CAIRO, MISRI

Mipango imeanza kuupanua Mfereji wa Suez nchini Misri kama njia ya kuhakikisha usalama na ufanisi wa usafirishaji, hasa kwa njia ya meli.

Machi mwaka huu biashara duniani iliingia kwenye mtanziko mkubwa baada ya meli moja kubwa ya mizigo kukwama ikiwa katikati ya mfereji huo mwembamba.

Meli hiyo iitwayo Ever Given, ambayo ni ndefu karibu sawa na jengo refu nchini Marekani la Empire State, ilikwamuliwa baada ya siku sita.

Ingawa siku hizo zinaonekana kuwa chache, lakini katika eneo hilo zilikuwa ni nyingi, kwa sababu katika kipindi hicho hakuna meli iliyokatiza kati ya Ulaya, Afrika, Asia na Mashariki ya Mbali.

Meli nyingi zililazimika aidha kusubiri au kuzunguka Afrika Kusini ambako safari inaongezeka kwa takriban wiki tatu.

Katika jitihada za kuzuia jambo kama hilo kutokea tena, mipango imeanza kuupanua mfereji huo muhimu kwa biashara.

Mamlaka ya Mfereji wa Suez (SCA) ilitangaza katikati ya mwezi uliopita kuwa imeanza kuchimba pembezoni mwa mfereji huo ili kuongeza upana wake, hasa upande wa kusini, ambako meli ya Ever Given ilikwama.

Eneo hilo lenye urefu wa kilometa 30 litapanuliwa kwa meta 40 (futi 131) kwa kina kuongezwa hadi futi 72 kutoka futi 66 za sasa, kwa mujibu wa SCA. 

Mipango hiyo pia itahusisha ujenzi wa njia ya pili karibu na Ziwa Great Bitter, ambayo ilifunguliwa mwaka 2015. Njia hiyo itaongezwa kwa kilometa 10 (maili sita) ili kuruhusu meli mbili kupishana katika kipande cha kilometa 82 (maili 51).

Kazi hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa mfereji huo na kupunguza muda wa meli kuvuka eneo hilo, pia kuongeza usalama majini.

Hata hivyo, bado kuna maswali iwapo mipango hiyo itaweza kuzuia tukio la meli kukwama katika siku za usoni.

“Kupanua mfereji ni wazo zuri. Lakini swali ni je, iwapo mfereji utapanuliwa, watengenezaji meli nao hawatatengeneza meli kubwa zaidi?” anahoji Sal Mercogliano, mtaalamu wa masuala ya usafiri wa majini anayefanya kazi katika Chuo Kikuu cha North Carolina.

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, uwezo wa meli kubwa kubeba makasha umeongezeka kwa asilimia 1,500 na kuongezeka maradufu katika muongo mmoja uliopita, kwa mujibu wa Kampuni ya bima za meli, Allianz Global Corporate and Speciality.

Meli kubwa za mizigo hivi sasa zina uwezo wa kubeba hadi makasha 24,000 zikiwa na upana wa futi 200. Meli ya Ever Given, ambayo ina uwezo wa kubeba makasha hadi 20,000 ilikuwa imebeba makasha 18,000 wakati ilipokwama, ikiwa na urefu wa meta 400 (futi 1,312) na upana wa meta 59 (futi 194).

Meli ndogo (kulia) ikiivuta meli kubwa ya Ever Given (kulia) ambayo ilikwama katikati ya Mfereji wa Suez na kuzuia meli nyingine kupita.

By Jamhuri