Kuanzia leo safu hii itakuletea orodha ya watu kumi wanaotajwa kuwa ni wadunguaji hatari duniani.

Udunguaji ni taaluma maalumu inayotumiwa na aghalabu askari, kulenga shahaba na kuwapiga risasi watu au vitu vilivyo katika umbali ambao kwa kawaida ni vigumu kulenga shabaha kwa ufasaha.

Ni kazi inayohitaji utulivu wa mwili na akili. Baadhi ya wadunguaji hutumiwa na mamlaka za serikali, hasa taasisi za upelelezi na majeshi, kuwaua maadui zao.

Kwa kawaida mdunguaji huifanya kazi yake kwa kujificha ili kutoonekana kwa yule anayemlenga. Aghalabu, mdunguaji huwa mbali sana na shabaha ili kuepusha kujulikana kuwa anafanya nini.

Pamoja na kuua kwa kutumia bunduki, lakini wadunguaji wataalamu pia hufundishwa teknolojia nyingine za kipelelezi kama vile kufuatilia watu bila kujulikana, uwezo mkubwa wa kulenga shabaha, uwezo mkubwa wa kujificha, uwezo mkubwa wa kuingia katika kundi la adui bila kujulikana, uwezo mkubwa wa kufanya uchunguzi wa eneo kwa kipindi kifupi na uwezo wa kuigundua shabaha haraka, miongoni mwa mambo mengine mengi.

Lakini pia wapo wadunguaji ambao hutumiwa na makundi na magenge ya kuhalifu ambayo huwalipa ili kuwamaliza mahasimu wao.

Leo tuanze ripoti hii kwa kumuangalia Thomas Plunkett. Huyu alikuwa ni mwanajeshi katika jeshi la Uingereza akitumikia kikosi cha British 95th Rifles. 

Kinachomfanya aingizwe katika orodha ya wadunguaji kumi hatari duniani akiwa katika nafasi ya kumi, ni rekodi aliyoiweka ya kuweza kumdungua Jenerali wa Kifaransa, Auguste-Marie-François Colbert, ambaye alikuwa ni mwanajeshi matata sana.

Katika vita ya Cacabelos mwaka 1809, Plunkett akitumia rifle, aliweza kumpiga risasi jenerali huyo wa Kifaransa akiwa umbali wa meta 600.

Alipata sifa kwa sababu katika kipindi hicho, bunduki aina ya rifle ilikuwa haina uwezo mkubwa sana wa kupiga vitu vilivyo mbali kwa ufanisi. Lakini Plunkett aliweza kuitumia bunduki hiyo hiyo isiyoaminika na kuweza kummaliza jenerali huyo aliyekuwa tishio.

Ili kuwathibitishia wenzake kuwa hakubahatisha kumdungua jenerali huyo, Plunkett aliamua kurudia tukio hilo. Baada ya kumdungua jenerali, akaweka risasi nyingine kwenye bunduki yake na kumlenga meja aliyekuja kumsaidia jenerali aliyekuwa ameanguka baada ya kupigwa risasi. 

Risasi hiyo nayo ilimpata meja huyo kwa ufanisi mkubwa na kumuua na hilo lilithibitisha kuwa Plunkett hakubahatisha.

Kwa kawaida, katika kipindi hicho askari waliokuwa kwenye kikosi cha Plunkett walikuwa wamefundishwa kulenga shabaha katika umbali wa meta 50 tu lakini Plunkett aliweza kulenga  shabaha iliyo umbali wa mara 12 ya huo waliofundishwa.

Katika Vita ya Pili ya Buenos, kikosi cha Plunkett kilishiriki katika mapigano ya mitaani na Plunkett alifanikiwa kuwadungua wanajeshi takriban 20 wa Hispania akiwa amejificha juu ya paa la nyumba.

560 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!