Jenista MhagamaTaasisi za Serikali zimeanza kugongana kutokana na Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano kupitisha sheria zinazokinzana.

Utata huo umetokea baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa tangazo lililotiwa saini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu linalohusisha utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini.

Katika tangazo hilo lililotiwa saini Desemba 14, mwaka huu, na Waziri Jenista Mhagama linawataka waajiri wote nchini kufuata Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika rasmi Septemba 15, 2015.

“Tunapenda kuwaarifu waajiri wote nchini kwamba Serikali imetunga sheria ya kuratibu ajira za wageni nchini Na. 1 ya mwaka 2015 ambayo imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba 2015. 

“Kwa mujibu wa sheria hii, kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” inasema sehemu ya tangazo hilo.

Katika taarifa hiyo inayoendelea kwa kusema “Kwa taarifa hii, tunapenda kuwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi kuwa wanatenda kosa.” Tangazo hilo pia limenukuliwa likisema: “Serikali inatoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.”

Kutokana na tangazo hilo la Serikali, JAMHURI imelazimika kufuatia kwa ukaribu kuhusiana na tangazo hilo ambalo limelalamikiwa na baadhi ya watu kutokana na kukinzana na sheria na taratibu za Idara ya Uhamiaji nchini.

Mmoja wa viongozi wa Idara ya Uhamiaji anaeleza kuwa upitishwaji wa sheria hiyo haukuangalia suala muhimu la ulinzi na usalama wa nchi, jambo ambalo si sahihi.

Anasema kuwa kibali cha CTA (Carry on Temporary Assignment) kimekuwa kikitolewa na Idara ya Uhamiaji nchini kutokana na sheria zake, hivyo kutolewa na kamishna wa kazi si jambo sahihi.

Anaeleza kuwa kawaida zipo taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali hivyo na hatimaye kupatiwa kibali cha ajira ambacho hutolewa na kamishna wa ajira.

“Tatizo lililopo hapa ni Wizaya ya Kazi kupitia Kamishna wa Kazi kuingilia kazi za Uhamiaji kwa maana ya wao kuwa na vibali sawa na vile vinavyotakiwa kutolewa na Idara ya Uhamiaji ambayo ndiyo inayohusika na wageni wote wanaoingia nchini. Haiwezekani iwe rahisi kiasi hicho kumpatia mgeni kibali huku hujui historia yake, ni lazima taratibu zifuatwe,” anasema.

Hata hivyo anaeleza kuwa kamishna wa kazi amekuwa akitoa vibali ambavyo ni sawa kabisa na vile vinavyotolewa na Uhamiaji mpaka madaraja yake.

“Wamehamisha mpaka madaraja yale yale yanayotolewa na Uhamiaji na kuyapeleka huko Kazi, haya ni mambo ya ajabu. Kama walitaka kufanya hili jambo, tulitakiwa kukaa wote wizara hizi mbili – Mambo ya Ndani na Kazi – ili tuwekane sawa, tuelewane nani anapaswa kufanya nini siyo kama hivi inavyofanyika. Mambo mengine ni siri, ya kiusalama wa nchi, huwezi kuyaacha hivi hivi bila kuyazingatia,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, JAMHURI ilifika Ofisi ya Kamishna wa Uhamiaji wa Vibali vya Ukaazi nchi na pasi, Vicky Lembeli, aliyesema, “Mimi si msemaji wa idara hiyo hivyo ni vyema kuwasiliana na kitengo cha habari.

“Hapa mimi kazi yangu si kuongea na watu, nina kazi za kufanya siwezi kukueleza chochote, nenda kwa watu wa habari wanaweza kukwambia chochote, na kama utataka kibali kajaze fomu halafu utajua taratibu zake ni zipi, samahani,” anasema Kamishna Lembeli. 

Pamoja na Lembeli kukana, ukweli ni kwamba yeye ndiye anayehusika na utoaji wa vibali kwa wageni nchini, lakini alikana kutoka maelezo. Hata hivyo, JAMHURI ilipofika ofisi kitengo cha habari ilielezwa kuwa wahusika wapo nje ya ofisi.

2848 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!