CCM waache unafiki tozo ya kodi ya simu

Nianze kwa kuwashukuru wasomaji wa JAMHURI waliotumia muda na gharama kunipigia simu na kunitumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), kuelezea maoni na mitazamo yao kuhusu makala niliyoandika wiki iliyopita katika Safu hii, iliyokuwa na kichwa cha habari “Majeshi ya vyama vya siasa yafutwe”.

Leo ninakuleteeni mada inayohusu suala la tozo ya kodi ya laini au kadi za simu za kiganjani. Wengi wetu tumesikia na hata kulalamikia hatua hiyo iliyopitishwa na Bunge kabla ya kuidhinishwa na Serikali kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2013.

 

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita, chama tawala CCM kilikaririwa na vyombo vya habari kikiitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kutengua sheria hiyo.  Binafsi ninaichukulia kauli hiyo ya viongozi wa CCM kuwa ni ya kinafiki kwa sababu wameitangaza huku wakijua wazi kwamba sheria hiyo imefanikishwa na wabunge wanachama wa chama tawala.

 

Wengi wetu ni mashahidi wa mijadala ya bungeni. Tunaona na kusikia kuwa wabunge wanachama wa CCM ndiyo wanaowezesha kupita kwa miswada yote kutokana na wingi wao.

 

Muswada wa sheria ya kodi ya kadi za simu za mkononi ulijadiliwa kwa kina bungeni. Takribani wabunge wote wanachama wa vyama vya upinzani waliupinga wakiungwa mkono na wabunge wachache wanachama wa CCM, ingawa hatimaye wachache hao walizidiwa nguvu na idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala waliouunga mkono hadi kuupitisha.

 

Kwa mujibu wa sheria hiyo, sasa kila Mtanzania anayemiliki kadi ya simu ya kiganjani anapaswa kuilipia Sh 1,000 kwa mwezi. Chama cha Waendeshaji wa Simu za Kiganjani Tanzania (MOA) walikaririwa hivi karibuni wakisema hawakushirikishwa katika mchakato wa kupendekeza tozo hiyo.

 

Wiki iliyopita, Katibu Mwenezi wa CCM (Bara), Nape Nnauye alikaririwa na vyombo vya habari akisema “Kama chama tawala tunaona hatuwezi kukaa kimya kwa jambo ambalo linawabebewa wananchi nzigo.”

 

Leo tunapoona na kusikia kiongozi wa CCM akipinga sheria hiyo ni jambo lisiloingia akilini. Swali moja linatosha kujiuliza: kulikuwa na ugumu gani kwa viongozi hao wa chama tawala kujitokeza mapema kuwashauri wabunge wanaotokana na chama hicho kabla hawajapitisha muswada wa sheria hiyo?

 

Ni jambo lisiloingia katika akili za wengi kuwa huu ndiyo muda mwafaka kwa viongozi hao wa CCM kujitokeza kukataa tozo ya kodi ya simu za kiganjani. Huo ni unafiki tu! Ni kutaka kujivua lawama pasipowezekana.

 

Tayari Serikali kupitia Wizara ya Fedha imesisitiza kwamba itaendelea kusimamia utekelezaji wa tozo ya kadi za simu hizo, kwa kuwa ilipitishwa na wabunge wengi (wa CCM) kwa utaratibu unaokubalika kisheria.

 

“Tozo hii ipo kisheria,” amesisitiza Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, na kufafanua kuwa mchakato wa tozo hiyo umefuata utaratibu wa kisheria, hivyo hakuna anayeweza kuifuta kwani imependekezwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti na Serikali ikaona inatekelezeka.

 

Kwa ukweli usiopingika, tozo hiyo itachangia kuwakandamiza Watanzania wengi kiuchumi, na huenda baadhi wakaamua kujiengua katika matumizi ya simu za mkononi kutokana na uwezo duni wa kipato walionao. Ni dhahiri kuwa watakaojiondoa kwenye matumizi ya simu hizo watakosa wigo mpana wa kufanya mawasiliano katika juhudi za kujikwamua kiuchumi.

 

Kwa hivyo, chama tawala hakiwezi kukwepa lawama za kuwaongezea Watanzania kikwazo cha maendeleo yatakayowawezesha kuondokana na umaskini unaowakabili. CCM waache unafiki katika mzigo huu wa tozo ya kodi za kadi za simu za mkononi, wao ndiyo walioubariki kwa sababu wanazozijua wenyewe.

Please follow and like us:
Pin Share