Malalamiko ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) dhidi ya Mtendaji Mkuu wao huenda yakapatiwa ufumbuzi leo katika mkutano na viongozi wa ngazi za juu.

Wafanyakazi hao wanalalamika kuwa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Dk. Akwilina Kayumba anawaongoza kimabavu huku wakimhusisha na matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya OSHA, Gideon Nasari ameithibitishia JAMHURI kwamba amepanga kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Eric Shitindi kwenda kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi hao Dar es Salaam leo.

 

“Tumekubaliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira kwenda kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wa OSHA Jumanne ijayo (leo), ninataka jambo hili lipatiwe ufumbuzi,” amesema Nasari. Amesema ataongoza vikao vitatu tofauti, ambapo ataanza kukutana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Dk. Kayumba, baadaye menejimenti ya mamlaka hiyo kabla ya kukutana na wafanyakazi wote.

 

“Ninategemea kupata ushirikiano kutoka kwa Katibu Mkuu huyo au mwakilishi wake, lakini hata wasipokuja ninajua nina wajibu wa kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi hao,” ameongeza mwenyekiti huyo.

 

Wafanyakazi wa OSHA wamesema watakuwa huru kuanika wazi unyanyasaji wanaofanyiwa ikiwa Mtendaji Mkuu wao huyo hatashirikishwa katika mkutano wao na viongozi hao.

 

Hivi karibuni, Dk. Kayumba alizungumza na JAMHURI na kuzikana tuhuma za kuwanyanyasa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

 

“Hayo yote unayoyasema sijawahi, sichukui hata senti ya Serikali, najua hapa Tanzania kuna watu ambao wako corrupt (wala rushwa) mimi siko corrupt (si mla rushwa), lakini kuna mahali ninatakiwa nilipwe kama vile kuandaa hotuba. Mimi ni mtoto wa mkulima, nawapenda wafanyakazi wangu,” amesema Dk. Kayumba.

 

1062 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!