*Asaka ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania nje ya nchi

*Ateta na mabalozi wa nchi mbalimbali, waonesha nia

Hakika juhudi zake hizi zinadhihirisha jinsi alivyo mzalendo mwenye dhamira ya kuona uchumi wa nchi unakua kama si kustawi,  na maisha bora yanawezekana kwa kila Mtanzania.

Mtanzania huyu si mwingine yeyote bali ni Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP zinazoendesha vituo vya ITV na Radio One Stereo, magazeti ya Nipashe, The Guardian, Kulikoni na This Day.

Katika kudhihirisha jinsi anavyotamani kuona maendeleo ya Watanzania, Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), amefanya juhudi za kusaka ushauri wa ufumbuzi wa matatizo ya nchi kutoka kwa mabalozi wa nchi mbalimbali.

Ameweza kukutana na kufanya nao mazungumzo maalumu kwa nyakati tofauti ofisini kwake, makao makuu ya IPP jijini Dar es Salaam.

Huku akiwa mwongozaji wa mazungumzo hayo, Mengi amekuwa akijikita zaidi katika hoja za kuboresha uchumi, elimu, afya (miongoni mwa huduma nyingine za kijamii), amani, kuongeza ajira kwa vijana, matumizi sahihi ya rasilimali za nchi na udhibiti wa rushwa na bidhaa bandia nchini.

Balozi wa Finland

Miongoni mwa aliokutana na kuteta nao ni Balozi wa Finland nchini, Sinikka Antila. Mengi ametumia fursa hiyo kumuuliza Balozi Antila kwamba anadhani Tanzania itakuwa na nafasi gani kimaendeleo baada ya miaka 10 ijayo, na inawezaje kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka mataifa mengine. Balozi huyo wa Finland amesema Tanzania inaweza kujitegemea na kuondokana na utegemezi huo, kama itatumia vizuri rasilimali zake.


“Rasilimali ndiyo nguzo ya maendeleo ya nchi. Tanzania ikitumia vizuri rasilimali zake kwa kuweka kipaumbele katika sekta muhimu kama vile afya na elimu, itapiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi cha miaka kumi ijayo,” amesema.


Kwamba viongozi wanapaswa kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma, zinazotokana na rasilimali zilizopo kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa mfano mzuri wa kuigwa barani Afrika.

 

Balozi Antila ametoa wito kwa Watanzania kutoendelea kujikita katika kuzungumzia gesi asilia pekee, kwani kuna rasilimali nyingine nyingi kama vile madini na misitu ambazo zina nafasi kubwa ya kuchangia kukuza uchumi wao.

 

Ametoa mfano kwamba Finland inashirikiana na sekta binafsi kukuza uchumi wake, kutokana na pato kubwa linalotokana rasilimali za misitu.

 

“Ukosefu wa ajira kwa wananchi wengi ni miongoni mwa mataizo yanayoikabili Tanzania, lakini sekta za misitu, kilimo na biashara ndogondogo zitasaidia kupunguza tatizo hilo,” ameongeza. Anashauri Serikali kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na rasilimali zilizopo, na kuweka wazi mapato yanayotokana na rasilimali hizo ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima kati yake na wananchi.

 

Akijibu swali jingine la Mengi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Balozi huyo amesema Tanzania inajitahidi kufanya vizuri katika ukanda wa Afrika, kwani imeruhusu kuanzishwa kwa vituo vingi vya redio, televisheni na magazeti. Hata hivyo, Mengi amesema bado kuna hitaji la kurekebisha sheria kandamizi zinazominya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Balozi wa Korea Kusini

Katika mazungumzo na Balozi wa Korea Kusini, Chung IL, Mwenyekiti Mtendaji huyo wa IPP ameomba ushauri wa balozi huyo juu ya nini kifanyike ili kufikia mafanikio ya maendeleo ya kweli Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli usiopingika kwamba Watanzania wengi wanakabiliwa na umaskini kiasi cha baadhi yao, kuishia kupata mlo mmoja usiokamilika kwa siku badala ya mitatu iliyokamilika kama inavyohimizwa na wataalamu wa lishe na afya.


Hata hivyo, ushauri wa Balozi IL kwa Mengi unatia matumaini kwamba Tanzania bado ina fursa ya kuwezesha wananchi wake kupiga hatua kubwa ya maendeleo, ikiwa itaweka kipaumbele cha juu katika elimu na amani.

 

“Elimu na amani vina nafasi kubwa ya kuwezesha maendeleo, vitu hivi vinapaswa kuwa funguo za mafanikio Tanzania,” amesema IL.

 

Balozi huyo amedokeza kuwa Korea Kusini imezidi kupaa kimaendeleo, kutokana na serikali yake kuelekeza uwekezaji mkubwa katika kunoa akili za watu wake (kwenye elimu).

 

Katika hatua nyingine, Balozi IL ameeleza kuridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania, katika kutafuta maendeleo ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujenga mazingira ya kuvutia wawekezaji wa kigeni.

 

Amesema Korea Kusini inaona faraja kuendelea kushirikiana na Tanzania katika jitihada za kuwajengea Watanzania uwezo wa kumudu changamoto za kiuchumi.

 

Kuhusu wafanyabiashara wa Tanzania, Balozi IL amesema Korea Kusini iko tayari kufungua milango ya ushirikiano katika kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali.

 

Amesema mipango ya uwekezaji na kuelekeza nguvu kubwa katika kugharamia masomo kwa watoto, imechangia kwa kiasi kikubwa kuipaisha nchi hiyo kimaendeleo.

 

“Nchi yangu [Korea Kusini] inapiga hatua ya maendeleo kutokana na sera nzuri katika kusimamia sekta ya elimu, na ambayo inaheshimiwa na viongozi wote wanaoingia madarakani,” amesema. Mengi anatamani kuona Tanzania nayo inakuwa na sera nzuri ya elimu, inayoeleweka na kuheshimiwa na kila kiongozi anayeingia madarakani, badala ya kuruhusu kila waziri anayeingia kuibadili atakavyo.

 

Kuhusu mafanikio ya mapambano dhidi ya rushwa huko Korea Kusini, Balozi IL amesema yametokana na wananchi wa nchi hiyo kutambua wajibu wa kushiriki katika vita hiyo, lakini pia mahakama zimekuwa zikishughulikia ipasavyo kesi za rushwa. Kwa upande wake, Mengi ameiomba Korea Kusini kupitia kwa Balozi huyo, ifikirie kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini Tanzania waweze kuboresha shughuli zao na kufuta umaskini unaowakabili.


Ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza Serikali ya Korea Kusini kwa kufanikiwa kukabili vitendo vya rushwa, lakini akasema kama ilivyoshauriwa na Balozi IL kwamba hata Tanzania inaweza kufanikiwa katika hilo iwapo watu wake watashiriki kikamilifu kupambana na tatizo hilo.

Balozi wa India

Mengi pia amekutana na Balozi wa India hapa Tanzania, Debnath Shaw, na kutumia fursa hiyo kumwomba ushauri kuhusu ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili sekta za afya, elimu, umeme, viwanda, biashara na uwekezaji nchini.

 

Pamoja na mambo mengine, kikubwa ambacho Balozi Shaw ameahidi ni ujenzi wa mtambo wa umeme wenye uwezo wa kuzalisha megawatt 250, utakaotekelezwa na kampuni inayojulikana kama Kumar Group, katika Kanda Maalumu ya Kiuchumi Bagamoyo.

 

Amesema India inatekeleza jukumu la kushirikiana na Tanzania kuimarisha uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara Wahindi kutambua umuhimu wa kuwekeza hapa nchini.


Balozi Shaw amedokeza pia kwamba kampuni nyingine ya India imeonesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya umeme, endapo itahakikishiwa upatikanaji wa gesi ya kutosha kuzalisha nishati hiyo chini ya gridi ya Taifa, kupunguza tatizo la huduma hiyo nchini.

 

“Tuna dhamira ya kuisaidia Tanzania kuendeleza teknolojia inayohitajika kulingana na mazingira yaliyopo,” amesema. Akizungumzia sekta ya afya, Balozi Shaw amesema India itaendelea kuisaidia Tanzania kuimarisha huduma mbalimbali zikiwamo za upasuaji.


“Tumesikia pia kwamba kuna ARV (dawa za kupunguza makali ya ukimwi) bandia hapa Tanzania, tuliomba Serikali tukakagua hizo dawa na kubaini kuwa hazikutoka India. Katika hili India itasaidia kulinda watumiaji wa ARV huku Tanzania,” amesema Shaw.


Akijibu hoja ya Mengi kuhusu kuisaidia Tanzania kuwezesha usindikaji wa korosho zinazozalishwa nchini, Balozi Shaw ameipa Serikali changamoto ya kuweka sera nzuri itakayosimamia ujenzi na uendeshaji wa viwanda vya kusindika zao hilo na mengineyo.

 

Kwa mujibu wa Mengi, usindikaji wa korosho utaongeza thamani ya zao hilo, hivyo kuwezesha wakulima na Watanzania kwa jumla kunufaika na mauzo yake ndani na nje ya nchi.


Mengi ameiomba India kupitia kwa Balozi huyo, kuangalia uwezekano wa kuwainua Watanzania katika nyanja za biashara na elimu, hoja ambazo huenda zikashughulikiwa baada ya Balozi Shaw kuziwasilisha katika Serikali ya India.


 

By Jamhuri