Mwaka 1974 hadi 1978 nilikuwa Katibu Mkuu wa kwanza miongoni mwa waasisi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), Dar es Salaam. Mwaka 1976 Katibu wa wanachuo, Chuo cha TANU Kivukoni, na Katibu wa TANU (Radio Tanzania Dar es Salaam-RTD) kazini.

Katika madaraka yangu hayo nilikuwa bado kijana. Katika kuwaongoza wacheza mpira wa miguu, mashabiki na wanachama wa klabu za mchezo huo pamoja na wasomi chuoni na wafanyakazi kazini, niliweza kubaini kumbe kuna aina mbalimbali za viongozi katika mustakabali wa maendeleo ya jamii yoyote duniani.

 

Si hivyo tu, niliweza kutambua kumbe kuna viongozi wa siasa, utawala, taaluma, ulinzi na usalama, maadili, michezo, mila na desturi na kadha wa kadha ndani ya mfumo wa maendeleo ya jamii.

 

Tambuzi zangu zilinifikisha kuona na kuthibitisha miongoni mwa viongozi wote hao kuna migongano ya maslahi, taaluma, uwezo, udugu na upendeleo katika kupeana au kuchaguana kushika madaraka na uongozi – uwe ndani ya kundi au kundi na kundi jingine.

 

Katika kutambua madaraka, migongano na aina ya viongozi niliweza kuweka viongozi hao katika makundi matatu. Kiongozi mtaji, kiongozi kilemba na kiongozi halisi. Dhamira, malengo na mwelekeo wao wa kuleta maendeleo ya watu ndani ya jamii haukuwa kamilifu kama walivyokusudia na wakati mwingine hupotea kwa sababu miluzi yao haikufanana.

 

Dhamira ya kiongozi mtaji ni kushika madaraka akiwa na malengo ya kujinufaisha kwa kuwatumia anaowaongoza kama mtaji, nyenzo au ngazi ya kumfikisha katika malengo yake ya kuwa tajiri na ya kuwatia umaskini anaowaongoza. Mali na fedha ndiyo maoni yake. Huyu ni kiongozi mbaya sana, fisadi.

 

Kiongozi kilemba madhumuni yake ni kuwa mtukufu, mkubwa na mwenye mikogo tu. Hujisikia ufahari na ukubwa anapoitwa, Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, au Mheshimiwa Mbunge na kadhalika. Ni mchache wa mawazo au rai ya kuleta maendeleo ya watu. Analoambiwa hulipokea hata kama lina kasoro au madhara. Hana upeo wa kuhoji. Ni mwingi wa maneno na bla blaa. Huyu ni kiongozi hatari sana.

 

Kiongozi halisi nia yake kubwa ni kuleta maendeleo ya watu na nchi yake na kuishirikisha jamii yake katika nyanja mbalimbali za kuleta maendeleo. Lengo lake kila mtu awe na maisha bora. Kauli na vitendo vyake huwa dira na mwongozo mbele ya anaowaongoza kwa sababu zina ukweli na zinatekelezeka. Ni msikivu na mwenye huruma, upendo na haki. Huyu ni kiongozi adilifu.

 

Nimesema miluzi yao haifanani kwa sababu kila kundi la viongozi lina madhumuni na malengo kutokana na dhamira zao za dhati moyoni. Lakini mbele ya uso wa wanajamii, viongozi wote wanaonesha sura za upendo, huruma na kujali shida za wanajamii. Wanaeleza wako mstari wa mbele katika kutafuta tiba sahihi ya kuwaondolea wanajamii maovu na machungu.

 

Ushahidi upo wazi, si leo si jana, wala si juzi, Watanzania tumepata kuona na kusikia kutoka kwenye majukwaa, mikutano, ofisini na vikao vya mipango na vya utendaji, viongozi wanavyounguruma, wanavyopandisha jazba, hata wengine kudiriki kulia na kuapa mbele ya Mwenyezi Mungu hawatakubali kuendelea kuona maovu na machungu wayapatayo wanajamii. Watahakikisha wanaondoa madhila yote hayo.

 

Baada ya kueleza hayo, sasa niende kwenye mada ya leo. Vijana hamna budi kuwa macho na aina ya viongozi wanaotaka muwachague ili wawaongoze katika harakati za kuleta maendeleo yenu binafsi na ya Taifa letu. Ni haki na wajibu wenu kuwapima kabla ya kuwapa uongozi.

 

Muwapime kwa kauli zao, vitendo na desturi zao ndani ya jamii. Daima kiongozi bora na mwenye manufaa hatangazwi. Hujitangaza mwenyewe kutokana na uadilifu wake mbele ya jamii. Mtu anayetangazwa, anayetumia fedha kama mtaji wa kuwa kiongozi hafai kuwa kiongozi.

 

Wanaotaka kuwa viongozi baadhi yao hupenda kuwa na wapambe, kutoa hongo na rushwa, kusema maovu ya wenzao, hujifanya wasamaria wema kutoa kashata. Wengine hutoa machozi mithili ya mamba akamataye mtu mtoni, huku analia, huku ana mla na kupoteza maisha ya mtu!

 

Ninayosema yamekwishatokea tangu tupate Uhuru na hasa ujio wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Vyama vya siasa vimepoteza sifa ya kutoa viongozi bora kwa sababu ya kutumia fedha, wapambe na vilio vya mamba.

 

Ofisi za umma nazo zimelalamikiwa kupuuza kanuni na sheria za utumishi, badala yake kufuata udugu na upendeleo. Wanaofanya yote hayo na wanaolalamika ni vijana wenyewe! Kulikoni?

 

Vijana, pimeni yanayotokea kwenye mikutano ya hadhara ya siasa kuhusu kashfa na masimango yanayotolewa na viongozi dhidi ya viongozi wenzao. Matusi, kejeli na ugomvi unaofanywa bungeni, mvutano wa madaraka na ukweli kati ya viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wabunge na vyama vya siasa.

 

Pamoja na kutambua ujana wenu ni maji moto, wenye damu inayochemka, misuli yenye nguvu bado muoneshe kuwa mna hekima pevu, weledi wa mambo na muono wa mbali katika kujenga Taifa la Watanzania.

 

Busara yenu inatakiwa mbele ya wazee wenu. Kama si busara ya vijana wa zamani, leo vijana msingekuwapo na wazee hawa msingewaona. Tafakari sana makundi yale matatu.

1160 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!