Tulijikomboa ili tuwe huru, tuondokane na dhuluma

Watanzania wameadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika. Hizi ni sherehe kubwa kwa sababu zinaturejesha kwenye kumbukumbu za kazi kubwa iliyotukuka ya ukombozi iliyofanywa na waasisi wa taifa letu.

Hatuna budi kuadhimisha siku hii kwa kufanya tathmini ya hali iliyokuwa kabla na baada ya Uhuru na miongo hii ambayo inaelekea kufikia sita.

Historia ya Uhuru wetu haina budi kufundishwa katika ngazi zote za shule na vyuo ili kuwawezesha vijana wengi kutambua na kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu katika kupigania Uhuru wetu. Sharti tuwape elimu vijana ili watambue kuwa mapambano ya Uhuru haikuwa kazi nyepesi kama baadhi wanavyodhani.

Uhuru tuliopata ni uhuru wa bendera, yaani tulishusha bendera ya mkoloni na kupandisha bendera ya Tanganyika huru. Mapambano ya kudai uhuru hayakomei kwenye bendera pekee. Bado tunayo vita mpya – vita ya kiuchumi – inayohitaji mshikamano na weledi wa hali ya juu zaidi. 

Uhuru wetu utakuwa hauna maana kama Watanzania wataendelea kuishi kwenye madhila na dhiki kubwa. Uhuru wetu, kama ulivyoainishwa na waasisi, lazima utuwezeshe kuwashinda maadui wakuu watatu – ujinga, maradhi na umaskini.

Miaka 58 sasa bado tunao maadui hawa, na kwa kweli kunahitajika juhudi za kila mdau kwenye vita hii ili kuhakikisha ushindi unapatikana.

Wazee wetu waliamua kuingia kwenye mapambano ya kudai Uhuru ili kuwafanya wao na vizazi vilivyofuata wawe huru – na wafaidi matunda yatokanayo na rasilimali za nchi yetu.

Uhuru haukulenga kumwondoa mkoloni tu ambaye alikuwa Mzungu, bali ulilenga kuhakikisha wakoloni na vibaraka wao – bila kujali rangi zao – wanakoma kuwadhulumu wananchi.

Uhuru haukumaanisha kuwa waondolewe Wazungu na mbadala wao wawe weusi au watu wa rangi nyingine. Vipo vimelea vinavyoashiria kuwapo kwa baadhi ya viongozi katika ngazi mbalimbali walioamua kuwa wakoloni weusi.

Ziara za rais na viongozi wengine wakuu tunaona zinavyogubikwa na malalamiko mengi ya wananchi wanaodhulumiwa. Ziara hizi zimegeuzwa kuwa viwanja vya kumwaga machozi kutoka kwa wanyonge. 

Haya yanafanyika ilhali nchi ikiwa na viongozi kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi taifa. Tusiruhusu kuendelea kwa hali hii. Viongozi hawana budi kuwatumikia wananchi.

Uhuru wa kweli ni ule unaohakikisha kila mwananchi anatendewa haki katika nyanja zote kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Uonevu, dhuluma na unyanyasaji ni matendo yanayoathiri haki na uhuru wa watu.

tuondokane na dhuluma