Kumeibuka mgogoro wa ardhi, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara kati ya uongozi wa wilaya hiyo na wakazi wa Kijiji cha Bisarwi, kudai kuwa wanataka kupokonywa mashamba yao na kupewa mwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa na kujenga kiwanda cha sukari.
Mashamba hayo yaliyopo katika Bonde la Mto Mara, yanadaiwa na wananchi  hususani wa vitongoji vya Kwikoma na Makora walio kati ya 150 na 200, wanadai kuwa uongozi wa wilaya umeazimia kuwapokonya mashamba hayo yenye ukubwa unaokadiriwa kuwa hekari 300.
Baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo wamezungumza na JAMHURI na kuelezea hisia zao juu ya kitendo hicho, ambacho wao wanakiita kuwa ni ‘dhuluma wanayofanyiwa na uongozi wa Wilaya ya Tarime’.


Akizungumza na JAMHURI, David Mgesi, mwenyeji wa Kijiji cha Bisarwi, amesema kuwa hadi sasa maofisa ardhi wa Wilya ya Tarime wamekwishapima maeneo yote na wameweka bikoni maeneo yote wanayoyahitaji.
“Hakuna aliyeshirikishwa kwenye hili suala. Sisi wananchi hatuna shida na uwepo wa kiwanda hicho kwa sababu ndiyo maendeleo, lakini sisi wamiliki wa ardhi mbona hatuulizwi? Sisi wenye maeneo hatuko tayari kuuza au kufidiwa maeneo yetu, kama ni suala la kilimo kwa nini hawa wawekezaji wasiingie ubia nasi wa ardhi hii?” amehoji Mgesi.


“Waananchi tunataka ardhi yetu tubaki nayo na kama ni kulima miwa hata sisi tunaweza kulima kwani kiwanda kitahitaji pia kununua kutoka kwa wakulima. Na kuhusu eneo la kujenga kiwanda siyo tatizo ila mashamba yetu yasihusishwe. Ni afadhali watu wahamishwe kwenye maeneo wanayoishi wasogee sehamu nyingine kiwanda kijengwe ili mashamba ya watu yabaki kama yalivyo,” amesema Mgesi.


Amesema kuwa kuhusu mashamba, mamlaka ya kijiji haihusiki kwa sababu hayo ni mashamba ya watu binafsi.


Mgesi amesema kuwa viongozi wa vijiji walishiriki kuandika majina ya wamiliki wa mashamba wanaokadiriwa kuwa kati ya 150 na 200, ambapo majina hayo yalitumika kuwalazimisha wananchi kusaini kuwa wameridhia mashamba yao kuchukuliwa na mwekezaji.
“Februari 7, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya alikuja na Polisi na kulazimisha wananchi kusaini kuwa wamekubali maeneo yao yachukuliwe na mwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa na kiwanda,” amesema Mgesi.
“Kuna upotoshaji unaofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime na watu wanaojiita viongozi wa jadi, kuwa mashamba haya yamekuwa yakitumika kwa kilimo cha bangi, hivyo ni lazima yachukuliwe ili kutokomeza kilimo hicho. Siyo kweli; Mkuu wa Wilaya anapotosha, sisi hapa tunalima mahindi na mtama pamoja na shughuli za uvuvi,” amesema Mgesi.


“Upotoshaji mwingine ni kwamba haya ni mashamba pori, tunamuomba Waziri wa Ardhi aje aone kama haya ni mashamba pori kweli. Haya ni mashamba yetu na hata makaburi ya babu zetu yapo kwenye mashamba haya,” amesema Mgesi.
Bonde la Mto Mara lina urefu wa kilomita 70 likijumuisha kata kama tano na vijiji kadhaa. Hili bonde wananchi wamekuwa wakilitumia kwa shughuli za kilimo na uvuvi kutokana na uwepo wa mto huu. Bonde hili lina ukubwa wa hekari 11,000.
JAMHURI limezungumza na Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Murimi Zabloni, ambaye amesema hadi sasa yeye hajui hata jina la hiyo kampuni inayohitaji mashamba hayo ya wananchi kwa ajili ya kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda. Amesema kuwa anachofahamu ni kuwa kampuni hiyo ni ya Wahindi kutoka Uganda.


“Januari 31 mwaka huu, tulikutana kwenye kikao cha pembejeo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, mbunge ni mjumbe kwenye kile kikao ila mimi nilikwenda kumuwakilisha. Mimi nilitumia fursa hiyo kumueleza DC tatizo hilo la wananchi kutaka kuporwa mashamba yao akasema hakuna mtu atakayeporwa.”
“Mimi nikamwambia kuwa basi nitakwenda kuwaeleza wananchi taarifa hii nikiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri. Hivyo, Februari 2, tukaenda kukutana na wananchi, tulipomaliza kikao tu difenda ikaingia,tunaambiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya kuwa tumefanya mkutano wa kuzuia kiwanda tena bila kibali.
“Tukasema mkutano huu ni wa kuwaeleza yale Mkuu wa Wilaya aliyotuambia kuwa wasiwe na wasiwasi. Mkuu wa Upelelezi akasema Mkuu wa Wilaya ameagiza tuwekwe ndani. Kwa hiyo, wakatukamata na kutuweka mahabusu kwa siku saba,” amesema Zabloni.
Amesema jumla walikamatwa watu wanne ambao ni yeye, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Moses Misiwa, pamoja na wanakijiji wawili – Marwa Kisamure (67) na Mwinyi Marwa.
“Februari mwaka huu, kupitia Ofisi ya Mbunge nilimwandikia Mkuu wa Wilaya barua  nikimweleza kwamba mbunge anataka kuanza ziara jimboni, lakini kabla hajaanza anaomba ukutane naye ili mzungumzie hali iliyojitokeza kwa wananchi wa vitongoji vya Kwikoma na Makora, nasikitika Mkuu wa Wilaya hakujibu. Kwa hiyo, tulianza ziara Machi 2 bila mawasiliano na DC,” amesema Zabloni.


JAMHURI limezungumza na Mwinyi Marwa ambaye amekiri kukamatwa na kuwekwa sero kwa siku saba. Amesema kosa lililofanya akamatwe ni kuhoji juu ya uhalali wa kuchukuliwa kwa eneo aliloririthi kwa baba yake, lenye ukubwa wa hekari tisa bila kushirikishwa wala kuridhia.
“Nimepata taarifa kuwa uongozi wa kijiji unaunda mpango wa kunibambika kesi ili nifungwe. Kesi ninayoundiwa ni kwamba ninamiliki muhuri wa mwenyekiti wa kitongoji cha Makora kinyume cha sheria, jambo ambalo sijawahi kuwa hata mjumbe wa nyumba kumi,” amesema Marwa.
Vyanzo vyetu vimelieleza JAMHURI  kuwa Mei 3, mwaka huu wananchi wa kijiji cha Matongo walifunga Ofisi ya Kijiji hicho wakidai hawajashirikishwa na hawajui kinachoendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, ameliambia JAMHURI kuwa hawezi kuzungumza ili kupata ukweli na uhakika wa tuhuma hizi zinazoelekezwa kwake. Alikataa kwa kusema kuwa hawezi kuzungumza.
“Hayo mambo siwezi kuzungumza na vyombo vya habari,” amesema Luoga na kukata simu.


Range Wantari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bisarwi, alipoulizwa kuhusiana na kuandika orodha ya majina ya wananchi bila kuwahusisha ikiwamo kuongeza majina yasiyo ya wakazi wa vitongoji vya Kwikoma na Makora na kwamba hawamiliki mashamba katika vitongoji hivyo.
Amesema kuwa wananchi wameelezwa habari za kuchukuliwa kwa mashamba hayo katika mkutano maalumu uliofanyika wiki iliyopita.
Kuhusu majina yasiyo ya wakazi wala wamiliki wa mashamba hayo kuwekwa kwenye orodha ya wamiliki na kuwasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, amesema kuwa suala hilo siyo la kweli na wala haliwezi kuthibitishwa na walalamikaji kwa kuwa yeye ndiye anayefahamu vizuri watu anaowaongoza.
Alipoulizwa kuwa ni kwanini taarifa imetolewa baada ya maeneo kupimwa na kuwekewa bikoni, alijibu kuwa ndivyo utaratibu ulivyotakiwa kuwa.


JAMHURI limezungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Cliford Tandali, juu ya mgogoro huo ambapo ameelezea namna anavyoushughulikia.
“Mwezi Aprili mwaka huu, nilikutana mjini Dodoma na uongozi wa Wilaya ya Tarime na baadhi ya wajumbe wa halmashauri, ambapo tulifikia azimio la kwamba suala hili likajadiliwe upya katika ngazi ya halmashauri kwa sababu limeonekana kupelekwa haraka haraka,” amesema Tandali.
“Sisi kama TIC kabla hatujafanya uamuzi wa kuingia mkataba na mwekezaji, ni lazima tujiridhishe kwa utafiti wetu na kwa kushirikisha maoni ya baraza la madiwani. Tukiona kuna mvutano ni vema ukatatuliwa kwanza maana lengo ni kuijenga Tanzania,”amesema Tandali.
Amesema kuwa bado TIC inasubiri mrejesho kutoka kwa baraza la madiwa juu ya kasoro zilizojitokeza ikiwamo wananchi kudai kutoshirikishwa.


Wakati Tandali akisema hayo, Katibu wa mbunge jimbo la Tarime Vijijini, Murimi Zabloni, amelieza JAMHURI kwamba Mei 9, mwaka huu madiwani wa Halmashauri ya Mji na wa Halmashauri ya Wilaya wamekwenda Dodoma kujadili suala hili kwa udhamini wa mwekezaji anayelihitaji eneo hilo.
“Yale tuliyokubaliana na Mkurugenzi wa TIC hatujayatekeleza, halafu wenzetu wameamua kwenda kujadili suala hili kwa siri Dodoma kwa ufadhili wa mwekezaji. Madiwani wa mji hawawakilishi watu wanaoguswa na suala hili ila wamejumuishwa,”a mesema Zabloni.
“Wameondoka ujumbe wa watu takribani hamsini. Taarifa nilizonazo ni kwamba wamekwenda kulazimisha kulimaliza suala hili kibabe. Wananchi hawatakubali. Sisi bado tunasimamia makubaliano kati yetu na Mkurugenzi wa TIC,” amesema Zabloni.
Amesema ujumbe huo umekwenda kumuona Waziri wa Tamisemi.


“Mimi nimeona kwenye vyombo vya habari, Waziri akimuagiza Mkurugenzi achukue hatua kwa sababu anazosema baraza la madiwani linachelewesha mradi. Madiwani walikubaliana tarehe 3 mwezi huu kwa kupiga kura juu ya utatuzi wa suala hili. Nashangaa madiwani wa CCM wamejitenga na kwenda kumuona Waziri. Sisi tutawaeleza wananchi,” amesema Zabloni.
Sore Makori, mkazi wa Kitongoji cha Makora, anayemiliki hekari 3.5 katika Bonde la Mto Mara, amesema kuwa Polisi walikuja kitongojini hapo mwezi Februari kuwatisha na kuwalazimisha kusaini kuridhia mashamba yao kuchukuliwa na kisha orodha ile ya majina kupelekwa kwa mwekezaji.
“Sisi mwekezaji tunamuhitaji sana, hatukatai wala hatupingi ila tunachokikataa ni kulazimishwa kulipwa fidia ya maeneo yetu. Tunachohitaji sisi ni kuingia ubia na mwekezaji wa kutumia mashamba yetu kwa kilimo cha miwa,” amesema Makori.

1442 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!