NAIROBI, KENYA

Joto la kisiasa nchini Kenya linazidi kupanda kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Katika hatua iliyoshitua siasa za nchi hiyo, wiki iliyopita Rais Uhuru Kenyatta alitangaza hadharani kuwa anaunga mkono upande wa upinzani chini ya kinara wao Raila Odinga.

Taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha wanasiasa mashuhuri jijini Mombasa na kuhudhuriwa na viongozi wa upinzani na Rais Kenyatta zinaeleza kuwa rais huyo ameamua kuacha kumuunga mkono makamu wake, Wlliam Ruto na kuwaeleza wapinzani hao kuwa wanapaswa kuungana chini ya Raila ili waweze kuchukua uongozi wa nchi hiyo yeye atakapoachia madaraka mwakani.

Pamoja na Raila anayeongoza Chama cha ODM, mkutano huo ulihudhuriwa pia na Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Pia mkutano huo ulihudhuriwa na Gavana wa Kakamega na Naibu kiongozi wa ODM, Wycliffe Oparnya.

Hiyo inaoekana kama mwendelezo wa juhudi za Uhuru kuwaunganisha wanasiasa wa upinzani ili waweze kumshinda Ruto ambaye naye amejizatiti kumrithi.

Uhuru, ambaye hivi sasa haelewani kabisa na Ruto, ameamua kuunga mkono wapinzani wazi wazi na mara kadhaa ameonekana akifanya kampeni kwa ajili yao.

Lakini mara kadhaa amesisitiza kuwa ili waweze kuchukua nafasi hiyo kwa urahisi ni vema wakaungana chini ya Raila.

Mkutano alioufanya wiki iliyopita katika Ikulu ya Mombasa, akiwakaribisha wanasiasa hao wa upinzani, ni moja ya juhudi zake hizo.

Uhuru ameshaeleza wazi wazi kuwa dhamira yake ni kumuona Raila akiirithi nafasi yake na si mtu mwingine.

Hata hivyo, viongozi hao wa upinzani bado hawajaweka msimamo wa pamoja iwapo wanakubaliana na pendekezo hilo la Uhuru.

Wengi wa wanasiasa hao nao wana mpango wa kuania nafasi hiyo. Baadhi yao wanaamini kuwa baada ya kushiriki kwenye uongozi wa nchi hiyo na harakati za siasa kwa muda mrefu, wakati umefika sasa kwa Raila kustaafu na kubakia kuwa mmoja wa wazee wa taifa.

Ingawa hakukuwa na taarifa zaidi kuhusiana na kikao hicho lakini kimefanyika siku chache tu baada ya Ruto kuzuiliwa na askari kwenda nchini Uganda na mwenza wake wa biashara kutoka Uturuki, Harun Aydin, kufukuzwa nchini humo kwa nguvu.


Rais Uhuru Kenyatta (katikati) akiwa amezungukwa na wanasiasa mashuhuri nchini Kenya; Raila Odinga (ODM), Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) katika Ikulu ya Mombasa. (Picha na Ikulu ya Kenya).
850 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!