Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema vyombo vya dola vimeanza kuchunguza taarifa za kuwapo kwa zaidi ya Sh bilioni 300 zilizofichwa katika benki nchini Uswisi.

 

Pinda ameliambia Bunge kuwa Serikali imepata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari, na kwamba tayari wameanza uchunguzi na baadaye watatangaza matokeo.

 

Waziri Mkuu alitoa msimamo wa Serikali alipokuwa akijibu hoja za baadhi ya wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Ofisi yake ya mwaka wa fedha wa 2012/2013.

 

Uchunguzi huo, kwa mujibu wa Pinda, unafanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kitengo cha Kiiteliejensia cha Wizara ya Fedha.

 

Habari za kuwapo mabilioni hayo nje ya nchi zimetolewa na vyombo vya habari na mitandao mbalimbali vilivyonukuu ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB).  Pamoja na Tanzania , nchi nyingine ambazo zina fedha katika benki za Uswisi ni Kenya (dola milioni 857), Uganda (dola milioni 159), Rwanda (dola milioni 29.7) na Burundi yenye dola milioni 16.7.

 

Mbunge wa awali kuibua hoja hiyo bungeni alikuwa ni Zitto Kabwe , wa Kigoma Kaskazini (Chadema).

 

Mbunge huyo alipendekeza wenye akaunti hizo watajwe. Hadi sasa kuna habari kwamba fedha hizo ni mali ya vigogo sita, wakiwamo wastaafu.

 

Akijibu hoja hiyo, Pinda alisema, “Kwa kweli hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hiyo, na sisi tunasema wabunge kupitia Kamati zetu zile tatu za masuala ya fedha na kamati nyingine za kisekta mnatusaidia sana maana lazima tubadilike ili tuweze kutoka hapa tulipo.”

 

Pinda alisema hatua kadhaa za kinidhamu zimekuwa zikichukuliwa kwa viongozi na watendaji wabadhirifu.

 

Fedha za rada

 

Kuhusu fedha za rada zilizorejeshwa, Waziri Mkuu alisema zitatumika kwa ununuzi wa vitabu na madawati, kwa kuwa ndiyo makubaliano yaliyofikiwa na pande husika.

 

Pande hizo ni Serikali kupitia Wizara ya Fedha, wakati Uingereza iliwakilishwa na DFID, BAE Systems na SFO.

 

“Matumizi ya fedha hizo yanalenga kuimarisha uendeshaji wa Elimu ya Msingi ambako asilimia 75 ya fedha zitatumika kununua vitabu vya kiada, vitabu vya mwongozo kwa walimu, mihutasari na miongozo ya mihutasari, asilimia 25 itatumika kununua madawati,” amesema Pinda.

 

Vitabu vitanunuliwa kutoka kampuni 13 za wachapishaji zilizoteuliwa ambazo ni Ben Company, Best Deal Publisher, E & D Vision, Education Books Publisher, Jadida, LongHorn, Longman, Macmillan, Mkuki na Nyota, Mture, Oxford, Taasisi ya Elimu Tanzania na Ujuzi Book.

Kampuni mbili kati ya hizo ni za nje.

 

Mnyika kumkatia rufaa Ndugai

 

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, anakata rufaa kupinga kufukuzwa kwake bungeni kwa kauli ya kumwita Rais Jakaya Kikwete ‘dhaifu’.

 

Rufaa hiyo ataielekeza katika Kamati ya Bunge ya Kanuni. Anapinga uamuzi wa a Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na uamuzi wa kumtoa bungeni

 

Mnyika alitolewa bungeni baada ya kukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’.

Mnyika anasema anakusudia kukata rufaa dhidi ya Ndugai, ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaoweka kumbukumbu sahihi, na pia yeye apate haki.

 

Anasema kutamka kuhusu udhaifu wa rais, si kumtukana wala siyo kutumia jina lake kwa dhihaka.

 

“Pamekuwapo na propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi, chanzo ni udhaifu wa Naibu Spika Ndugai, kwa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma iliyotolewa. Naheshimu taasisi ya urais na umri, naamini pia katika matumizi ya lugha za kidiplomasia, hata hivyo, niliamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili ujumbe ufike kwa mamlaka zote,” amesema.

 

Anajitetea kuwa hata viongozi wa kidini wamekuwa wakiusema hadharani udhaifu wa Rais Kikwete. Anasema wabunge wamekuwa na udhaifu kutokana na Katiba kuweka nguvu kubwa kwa rais, kwamba wasipopitisha bajeti anaweza kuvunja Bunge.

 

“Woga huo wa Rais kulivunja Bunge ndiyo maana wamekuwa wakipitisha bajeti kwa kauli za `ndiyo’ kwa asilimia 100, hata kama kuna maeneo ambayo wanayapinga. Bunge litakapokuwa likijadili utekelezaji wa bajeti katika Ofisi ya Rais ya mwaka 2012/2013 nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kufanikisha ahadi alizozitoa kwa Watanzania,” amesema.

 

Mzungu aliyeiweka ‘Serikali mfukoni’ abanwa

 

Wimbi la wageni kuingia nchini na kuiweka ‘Serikali mfukono’ limeendelea kugusa hisia za wabunge.

 

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) amesema Kampuni ya Madini ya Minerals Extractions Technologies Ltd, mmiliki wake anafanya biashara ya madini kwa njia za utapeli na ujasusi.

 

Minerals Extractions Technologies Ltd ni kampuni ambayo inafanya kazi ya kusafisha mchanga wa dhahabu katika baadhi ya migodi iliyopo Kanda ya Ziwa.

 

Imeshalalamikiwa kwa kukataa kushirikiana na mpango wa kufuatilia mapato yanayolipwa kwa Serikali na kampuni za madini, gesi na mafuta (TEIT) unaoongozwa na Jaji Mark Bomani.

 

Mohamed amependekeza iundwe kamati ya wabunge sita kutoka Kamati tatu za Bunge ili kuichunguza kampuni hiyo na mmiliki wake.

 

Mbungde huyo amesema mmiliki wa kampuni hiyo anatamba kwa kusema kwamba Tanzania hakuna mtu anayeweza kumgusa.

 

Mohamed alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Serikali ya 2012/2013. Amesema raia huyo wa kigeni anamiliki hati tano za kusafiria; tatu kutoka nchini mwake Ubelgiji; na mbili za Burundi na kwamba bado anaishi nchini licha ya kufukuzwa.

 

Alisema polisi walitakiwa wamkamate alipokuwa katika hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam , lakini kwa kuthibitisha kwamba amekuwa akiishi nchini kijasusi, taarifa hizo zilimfikia kabla ya kutekelezwa kwa mpango huo.

 

“Huyu mtu aliwahi kumtukana Kamishna wa Nishati na Madini ambaye ni mbunge mwenzetu (Dk. Dalaly Kafumu). Tumeshirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (Pereira Ame Silima) na polisi walikwenda kumkamata lakini…ndo maana nasema ni jasusi, alikuwa amekodi vyumba viwili katika hoteli ya Holiday Inn kwa hiyo hakukamatwa,” alisema Mohamed.

 

Amesema amekuwa akiliibia taifa mamilioni ya fedha kutokana na kufanya udanganyifu katika kiasi cha dhahabu ambacho amekuwa akikisafirisha kwenda nje ya nchi kila wiki na kwamba baadhi ya vyombo vya dola vinafahamu suala hilo , lakini vimepuuza kuchukua hatua.

 

“Huyu bwana amekuwa akisafirisha kila wiki kilo 15 za dhahabu kwenda nje ya nchi, lakini anafanya udanganyifu mkubwa hivyo kuliibia taifa mamilioni ya pesa, lazima Bunge hili lichukue hatua kwa kulifanyia kazi suala hili,” amesema Mohamed.

 

Aliahidi kuwasilisha kwa Spika nyaraka zinazohusu kampuni hiyo na madudu inayofanya.

 

Wachungaji hatuombei wazinzi-Msigwa

 

Wabunge wameendelea kurushiana vijembe, safari hii Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), akimjibu Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) kwamba kazi ya wachungaji si kuombea wazinzi.

 

Kauli hiyo aliitoa baada ya Nchemba kuchambua hotuba ya wapinzani na kupendekeza waombewe.

Msigwa alijibu kwa kusema hakuna kanuni yoyote ya uchumi inayosema Serikali ikiendesha mambo hovyo, ifanyiwe maombi.

 

Akasema yeye kama mchungaji huwa wanaombea wazinzi na watu waotembea na wake za watu, na si matatizo ya kiuchumi.

 

“Inashangaza sana kuona watu wanaunga mkono bajeti, kila mwaka deni la taifa linaongezeka na sasa limefika Sh trilioni 20, fedha ambazo ukizigawanya kila Mtanzania atakuwa anadaiwa Sh 400,000.

 

“Nilivyokuwa naona wabunge wamevaa suti na wanachangia hoja bungeni nilipenda jambo hilo na kutamani siku moja niwe mbunge, lakini baada ya kuingia bungeni nimegundua kuwa hakuna kitu,” alisema.

 

Alisema bunge hilo hivi sasa halieleweki na kwamba mbunge mwenye elimu ya kutosha akisimama kuchangia hoja huwezi kumtofautisha na mtoto wa darasa la pili.

 

“Yaani mbunge profesa akisimama kuchangia hoja huwezi kumtofautisha na mtoto wa darasa la pili, watu wenye akili, akili zao wameziweka mfukoni na kuweka ushabiki wa vyama mbele, tumekuja bungeni kumaliza matatizo, siyo kuongeza matatizo,” alisema Msigwa.

 

Huku akitumia mifano ya wanasaikolojia mbalimbali, alisema ni aibu kuona Watanzania wanazidi kuwa masikini harafu kila mwaka yanayozungumzwa ni tofauti na yanayotendeka.

 

“Ufikie wakati wabunge tutambue kuwa tumekuja hapa bungeni kuwatumikia wananchi, Watanzania waliotuchagua wanateseka na wabunge hapa bungeni mnazungumza maneno ya khanga tu,” alisema Msigwa.

 

Wakati wa Uchaguzi Mdogo Jimbo la Igunga mwaka jana, kuliibuka madai kwamba Nchemba alifumaniwa akiwa na mke wa mtu. Taarifa hizo hazikuthibitishwa, na haikujulikana kama kauli ya Msigwa ililengwa tuhuma hizo

 

‘Takukuru nayo ichunguzwe kwa ulaji rushwa’


Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) ameonyesha wasiwasi wake juu ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akisema nayo inapaswa kuchu.

nguza kwa ulaji rushwa.

 

Kessy alitoa wito huo alipokuwa akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, na kutamka bayana kuwa haiungi mkono.

Akasema anaweza kubadili msimamo endapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda angetoa kauli ya kuichunguza taasisi hiyo ambayo ameituhumu  kuwa imeshindwa kupambana na rushwa.

 

“Kwa muda mrefu Serikali imekuwa haisikii maoni ya wabunge, hali inayochangia kukithiri vitendo vya kifisadi mbele ya jamii.

 

“Lazima sasa Serikali itoe maelezo ya kina juu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya watu waliofanya ufisadi katika ununuzi wa rada,” alisema.

 

Alitaka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliofilisi mashirika kadhaa muhimu, yakiwamo ya Ndege Tanzania (ATCL), na Shirika la Reli Tanzania (TRC).

 

“Tunajua mna macho, lakini hamuoni, mna pua, lakini hamnusi hata harufu ya ufisadi ulioenea kila kona! Tunahitaji hata hii Takukuru tuichunguze maana imeshindwa kupambana na ufisadi mkubwa.

 

“Leo hii hizi fedha za rada hebu tunahitaji Serikali itueleze kwa kina ni kina nani walioingia mkataba na hatua gani wamechukuliwa hadi sasa.

 

“Hata suala la mifuko ya majimbo, utakuta tunapewa fedha sawa na watu waliokuwa na majimbo kama machungwa, wakati wengine majimbo yetu ni makubwa kama matikiti.

 

“Kama Serikali itaendelea kutoa fedha hizi kwa usawa, ni bora zifutwe ili kila mtu ajue anapambana vipi na hali halisi katika jimbo lake,” alisema Kessy.

 

Mbunge Hewa atuhumiwa ‘ujambazi’

 

Mbunge wa Ilemela (Chadema), Highness Kiwia, amemtaja Mbunge wa Viti Maalumu, Maria Hewa (CCM) kwamba anahusika na kutekwa kwake na kukatwa mapanga.

 

Kiwia aliambia Bunge kwamba ana ushahidi unaothibitisha kuwa gari la Hewa, lilikuwapo wakati wa tukio la kukatwakatwa mapanga.

Kiwia na Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli (Chadema), walikatwa mapanga wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirumba. Tukio hilo lilitokea Machi, mwaka huu.

 

Akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, Kiwia aliwashukuru wote walimwombea na kupata matibabu nchini India .

 

“Ninatambua ulikuwepo mpango wa muda mrefu wa kutaka kuniua, taarifa nilizipata nikazipuuzia, lakini kilichonikuta nilibaini kuwa mpango huo ni wa kweli na bado upo,” alisema.

 

Alisema mabadiliko katika jiji la Mwanza, hususani Ilemela hayawezi kuzuliwa kwa kuondolewa kwa roho ya mtu mmoja peke yake na kwamba hata asipokuwapo dhamira ya wananchi wa jiji hilo bado iko pale pale.

 

“Waasisi wa taifa hili walitarajia nchi hii itakuwa na viongozi ambao watakuwa na ndoto ya uzalendo, uadilifu na uongozi bora, Mheshimiwa Baba wa Taifa….”

 

Alipofika hapo, Naibu Spika, Job Ndugai, aliyekuwa akiongoza kikao hicho, alimtisha na kumwuliza kama ana hakika na anachokisema.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 68, na kusema, “Msemaji amesema kuwa anafahamu watu waliohusiaka kufanya jaribio ni wanachama wa CCM wa Ilemela, lakini pili anajua na uhakika juu ya taarifa za nia ya kutaka kumjua sasa huyo ni kiongozi na ni mwenzetu na nchi hii inatawaliwa na utawala wa sheria

 

“Hakuna sheria inayoruhusu mtu kutisha wala kufanya vitisho hivyo vya kumuua tena akiwa mbunge, nimesimama hapa kuomba kiti chako kimuombe mheshimiwa mbunge atoe huo ushahidi wa hao watu wanaotaka kumuua ili serikali iweze kumsaidia…moja ya jukumu la serikali ni kulinda raia wake.”

 

Kiwia alikubali kuwasilisha ushahidi na kuongeza kuwa gari la Hewa, lilikuwepo kwenye tukio.

 

Naibu Spika alimpa Kiwia siku saba awe amewasilisha ushahidi wa hayo aliyoyasema bungeni kuhusu Hewa.

 

1161 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!