Kuna kundi kubwa la wananchi ambao wamekuwa wakizunguka katika ziara anazofanya Rais Dk. John Magufuli kwa lengo la kufikisha kero zao kwake. 

Watu hao wamefikia hatua hiyo baada ya viongozi na watumishi katika ngazi nyingine kushindwa kuwasaidia kutatua matatizo yao. Hili linasikitisha sana.

Viongozi hawa na watumishi wanapaswa kufahamu kuwa walichaguliwa, kuteuliwa au kuajiriwa kushika nyadhifa walizo nazo ili kuwahudumia wananchi wenye shida na matatizo mbalimbali. Jukumu lao la kusukuma maendeleo litakuwa na maana zaidi iwapo shida na kero zinazowakabili wananchi zitatatuliwa kwa wakati.

Lakini kwa bahati mbaya sana, inaonekana kuwa viongozi wengi nchini hawatimizi wajibu wao sawasawa kutatua kero na shida zinazowakabili wananchi katika maeneo yao. Ndiyo maana huwa wanakimbilia kwa rais ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao.

Siku hizi hata rais mwenyewe anapokuwa katika ziara anatambua kuwa kuna watu ambao wanataka kufikisha shida zao kwake. Ndiyo maana katika hotuba zake hujitahidi kuweka muda kwa ajili ya watu kutoa kero zao kwake. Wakati mwingine huwataka askari kuwaruhusu watu waonyeshe mabango yao ambamo wameandika kero mbalimbali zinazowakabili.

Katika siku za hivi karibuni JAMHURI limekuwa likipokea watu mbalimbali ambao wanatoa kilio kwa rais wakimwomba awasaidie kupata ufumbuzi wa matatizo yao baada ya viongozi wengine wa ngazi za chini kushindwa kuwasaidia.

Haya yote yanadhihirisha kuwa viongozi wa ngazi za chini hawatekelezi kikamilifu jukumu lao la kuwatatulia wananchi kero mbalimbali zinazowakabili. Kama hilo lingekuwa linafanyika, basi vilio vinavyoelekezwa kwa Rais Magufuli na watu wa kawaida vingepungua sana.

Wanachofanya viongozi hawa si tu kushindwa kutekeleza majukumu yao bali ni kumtegea rais ambaye sasa analazimika kufanya kazi ambazo wasaidizi wake walipaswa kuzifanya.

Matokeo ya hiki kinachofanywa na viongozi hao ni kuchelewesha maendeleo kwa Watanzania wote, kwa sababu badala ya kushughulikia masuala yanayopaswa kushughulikiwa na kiongozi wa nchi, Rais Magufuli analazimika kutumia muda huo kufanya kazi ambazo zilipaswa kufanywa na viongozi wengine. 

Mbaya zaidi, unaweza kukuta masuala yenyewe ambayo Rais Magufuli analazimika kuyashughulikia si makubwa sana ambayo iwapo viongozi wa ngazi za chini wangeamua kuyashughulikia wala yasingechukua muda mrefu kuyatatua.

Kwa maana nyingine, viongozi hawa wanaomtegea Rais Magufuli wanawahujumu Watanzania wote, kwa sababu wanaiba muda ambao rais angeutumia kushughulikia masuala mengine.

12440 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons