Katika sehemu ya tatu ya makala haya, Dk. Khamis Zephania alieleza maana na sababu za fumbatio, vidonda vya umio na jinsi vidonda vya tumbo vinavyotokea. Sasa endelea kumfuatilia katika sehemu hii ya nne…

Kuvuruga utendaji kazi wowote wa ulinzi mmojawapo hufanya kunyanzi za tumbo na utumbo mdogo kuwa rahisi kudhuriwa na asidi na pepsin na kuongeza hatari ya vidonda.

 

Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba chakula kinapoingia ndani ya mfuko wa chakula (tumbo) kwa ajili ya mmeng’enyo, tumbo huzalisha juisi mbalimbali ambapo juisi mojawapo maarufu ni hydrochloric acid kama tulivyoona. Katika mchakato wa kufanyika kidonda, asidi hiyo huanza kula kunyanzi za mfuko wa chakula (tumbo) au sehemu ya mwanzo ya utumbo mdogo (duodeni).

 

Vidonda vya aina yote hutokea kutokana na KUTOWIANA kati ya nguvu ya tumbo ya utemaji wa asidi na uwezo wa kunyanzi za tumbo/duodeni za kuzuia shambulio. Hii ndiyo sababu baadhi ya watu wanaoweza kuwa na asidi nyingi wanaweza wasipate vidonda, wakati wengine ambao wana asidi ndogo wanaweza kupata vidonda. Hii ina maana kwamba mtu anaweza kuwa na asidi nyingi lakini kunyanzi za tumbo lake zikawa na uwezo mkubwa wa kinga. Kwa hali hiyo mtu huyu anaweza asipate vidonda vya tumbo.

 

Pia, mtu anaweza kuwa na asidi ndogo, huku kunyanzi za tumbo lake zikawa na uwezo mdogo wa kinga. Mtu huyu ni rahisi kupata vidonda vya tumbo.

Uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo hutegemea:

 

1.    Vipengele ambavyo huongeza utemaji wa asidi ndani ya tumbo. Kwa mfano, vyakula vya moto na kusisimua, vyakula vya mafuta, uvutaji wa sigara kupindukia, pombe, chai, kahawa, na baadhi ya dawa kama vile corticosteroids, caffeine, reserpine n.k.

 

2.  Udhaifu wa kunyanzi au ute telezi wa   tumbo/duodeni kuzuia shambulio la asidi.

Kwa maana hiyo, katika kutibu vidonda vya tumbo, ni muhimu ama KUONGEZA NGUVU YA UKINZANI YA UTE TELEZI, au KUPUNGUZA UZALISHAJI WA ASIDI.

 

Sababu za vidonda vya tumbo:

Hakuna ugonjwa usio na sababu. Ugonjwa wa vidonda vya tumbo pia kama yalivyo magonjwa mengine una sababu zake. Kuzijua sababu ni suala muhimu sana, itakusaidia kujikinga dhidi ya ugonjwa, na pia hurahisisha matibabu.

 

Vidonda vya tumbo mara nyingi husababishwa na bakteria aitwaye Helicobacter pylori (H. pylori). Huyu bakteria kwa asilimia kubwa ndiye anayesababisha vidonda vyote vinavyodhuru mfuko wa chakula (gastric ulcers), na asilimia 95 ya vidonda vinavyodhuru sehemu ya awali utumbo mdogo (duodenal ulcers).

 

Sababu nyingine kubwa baada ya H. pylori ni kundi la dawa lijulikanalo kama non-steroidal ant-inflamatory drugs kwa kifupi ‘NSAIDs. NSAIDs ambalo husababisha takriban asilimia 20 ya gastric ulcers na asilimia tano ya duodenal ulcers.

 

Vilevile, kuna sababu nyingine kama urithi, msongo wa mawazo, uvutaji sigara, matumizi ya chai na kahawa, baadhi ya saratani, kisukari na magonjwa mengine.

 

Helicobacter pylori:

Katika mwaka 1982, Dk. Robin Warren, Muaustralia akiwashughulikia wagonjwa waliokuwa na vidonda vya tumbo, aligundua bakteria wadogo waliokuwa katika baadhi ya tumbo za wagonjwa wake. Yeye na washirika wake, Dk. Barry Marshall, waliwakuza bakteria hao waliogunduliwa kwa ajili ya matibabu na uchunguzi wa kisayansi (culture) kutoka katika sampuli za tishu, baadaye wakawapa jina ‘Helicobacter pylori.’

 

Kwa muda huo madaktari walikuwa wakiamini hakuna bakteria anayeweza kuishi ndani ya tumbo kutokana na asidi kali iliyo tumboni.

 

Dk. Warren na Dk. Marshall walishawishika kuamini kwamba bakteria huyu mpya ndiye aliyepaswa kulaumiwa juu ya vidonda vya tumbo, lakini walikuwa na wakati mgumu kuwashawishi madaktari wengine. Hivyo, Dk. Marshall alijijaribia mwenyewe kwa kunywa bika iliyojaa H. pylori.  Ndani ya siku chache, alikuwa na dalili ya uvimbetumbo (gastritis), ikiwa ni pamoja na kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo.

 

Dk. Marshall na Dk. Warren pia walionesha kwamba dawa za viua vijasumu (antibiotics) zinaweza kutibu maambukizi na kuzuia kurudi kwa vidonda vya tumbo. Dk. Warren na Dk. Marshall walitunukiwa Tuzo ya Nobel katika uvumbuzi wao huo. Baada ya ugunduzi wao, utafiti umepanuka zaidi leo, mambo mengi yanazidi kufahamika juu ya mdudu huyu.

 

Itaendelea

By Jamhuri