Wiki moja tangu kuchapwa kwa habari ya malalamiko ya Watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya ‘unga’ aina ya heroin kuhusu kucheleweshwa kwa shauri wakidai linachukua muda mrefu kusikilizwa, limefumua mambo mengine.

Taarifa zinasema kwamba shauri hilo lilitoka Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kwenda Mahakama Kuu Mei 17, mwaka huu lilianza kupata vikwazo vingi vya upepelezi kwani inaarifiwa kuwa awali Jaji Upendo Msuya anayesikiliza kesi hiyo alikataa kielelezo cha gari.

Gari ambalo watuhumiwa hao walikamatwa nalo Desemba 9, 2010 na ASP Lubbe – Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), wakiwa ndani ni Mitsubishi Pajero lenye namba za usajili za Kenya KAW 276 G.

Kesi hiyo iliahirishwa Desemba 7, 2015 na Jaji Msuya hadi mwakani kwa hoja ya kuitilia shaka hati ya upekuzi iliyofanywa na ASP Lubbe ambaye ni Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kabuku mkoani Tanga.

Hatua ya Jaji Msuya kukataa gari kuwa sehemu ya kielelezo katika kesi hiyo katika mwenendo wa makosa ya jinai, ilipingwa na Waendesha Mashtaka kabla ya kukubaliwa kwa mujibu wa mmoja wa maofisa kutoka ofisi ya Waendesha Mashtaka.

Waendesha mashtaka nao wameibuka wakihoji utaratibu wa kuwaita mashahidi katika mahakama ya wazi na kuita jina moja baada ya jingine na kulipa fedha za kujikimu.

“Shahidi ni mtu muhimu katika kesi yoyote ile. Hakuna kesi kama hakuna mashahidi. Anatakiwa au wanatakiwa kulindwa. Sasa kitendo cha kuwaita hadharani kwenye open court (mahakama ya wazi) na kuwalipa ni kosa.

“Mbaya zaidi watuhumiwa wanawaona mashahidi,” anasema ofisa huyo ambaye wakati wote alionesha kupinga utaratibu huo akisema kwamba namna fulani unaharibu utaratibu wa mahakama.

Awali taarifa ambazo gazeti hili ilizipata ni mtazamo wa watuhumiwa wakimlalamikia Jaji Msuya, wakihoji; “Sijui mheshimiwa Jaji ana malengo gani na kesi hii! Maana ameirusha tena hadi mwakani wakati ilibidi iendelee mwezi huu.”

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo waliokutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito kilo 50 ni; Ismail Shebe mwenye hati ya kusafiria Na. AB 293433 na Rashid Said Salum, mwenye hati ya kusafiria Na. AB 012971. Wote wakazi wa Dar es Salaam.

Mbali ya watuhumiwa hao, yumo pia raia wa Iran, Majed Armand, mwenye hati ya kusafiria  Na. 214488959 aliyezaliwa Chabahar, Agosti 25, 1973.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa hatua za awali mwaka 2013, lakini Jaji Msuya aliiahirisha Novemba 30, 2015 lakini akairusha tena hadi Desemba 7, mwaka huu.

Watu hao (Shebe na Salum) ambao ni watuhumiwa wa kwanza na pili katika kesi hiyo, walikutwa na dawa za kulevya kilo 50. Zilifahamika kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin baada ya kupimwa katika maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Baada ya mahojiano na Polisi ndipo watuhumiwa hao walipomtaja Armand, mkazi wa Mikocheni B, Dar es Salaam, aliyeunganishwa kwenye kesi hiyo. Kabla alifuatwa nyumbani kwake ambako alipekuliwa na kugundulika kuwa na dawa nyingine za kulevya gramu 953. 

Bila kutaka kufahamika nani hasa aliyekuwa kinara wa kulalamika, watuhumiwa hao wanaona kuwa hizo ni dalili za kuidhoofisha kesi hiyo dhidi ya watuhumiwa ambao wako ndani kwa sasa wakisubiri kesi hiyo iendelee tena hapo mwakani mara itakapopangiwa tena na Msajili wa Mahakama.

Mbali ya walalamikiwa katika kesi hiyo, pia mashahidi wanalalamikia usumbufu kwani wamekuwa wakiitwa mara kwa mara bila kesi hiyo kuendelea na malipo yao kucheleweshwa.

“Tunapata malipo yetu kwa shida. Tunaitwa hapa Tanga, halafu unaambiwa kesi inaahirishwa. Tumekuja katika kesi ya tarehe 30 Novemba  tukarudi makwetu, na tumekuja tena Desemba 7, ambako pia kesi imeahirishwa,” anasema mmoja wa mashahidi.

Hii si kesi ya kwanza ya ‘unga’ kuendeshwa na Jaji Msuya, kwani kumbukumbu zinaonesha kwamba alipata kutoa dhamana kwa watuhumiwa wanne wakiwamo raia wawili wa nje, waliokuja kutoroka baadaye.

Watuhumiwa hao walikamatwa na Februari 21, 2011 huko eneo la Mbezi Beach Jogoo, Dar es Salaam wakiwa na kilo 179 zilizokuja kuthibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin.

Waliokamatwa na mzigo huo ni Watanzania – Fred Chonde na Zuberi Mbwana – wakati wale raia wa nje ni Shabaz Malik Muhammad, raia wa Iran. Ana hati mbili za kusafiria. Hati hizo ni PQ 5144792 ya Iran na nyingine KE611868 ya kutoka Pakistan. Mwenzake ni Adbulghai Pirbaksh, raia wa Pakistan, ambaye hati yake ya kusafiria ni ZF410415. Wakati kesi hiyo ikiendelea, Jaji Msuya ndiye aliyewapa dhamana watuhumiwa hao Julai 5, 2011 kwa dhamana ya Sh milioni 10 katika dawa zenye thamani ya Sh bilioni tatu. 

Taarifa zinasema kwamba watuhumiwa hao walitoroka kwani hawakutokea Julai 23, 2011 wakati Jaji Msuya anafuta kesi hiyo akisema kwamba kulikuwa na kasoro upande wa mashtaka.

Mara baada ya upande wa Serikali kukata rufaa, kesi hiyo ilirudi tena mwaka huu na kusikilizwa kuanzia Agosti 4 hadi Agosti 8, ambako ilitolewa hukumu.

Mahakama ilimtia hatiani Fred Chonde na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh bilioni 15.6 huku ikimwachia huru Zuberi Mbwana aliyejitetea akisema kwamba alikwenda kwa Chonde kumsabahi hivyo hahusiki.

Pamoja na utetezi huo ulioacha watu midomo wazi  kwenye maelezo ya awali ya mashtaka ilielezwa mahakamani kwamba watuhumiwa walikutwa na mifuko ya kilo moja na kujazwa kwenye “pipi” zilizopimwa kwenye uzito mdogo ya gramu 10 kila mmoja. Watuhumiwa hao walikamatwa kwenye nyumba ya Diana Jacob Namfua.

2771 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!