Baada ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuuza nyumba zake za Kijitonyama jijini Dar es Salaam kwa Baraza la Kiswahili (BAKITA) kwa mkataba wenye utata NIC wameingia katika kashfa nyingine ya kutelekeza majengo yake kwa nia ya kuuziana kwa bei chee.

Nyumba za shirika hilo zilizoko katika mikoa ya Morogoro,  Shinyanga na jengo la Kitega uchumi lililoko jijini hapa zinaelezwa kwamba ziko katika mkakati huo wa kuzuuzwa kwa bei ya kutupa kwa maofisa wake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya Shirika hilo, nyumba zilizoko eneo la Forest Hill Mkoani Morogoro na Shinyanga ni miongoni mwa mali zinazotakiwa kuuzwa kwa utaratibu uliotolewa na Baraza la Mawaziri kwa nia kulifufua shirika baada ya kuwa na hali mbaya kwa kulemewa na mzigo wa madeni, lakini wakubwa wanataka kuchepusha.

Hata hivyo, baadhi ya nyumba hizo hazikuuzwa na Wakala wa Majengo (TBA), licha ya kuondolewa kwa watu waliokuwa wapangaji na sasa zimebaki kama magofu kwa nia ya kuzipunguza thamani ziuzwe kama viwanja.

Katika kukamilisha mkakati wa kulihujumu shirika baadhi ya wafanyakazi waliopangishwa jijini Dar es Salaam wamejitwalia nyumba nyingine katika mikoa hiyo kwa kuwaweka ndugu zao kushika nyumba kabla ya kugawana kwa kuuziana kama viwanja.

Kwa upande wa jengo la kitega uchumi la shirika hilo, mkakati uliowekwa na baadhi ya maofisa wake ni kuliuza kwa watu binafsi badala ya utaratibu uliowekwa kwamba linunuliwe na serikali kwa bei ya soko kupitia Wakala wa Majengo wa Serikali.

Maofisa hao wamekuwa wakimdanganya Mtendaji Mkuu wa Wakala, Elius Mwakalinga kwamba jengo hilo ni bovu na ukarabati wake utagharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Mwakalinga amelithibitishia JAMHURI, kwamba kumekuwa na ulaghai huo na hivyo kuamua kumchukulia hatua mmoja wa maofisa wake waliojificha katika mkakati huo kwa kumwamishia katika kituo kingine cha kazi.

Imeelezwa kwamba ulaghai huo unafanywa kwa makusudi na uongozi wa Bima na TBA kwa kuwahusisha baadhi ya maofisa wa Serikali kwa lengo la kuliua Shirika liuzwe kwa watu binafsi.

Vyanzo vyetu vimeeleza kwamba tangu Serikali ilipotoa maagizo imekuwa ikifanyika hujuma kubwa kuhakikisha mali hizo haziuzwi serikalini kupitia kwa wakala na badala yake zinunuliwe na watu binafsi na kuharibu mpango wa Serikali wa kuliboresha shirika.

“Jengo la kitega uchumi la shirika hilo halina hali mbaya ya ubovu kama inavyoelezwa, lakini ukarabati wake mkubwa ni kupaka rangi tu na ukarabati mdogo ambao hauwezi kugharimu mamilioni ya fedha.

“Hapa kuna mkakati mkubwa wa kupora mali za shirika hili na sasa ukizingatia kwamba Bodi ya Shirika la Bima ilimaliza muda wake mwezi Aprili mwaka huu, hakuna wa kuwasimamia hivyo kila mmoja anakuwa na uamuzi wake,” kinaeleza chanzo hicho.

Imeelezwa kwamba ufisadi uliofanywa na baadhi ya maofisa wa Shirika hilo ulitokana na kukosekana kwa Bodi kwa kipindi kirefu na kuiacha nafasi ya Mkurugenzi Mkuu ikikaimiwa kwa muda mrefu ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja.

Pamoja na kujimilikisha majengo hayo na mengine kuuzwa kwa njia zisizokubalika kwa kulitia hasara zaidi shirika, iwapo serikali itaendelea kufumbia macho baadhi ya watumishi wanaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za umma ndani ya shirika mzigo wa madeni utakuwa mkubwa na kushindwa kuwalipa wateja wake kwa wakati.

Hadi Desemba 31, 2008 uthaminishaji wa mali zote zisizo za msingi za biashara ya bima zilifikia Sh bilioni 31.7  ambazo zingefanikisha jitihada za Serikali za kulifufua Shirika hilo linalomilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali.

Uongozi wa Shirika la Bima umetetea uamuzi wake wa kuuza makazi kwa madai kwamba wametekeleza maagizo ya Baraza la Mawazi yaliyotolewa mwaka 2009.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa, Sam Kamanga anasema kwa sasa wamekuwa na mkakati imara wa kuboresha shirika hilo na kulifanya lijiendeshe kwa faida tofauti na lilivyokuwa awali kwani biashara ya bima ina faida licha ya kukabiliana na ushindani kutoka kwa kampuni binafsi 27.

“Shirika la Bima halina mtaji unaofikia Sh. milioni 500 wala kampuni hizo binafsi nazo hazina kiasi hicho cha mtaji, ndio maana tunafanya jitihada kuhakikisha tunajiendesha kwa faida na kulipa gawio kwa Serikali kila mwezi.

“Biashara ya bima inalipa ndio maana mkakati wetu ni kulifanya shirika liwe na tija bila kuchezea fedha na mali za umma na tumekuwa wakali kwa watumishi waliokuwa wamezoea udokozi,” anasema.

Anasema “haiwezekani tukose mashirika ya umma ambayo tunaweza” kujivunia kwa faida ya wananchi wote na kutoa mfano kwa nchi ya Ethiopia ambayo imekuwa na shirika lake la bima linalomilikiwa na Serikali kwa kuendesha biashara hiyo kwa mafanikio makubwa.

“Kama kwa nchi hiyo na nyingine wamefanikiwa kuendesha biashara hiyo ya bima nasi tunaweza kufanya zaidi yao,” anasema.

By Jamhuri