Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA), inahudumia Wakazi wapatao 194,756.

Hii ni kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 pamoja na wakazi wengine 30,000 waliopo maeneo ya Wilaya za Hai na Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Kwa sasa mamlaka hiyo ina wateja wapatao 23,123 wanaopata huduma ya maji safi na salama kutoka chemchem nne na visima virefu ambako uzalishaji wa maji safi na salama unakadiliwa kuwa ni wastani wa mita za ujazo 34,944 kwa siku iikilinganishwa na mahitaji ya mita za ujazo 45,082 kwa siku.

Hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Moshi kwa sasa ni wastani wa saa 18 hadi 24 kutegemea na eneo lilivyo ambako mamlaka hiyo imeugawa Mji wa Moshi katika kanda tisa ambazo ni Maili Sita, Shanty Town, Soweto, City Centre, Majengo, Bomambuzi, Chekereni na Himo.

Mamlaka hiyo ambayo ni moja ya mamlaka kubwa hapa nchini, imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha huduma kwa wakazi wa Mji wa Moshi ikiwamo utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza maji na kuwafikia wateja wengi zaidi.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha maji ya Coffee Curing chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 700 kwa siku, ujenzi wa chemchem ya mto karanga mradi utakaoongeza mita za ujazo 3,800 kwa siku.

Pamoja na jitihada hizo nzuri za MUWSA katika kuwapatia huduma bora ya maji safi na salama wakazi wa Mji wa Moshi na maeneo ya mji mdogo ya Himo, zipo changamoto kadhaa zinazoweza kukwaza ndoto hizo.

Moja ya changamoto hizo ni kuwapo na wateja wasiolipia ankara za maji kwa muda mwafaka na hivyo kuwapo na malimbikizo makubwa ya madeni na hawa hatuna budi kuwaita wadaiwa sugu.

Miongoni mwa wadaiwa hawa sugu ni taasisi za serikali ambazo zinadaiwa kiasi cha Sh bilioni 1.2, fedha hizi ni nyingi na endapo zitalipwa zinaweza kutumika kuboresha miundombinu ya maji na wananchi wakapata maji ya uhakika bila ya mgawo.

Deni hilo ambalo linatajwa kuendelea kuongezeka limekuwa kikwazo kwa juhudi za MUWSA za kufikisha huduma bora ya maji safi na salama na uondoaji wa majitaka kwa baadhi ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Joyce Msiru alizitaja taasisi hizo za serikali na kiwango cha deni wanachodaiwa kuwa ni pamoja na Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa (RPC) inayodaiwa Sh milioni 528.6; Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA) Sh milioni 401.9 na Gereza Kuu la Mkoa  la Karanga Sh milioni 203.7.

Mkurugenzi huyo akabainisha kuwa, taasisi hizo hazijalipa ankara za maji kwa muda wa miaka saba hadi sasa na zimekuwa hazionyeshi dalili zozote za kulipa licha ya kuwa wanaendelea kupata huduma hiyo kama wateja wengine.

Kutokana na deni hilo kuendelea kukua siku hadi siku huku kukiwa na jitihada duni za kulipwa kwa madeni hayo, Desemba 28, mwaka jana, Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka kwa kauli moja ikaiagiza menejimenti kutoa notisi ya siku 14 kwa taasisi hizo ziwe zimelipa madeni hayo vinginevyo huduma ya maji isitishwe.

Akawaeleza wanahabari kuwa mamlaka yake inayo miradi mingi ya kutekeleza ili kuwapatia huduma ya maji safi na salama wananchi, lakini kikwazo kikubwa ni fedha ambazo kiasi kikubwa zipo mikononi mwa taasisi hizo.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na upanuzi wa mtandao wa maji katika vitongoji vitano vilivyopo katika kijiji cha mabogini ambavyo ni Shule, Mpirani, Rau-Msufini, Sanyaline A na Kitongiji cha Mjohoroni.

“Wasipolipa madeni yao, tutasitisha huduma ya maji kwenye taasisi hizo na maji hayo tutayaelekeza kwenye maeneo mengine, madeni haya yamekwaza upanuzi wa miradi ya maji ambayo ingeweza kutatua tatizo la maji kwa wakazi wa Mji wa Moshi,” anasema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mamlaka hiyo inahitaji kiasi cha Sh milioni 459.081 kwa ajili ya ukarabati wa chemichemi ya Njoro ya Goa na ukarabati wa tanki la maji lililotelekezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi vijijini fedha ambazo alidai zinatoka ndani ya mamlaka yake.

Akaiomba Serikali ya Rais John Pombe Magufuli  kusaidia upatikanaji wa fedha ambazo mamlaka hiyo inazidai taasisi hizo ili ziweze kutumika kuboresha huduma ya maji ndani ya Manispaa ya Moshi na viunga vyake.

Mwaka  jana kilio hiki cha MUWSA kilitolewa mbele ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala ambaye kwa sasa ndiye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati akiwa katika ziara ya siku mbili mkoa hapa ya kutembelea na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji.

Aliyetoa kilio hicho alikuwa ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Elizabeth Minde wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo.

Alikwenda mbali kwa kudai kuwa, taasisi hizo hazitoi kipaumbele cha kulipa madeni hayo licha ya kuwa kila mwaka wa fedha zimekuwa zikipokea fedha kutoka hazina kwa ajili ya kulipia huduma za maji.

Makalla alikuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro ambako pamoja na mambo mengine alizindua chanzo kipya cha maji kilichopo Mto Karanga ambacho kinazalisha mita za ujazo 3,800 kwa siku na kunufaisha maeneo ya Bomambuzi, Pasua, Matindigani, Kaloleni, Soweto na Kiboriloni na viyongoji vitano vilivyopo katika Kijiji cha Mabogini. 

Ni kweli kwamba taasisi nyingi za Serikali zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara na watoa huduma kwa kushindwa kulipia huduma wanazopewa na taasisi mbalimbali licha ya kwamba wizara zao hutenga kwenye bajeti zake fedha kwa ajili ya taasisi zilizo chini yake.

Malalamiko haya yamekuwa ni ya siku nyingi na sasa yanaonekana kuwa sugu kutokana na taasisi husika kutoona umuhimu wa kulipia huduma hizo licha ya kuzihitaji kwa udi na uvumba na hivyo kuibua malumbano baina ya watoa huduma na watumiaji wa huduma.

Pamoja na mamlaka hiyo kuendelea kuzidai taasisi hizo, walimweleza Makalla kwamba bado wanaendelea kuzipatia huduma ya maji bila kusitisha huduma hizo kwa kile walichodai ni kutokana na mahitaji makubwa ya maji katika maeneo husika ya wadaiwa hao.

Kwanza ni jambo la kuwapongeza MUWSA kwa kuonesha moyo wa huruma wa taasisi hizo nyeti ambazo kwa hakika zikisitishiwa huduma hiyo panaweza pakatokea mtikisiko mkubwa unaoweza kuchafua hali ya hewa.

Wakati nikiwapongeza mamlaka hiyo kwa kuonesha uungwana kwa wadaiwa hao sugu, nashindwa kupata jibu la moja kwa moja kwamba ni kweli taasisi hizo hazina uwezo wa kulipia ankara za maji kiasi cha kuonewa huruma ya kutokusitishiwa huduma hiyo?

Swali hili haliwezi kupata majibu kwa sababu wakati MUWSA wakiwaonea huruma wadaiwa hawa wa mamilioni ya fedha, imekuwa mstari wa mbele kuwasitishia huduma wateja wake ambao madeni yao hayafikii hata robo ya fedha wanazozidai taasisi hizi.

Napata wakati mgumu kuelewa ni mfumo upi unaotumiwa na mamlaka hiyo kuwasitishia huduma wateja wake wadogo baada ya kuwatumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu zao za kiganjani na kuwapa siku saba wawe wameshalipia ankara zao.

Kama MUWSA wameweza kuwakabili wateja wadogo kwa kuwasitishia huduma za maji kwa kuwatumia ujumbe huo wa simu, wanashindwaje kufanya hivyo kwa wateja hao wakubwa ambao sasa wanaendelea kutumia huduma wasiyoilipia bila hofu wala woga. 

Wakati umefika sasa kwa mamlaka hiyo kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ili fedha zitakazopatikana zitumike katika kuboresha miundombinu ya maji pamoja na upanuzi wa miradi ya maji  ili watumiaji wa maji katika mji wa moshi waondokane na kero ya mgawo wa maji ambao umeanza kujitokeza hasa nyakati za kiangazi.

Itakuwa ni jambo la kushangaza kama si kuchekesha kwa mamlaka kubwa kama hiyo kushindwa kuchukua hatua kwa wadaiwa hao ambao iliwatangaza rasmi kwenye vyombo vya habari kuwa ni wadaiwa sugu.

Alipoingia madarakani Rais John Pombe Magufuli aliwaeleza Watanzania kuwa amejipa kazi ya kutumbua majipu (kupambana na ufisadi) na kazi ya kutumbua majipu ni ngumu hivyo MUWSA, wadaiwa hawa sugu ni majipu lazima yatumbuliwe na namna ya kuyatumbua ni kuwasitishia huduma ya maji.

1492 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!