sifa za kuwania nafasi hiyo, lakini safari hii tayari ametangaza: “Sitakubali mizengwe.”

Tanzania ina mihimili mitatu; Serikali inayongozwa na Rais Dk. John Magufuli, Mahakama – Jaji Othaman Chande na Bunge ambalo mhusika anatafutwa.

Sitta, Zungu na makada wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatarajiwa kuanza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uspika wiki hii.

“Tunatarajia bunge hili kuwa na changamoto zaidi kuliko yaliyotangulia. Hivyo basi kutokana na kile tunachokitarajia huko, ni lazima apatikane mtu atakayekuwa tayari kusimama na kusimamia chombo hicho bila kuyumbishwa,” anasema.

Wengine wanaotajwa kuitaka nafasi hiyo ni Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, Mwenyekiti wa UVCCM Mstaafu, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Kongwa Job Ndugai. Ndugai alikuwa Naibu Spika wa Bunge lililomaliza na anatajwa kuchapa bakora wanaompinga.

Kiti cha Spika kinaweza kuwaniwa na mtu yeyote ambaye atapitishwa na chama chake bila kujali kama ni mbunge au la.

CCM  kimekuwa na kawaida ya kutoa fursa kwa wanachama wake kuomba nafasi hiyo na baadaye vikao hufanyika kupitisha jina la mgombea mmoja.

Iwapo mgombea wa nafasi hiyo hatokuwa mbunge wa jimbo, ni lazima jina lake lipitishwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

2413 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!