Ndugu zangu, tunapokuwa tunajiuliza mhemuko wa udini unatoka wapi au nani wameusababisha na kuuasisi, si vibaya tukajua maadui wakuu kwa upande wetu Waislamu.

Ukimjua adui ni rahisi kupambana naye na ni nusu ya ushindi kwenye vita ya kutafuta haki au usawa au kuondoa tunaouita unyanyasaji kwa Waislamu au mfumo Kristo kama wengine wanavyopenda kuuita (Mimi si muumini wa dhana ya mfumo Kristo) maana nimeona wakati wote Waislamu wenzangu wakishika nafasi kubwa serikalini, kwenye mashirika ya umma na hata mashirika binafsi.

 

Siuoni mfumo Kristo kama unavyoitwa au kama baadhi ya Waislamu wenzangu wengine wanavyotaka kuaminisha umma wa Kiislamu juu ya hii dhana. Nasema sioni kwa kuwa bado naamini katika uwezo na si mfumo Kristo, siuoni kwa kuwa hii nchi ni ya Wakristo, wapagani, Waislamu, Wahindu na dini nyingine.

 

Siuoni mfumo Kristo kwa kuwa nimeshuhudia watu kama kina Omari Mahita, na Said Mwema wakiwa viongozi wa vyombo ambavyo mara kadhaa vimesababisha mauaji ya Waislamu wenzetu na ndugu zetu Wakristo.

 

Mtanisamehe wenye mtazamo tofauti na wangu lakini siuoni mfumo Kristo, nikimwangalia JK (Rais Jakaya Kikwete) na Makamu wake. Siuoni mfumo Kristo nikimwangalia wajina wangu Mohamedi Shein na Seif Shariff Hamad. Siuoni mfumo Kristo nikimwangalia Chande Othman, yule Jaji Mkuu na Othman Rashid, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Siuoni hata nikiungalia kwenye Wizara na Taasisi nyingine za Serikali.

 

Wanaoongea mfumo Kristo hawana uthibitisho wa kutosha kuhalalisha madai yao, ambayo kwa sasa nayaita hayana mashiko bali yametawaliwa na ukame wa maono na kiangazi cha fikra kinachopiga macho pazia mchana wa jua kali.

 

Kwa Waislamu na wasio Waislamu lazima tutambue kuwa adui wa Waislamu si Wakristo, wapagani, Wahindu au dini nyingine zinazopatikana kwenye huu ulimwengu.  Lazima tujue kuwa sisi ni ndugu tunaohitaji kuishi kwa upendo na kuvumiliana bila kuathiri imani zetu, na ikitokea lazima tutafute njia za amani kupata suluhu.

 

Kwa mtazamo wangu, hawa wafuatao hapa chini ndiyo maadui wakubwa wa Uislamu kwa Tanzania: Adui namba moja kwa Waislamu ni kutokuwa na shule na vyuo vingi vyenye kutoa elimu bora kwa vijana wa Kiislamu na hata wale wa upande wa pili wanaokuja kuitafuta elimu.

 

Najua kuna watu watapinga sana lakini ukweli mchungu lazima tuuseme ili tupate pa kuanzia. Mtakuwa mashahidi hata shule tulizonazo hazifanyi vizuri sana kwenye mitihani ya kitaifa, lakini pia hata shule zetu hazina mfumo wa kuandaa masheikh walioiva kwenye elimu dunia na akhera.

 

Mimi napendekeza harakati zetu ziwe kwenye kujenga shule za viwango pamoja na kuajiri walimu bora, bila kujali dini zao ili kuwaandaa vijana bora wanaoendana na kasi ya sayansi na teknolojia kuelekea soko la ajira ya ushindani na pia viongozi bora wa dini.

 

Pili, ni kukubali kufanya nyezo ya CCM kupata uhalali wa kuendelea kutawala milele! Mfano, suala la Mahakama ya Kadhi limebaki kitendawili! Tuunge mkono chama ambacho hakitatugawa na kuharibu umoja wetu wa kitaifa.

 

Tatu, BAKWATA (Baraza la Waislamu Tanzania) inamuweka inayemtaka. Lazima tupiganie BAKWATA iwe chombo huru cha Waislamu na tuwaweke viongozi wenye maono mapana tunaotaka sisi, hii itasaidia kurejesha imani kwa baraza hilo.

 

Napendekeza vigezo vya kuiongoza BAKWATA viwe ni kwa kiwango cha PhD kwa kuangalia uwezo wa elimu akhera na elimu dunia, lakini pia pamoja na uwezo wa kuongoza na kusimamia mambo. Chuo Kikuu cha MUM kinaweza kusaidia kuratibu kupatikana wataalamu na watendaji wengine wa BAKWATA ambao nao kiwango cha chini cha kuanzia kiwe shahada moja na kuendelea.

 

Nne, kutokufuata mafundisho ya Mtume. Mtume wetu Muhammad (SAW) alikuwa mwema, mwingi wa hekima na busara. Lazima tuyafuate mafundisho yake na kukumbushana mema na kukatazana mabaya.

 

Uislamu haujajengwa kwenye misingi ya uhasama, vurugu, fujo, chuki na mambo mengine mabaya. Uislamu umejengwa kwenye misingi ya usafi wa matendo mema, kumcha Mungu, ukarimu na kuhurumia na kuwajali wengine.

 

Tukiyafanya haya tutawaepuka wale wanaoutumia Uislamu wetu kama daraja ambalo baadaye hutuchafua wote. Mfano, wale walioingia kuchoma na kuvunja makanisa na kuiba sadaka, baadhi ya vifaa vya kanisa na mikate.

 

“Uislamu ni unadhifu.” Hii ni moja ya tafsiri ya hadithi za mtume wetu kipenzi Muhammad (SAW). Tuyafuate mafundisho yake kwa matendo ili tumuenzi kipenzi chetu.

 


1168 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!