Vifo vya mabilioni vyatikisa

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Katika siku za hivi karibuni, sekta binafsi na jumuiya ya wafanyabiashara nchini imetikiswa na vifo vya mabilionea vilivyotokea ndani ya wiki moja.

Vifo hivyo vinajitokeza kipindi ambacho serikali inaweka mazingira mazuri ya kodi kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji

wa ndani na nje ya nchi.

Wiki iliyopita pekee wamefariki dunia matajiri watano mfululizo, vifo ambavyo vimeibua maswali na taharuki kwa jamii, ikihoji mustakabali wa biashara walizoziacha nyuma.

Tanil Somaiya (Shivacom, Ultimate Security)

Ni katika wiki hiyo tajiri mfanyabiashara, Tanil Kumar Somaiya, alifariki dunia akiziacha kampuni kadhaa za mawasiliano

na ulinzi zikiendelea na kazi.

Kifo cha Somaiya kilitokea Agosti 11, mwaka huu jijini Dar es Salaam bila sababu za kifo chake kuwekwa wazi.

Enzi za uhai wake, Somaiya aliwekeza kwenye mawasiliano kupitia Kampuni ya Shivacom na Kampuni ya ulinzi ya

Ultimate Security.

Mbali na kampuni hizo, Somaiya pia ndiye wakala aliyepewa zabuni na serikali ya usambazaji wa magari aina ya IVECO

nchini.

Kabla ya kuwa bilionea, Somaiya aliwahi kufanya kazi ya uhasibu kwenye Kampuni ya IPP. Kupitia Shivacom, Somaiya anatajwa kuwa mtu wa kwanza kuingiza vocha za simu za ‘Shivajero jero’.

Alhaj Faraj Ahmed Abri (ASAS)

Kifo cha Somaiya kimefuatiwa na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Asas Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri, kilichotokea Agosti 12, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mwili wake umezikwa Ijumaa ya wiki iliyopita katika Makaburi ya Kisutu. Asas Group ni kampuni kubwa na ya zamani zaidi inayojishughulisha na biashara ya usafirishaji wa mizigo na mafuta kwenda DRC, Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi.

Kampuni hiyo pia inajihusisha na usindikaji maziwa, ufugaji, vituo vya kuuza mafuta na biashara ya majengo (real estate).

Awali, Asas Group ilifahamika kama A.S. Abri Transporters iliyoanzishwa mwaka 1936 mkoani Iringa kabla ya kubadilika na

kuwa Asas Group of Companies mwaka 1978.

Mathias Manga (Crown Crest, Gold Crest)

Mwingine aliyefariki dunia katika kipindi hiki ni aliyekuwa mfanyabiashara wa tanzanite na bilionea maarufu wa Arusha,

Mathias Manga.

Manga alifariki dunia Agosti 12 nchini Afrika Kusini alikokuwa amesafirishwa kwa ajili ya matibabu.

Anatajwa kuwa miongoni mwa matajiri wa Tanzania wenye ukwasi mkubwa, akiwekeza katika miradi mbalimbali.

Manga amewekeza katika uuzaji na uchimbaji wa tanzanite, akimiliki Mgodi wa Manga Gems Limited uliopo kitalu D,

Mirerani, Simanjiro, mkoani Manyara.

Huyu pia alikuwa mmiliki wa hoteli za Crown Crest ya Arusha na Gold Crest ya Mwanza. Kifo chake mbali na kuwagusa

wafanyabiashara wa Arusha, pia kimewasikitisha wanachama wa CCM, kwani aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Bilionea huyu ameacha majumba mengi ya kifahari jijini Arusha.

John Lamba (Travertine Hotel)

Ndani ya kipindi hicho kifupi, pia kimetokea kifo cha John Lamba, mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya Travertine ya Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam.

Kifo kingine kilichotikisa jamii ni cha mfanyabiashara aliyekuwa akimiliki Kampuni ya mabasi ya Sumry ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, Hamoud Sumry, kilichotokea Agosti 9, jijini Dar es Salaam.

Kijana huyo pamoja na kaka yake, Salum Sumry, ndio waliendesha kwa ufanisi mkubwa operesheni za Sumry High Class

Ltd kwa miaka kadhaa. Baadaye wakaachana na biashara hiyo na kugeukia kilimo cha kisasa, ambako wanamiliki maelfu ya ekari za mahindi katika Kijiji cha China, Kate, wilayani Nkansi.

Mapema Julai 31, mwaka huu, jumuiya ya wafanyabiashara ilimpoteza aliyekuwa mmiliki wa Peacock Hotel, Joseph

Mfugale.