ADDIS ABABA, ETHIOPIA

Imethibitishwa kuwa watu 4,867,727 walikuwa wameambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona (COVID-19) barani Afrika hadi kufikia katikati ya wiki iliyopita.

Taasisi ya kukabiliana na magonjwa barani Afrika iliyo chini ya Umoja wa Afrika (AU), Africa CDC, imesema kuwa hadi kipindi hicho jumla ya watu 131,441 walikuwa wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo, wakati wagonjwa 4,404,608 walikuwa wakipatiwa matibabu katika maeneo mbalimbali.

Africa CDC imezitaja Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, Ethiopia na Misri kama nchi ambazo zilikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi barani Afrika.

Eneo la kusini mwa Afrika ndilo limeathiriwa sana na maambukizi ya virusi hivyo likifuatiwa na kaskazini na mashariki mwa Afrika. Eneo la kati ya Afrika ndilo ambalo linaonekana kuwa na nafuu, kwa mujibu wa Africa CDC.

Wakati huo huo, Marekani imetangaza mpango wake wa kusafirisha chanjo nje ya nchi hiyo kwa mara ya kwanza.

Alhamisi iliyopita Marekani ilisema ina mpango wa kusafirisha nje ya nchi dozi milioni 25 za chanjo za COVID-19 katika mpango wake wa kusafirisha nje ya nchi dozi milioni 80 hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Takriban asilimia 75 ya chanjo hizo zitatolewa kama msaada kwa shirika linaloshughulikia masuala ya chanjo duniani lijulikanalo kama Covid-19 Vaccines Global Access (COVAX).

Asilimia 25 ya dozi hizo zitatolewa moja kwa moja kwa baadhi ya nchi zenye mahitaji, Ikulu ya Marekani imesema.

“Tunatoa msaada huu si kwa lengo la kupata upendeleo maalumu. Tunatoa dozi hizi ili kunusuru maisha ya watu na kuunga mkono jitihada za dunia kutokomeza janga hili,” anasema Rais Joe Biden katika taarifa ya maandishi.

Dozi milioni 19 katika sehemu ya kwanza ya dozi milioni 25 zitatolewa kupitia COVAX.

Takriban dozi milioni sita zitapelekwa Marekani ya Kusini na Kati;  katika nchi za Brazil, Argentina, Colombia, Costa Rica, Peru, Ecuador, Paraguay, Bolivia, Guatemala, El Salvador, Honduras, Panama, Haiti na nchi nyingi za Caribbean, pamoja na Dominican Republic.

Dozi milioni saba zitapelekwa barani Asia katika nchi za India, Nepal, Bangladesh, Pakistan, Sri Lanka, Afghanistan, Maldives, Malaysia, Philippines, Vietnam, Indonesia, Thailand, Laos, Papua New Guinea, Taiwan na visiwa vya Bahari ya Pacific. 


Wataalamu wa afya wakiwa wanasubiri kupatiwa dozi za dawa kwa ajili ya kuwachanja watu.

By Jamhuri