Hivi karibuni serikali ilitangaza kuwa imeanza mchakato wa kujitoa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Serikali ilieleza kuwa imeamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona hoja ambazo ilizitoa wakati inajiunga na mahakama hiyo hazijafanyiwa kazi.
Tunadhani kuwa sababu hii haijitoshelezi kwa serikali kuchukua uamuzi mkubwa kama huu ambao unaathiri watu wengine wengi.
Tunaamini hivi kwa sababu kujitoa kwa Tanzania hakutasababisha kutekelezwa kwa hoja hizo. Tunaamini kuwa serikali ilitoa hoja za msingi ambazo utekelezaji wake ungeboresha shughuli za mahakama hiyo za kutoa haki kwa wakazi wa Afrika.
Badala ya kujitoa, serikali ilipaswa kuweka shinikizo kubwa ili mahakama hiyo itekeleze hoja zake. Utekelezaji wa hoja za Tanzania ungesaidia kuboresha shughuli za mahakama na kuwapa faida Waafrika ambao wanaitumia mahakama hiyo.
Tunaamini pia kuwa kama nchi ambayo inajinasibu kuwa kinara wa kufuata na kuheshimu haki za binadamu, Tanzania haipaswi kujitoa katika chombo ambacho kimeundwa mahususi kwa ajili ya kuhakikisha haki za binadamu zinafuatwa na kuheshimika.
Tanzania ilipaswa kuwa kinara wa kuhakikisha kuwa chombo hiki kinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni bora ili kuhakikisha kile ambacho nchi inakisimamia katika suala la haki za binadamu kinafuatwa pia na nchi nyingine za Afrika.
Tanzania, kama moja ya nchi zinazoheshimika barani Afrika na duniani kwa ujumla katika suala la haki za binadamu, haipaswi kuacha kuifanya kazi hii ya kuhakikisha kuwa vyombo vilivyoundwa kwa ajili ya kusimamia masuala muhimu kama haya ya utawala bora vinafanya kazi kwa weledi na kwa mujibu wa kanuni bora kabisa.
Tunaamini kwa dhati kuwa serikali haipuuzi hata kidogo masuala ya haki za binadamu na ndiyo maana hilo ni moja ya mambo ya msingi sana ambayo yanatumika kupima iwapo serikali na taifa linaendeshwa kwa misingi bora.
Kama haya yanafanyika hapa nyumbani, ni jambo la busara kuhakikisha kuwa tunazihimiza nchi nyingine Afrika kuyafuata, kwani yanasaidia kuleta ufanisi.
Hivyo, tunaiomba serikali irejee uamuzi wake wa kujitoa katika mahakama hii na badala yake ishinikize na ihakikishe kuwa masuala ambayo ingependa kuona yanatekelezwa kama njia ya kuifanya mahakama ifanye kazi kwa ufanisi yanatekelezwa.
Kwa kufanya hivyo Tanzania itakuwa imezisaidia nchi nyingine za Afrika kuwa na chombo bora kinachochunga haki za binadamu.

714 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!