Vurugu za Mtwara ni uhuni na upuuzi

Kwa mara nyingine, wahuni kadhaa katika Mji wa Mtwara jana waliendesha vitendo vya uvunjifu wa amani. Watu kadhaa wameripotiwa kuuawa, kujeruhiwa na mali za mamilioni ya shilingi zimeteketezwa.

Hoja ya wahuni wanaoendesha vitendo vya vurugu ni kwamba hawataki utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

 

Awali, wananchi wengi waliunga mkono msimamo wa wana Mtwara wa kutaka Serikali iwaeleze wananchi hao ni kwa namna gani watanufaika na uwepo wa gesi. Serikali kwa upande wake imejitahidi sana kuwaeleza faida hizo. Kumechapishwa makala mbalimbali kueleza faida hizo, lakini msimamo wa baadhi ya wana Mtwara ni kuona gesi ghafi haisafirishwi kwenda Dar es Salaam.

 

 

Tunalaani kwa nguvu zote vurugu zinazosababishwa na kikundi cha wahuni waliochoka amani. Mwelekeo wa vurugu za sasa unaashiria kuwa hapa suala si gesi tu, bali huenda kukawa na nguvu nyingine nyuma ya suala hili. Nguvu hizo si nyingine, bali ni za kufifisha na hatimaye kuondoa sifa nzuri ya Tanzania ya kuitwa kisiwa cha amani na utulivu.

 

 

Tunasema hivyo kwa sababu hatuoni uchomaji mali za wananchi na za umma, tena yakiwamo magari ya wagonjwa, kama kuna uhusiano wowote na suala la gesi.

 

 

Matukio mengi ya uvunjifu wa amani yameendelea huku viongozi wa Serikali wakiwa hawaoneshi umakini katika kuupatia ufumbuzi mgogoro huu. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alithubutu kwenda Mtwara kutuliza mambo, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba hakufanikiwa.

 

Rais Jakaya Kikwete hajafanya juhudi za kwenda yeye mwenyewe kulitatua suala hili. Hatuamini kama intelejensia imeshindwa kumpa ukweli wa Mtwara ili yeye kama kiongozi mkuu wa nchi, aweze kuleta suluhu ya jambo hili.

 

Historia inaonesha wazi kwamba mataifa yote yaliingia kwenye migogoro mikubwa kwa kuanza na mambo kama haya ya “changu, changu, chako chetu”. Nigeria imekuwa kwenye mgogoro mkubwa kutokana na mambo ya aina hii, na pengine kutokana na watawala kuchelewa kuchukua hatua za kuzima cheche na viashiria vya migogoro hii.

 

Tunachukua fursa hii kuwalaani wahuni wote wanaojihusisha kwenye vurugu hizi. Hawa tunawaita wahuni kwa sababu hatudhani kama kweli wao kama sehemu ya nchi, wana haki pekee ya kuitumia gesi inayozalishwa Mtwara.

 

Mtindo huu ukiachwa uendelee, siku moja Tanzania itakuwa vipande vipande. Watajitokeza wananchi katika maeneo mengine kudai wafaidi wao peke yao rasilimali zilizo katika maeneo yao.

 

Ndiyo maana tunachukua fursa hii kuwasihi wana Mtwara na wananchi wote wapenda amani, kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili utatuzi wa jambo hili upatikane kwa njia za amani. Tunatambua kuwa Tanzania ina Jeshi lenye nguvu, lakini ni kujidanganya kuamini kuwa Jeshi linaweza kutuliza na hatimaye kuumaliza mgogoro huu.

 

Sote kwa pamoja tuungane na kuiona Tanzania ni nchi yetu sote. Rasilimali za nchi ni busara zikatumiwa na Taifa zima. Wanaochochea mgogoro huu lazima wasakwe na waadabishwe kwa mujibu wa sheria. Wanasiasa na viongozi wa dini wawe mstari wa mbele kuwapoza watu wao. Hatupo tayari kuiona Tanzania ikichafuka kwa maslahi au kiburi cha wahuni na wapuuzi wachache. Vurugu za Mtwara zimetosha.