Wao na mashangingi, masikini na sakafu

Rais Paul Kagame wa Rwanda alipotwaa madaraka, miongoni mwa “uamuzi mgumu” wa awali aliouchukua ni kuhakikisha anapunguza matumizi yanayosababishwa na magari ya umma. Akayakusanya kwa wingi. Akayaweka uwanjani. Akapewa orodha ya maofisa na watumishi wanaostahili kukopeshwa magari. Akawaagiza waende uwanjani- kila mmoja achague analotaka. Akahakikisha aliyechagua gari anakopeshwa-linakuwa mali yake. Huduma za mafuta na matengenezo zikaandaliwa utaratibu kwa kila gari na kwa muda maalumu.

Magari machache yaliyobaki yakawekwa kwenye “pool”. Waziri, mkurugenzi na mkubwa yeyote awaye, akitaka kusafiri, anapata gari kutoka kwenye “pool”. Kwa mbinu hiyo, Rwanda ikajivua gharama kubwa za kuhudumia magari ya umma. Ikaokoa mabilioni ya fedha. Juzi, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, kupitia Kamati yake, amewasaidia Watanzania kurejea kilio cha matumizi makubwa mno yanayofanywa na watumishi wa umma kupitia magari ya Serikali.


Chenge akinukuu taarifa ya Kamati yake, akasema, “Kwa miaka mitatu mfululizo, gharama za ununuzi wa mafuta na matengenezo ya magari zilikuwa kama ifuatavyo; mwaka 2008/2010 Sh bilioni 685; mwaka 2009/2010 Sh bilionbi 530; na mwaka 2010/2011 Sh bilioni 537. Kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011 gharama hizi zilikuwa sawa na asilimia 4.6 ya bajeti yote ya Serikali. Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miaka mitatu (2008-2011) Sh trilioni 1.8 zilitumika kuhudumia magari ya Serikali pekee…Kiasi hiki hakijumuishi gharama za ununuzi wa magari hayo.”


Chenge akaongeza kuwa katika Afrika Mashariki , Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kutokusanya mapato, lakini pia ndiyo inayoongoza kwa kutumia kiasi kikubwa cha gharama zikiwianishwa na pato la Taifa!

Ndugu zangu, matumizi haya ya fedha za umma, yakijumuishwa na gharama za ununuzi wa magari pamoja na posho za madereva; ni miongoni mwa mambo yanayoliumiza mno Taifa letu.


Tumeshuhudia mameya wa miji, manispaa na majiji wakijinunulia magari ya thamani kwa kigezo tu kwamba mapato ya halmashauri “zao” yanaruhusu. Ni Tanzania pekee ambayo mtoa msaada (Balozi wa Japan ) anakwenda kwenye shughuli ya kukabidhi kisima cha maji akitumia Land Cruiser GX, na kupokewa na Mtendaji wa Halmashauri akiwa na Land Cruiser VX V8. Huu ni ujuha.


Magari ya umma yanatumiwa kusomba majani ya ng’ombe. Ndiyo yanayobeba mkaa. Yanatumiwa na wakubwa kwenda na kutoka sehemu za starehe usiku wa manane. Yanatumiwa kwenye shughuli za kipaimara, ubatizo, kitchen party, mazishi ya marafiki, na kadhalika.


Barabara zote za Tanzania zinafunikwa na kupambwa na ma-STG, STH, STK, SM, ST, DFP, na mengine yasiyotaka kujulikana. Ukifika bungeni utadhani ni uawanja wa maonyesha na mashindano ya nani mwenye gari ghali zaidi!

Haya yanafanyika ilhali maelfu kwa maelfu ya kina mama na watoto wakikosa japo vitanda tu ndani ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu. Hospitali zimebaki kuwa vituo vya kupokea ushauri kutoka kwa madaktari! Hakuna dawa. Hakuna huduma.


Maelfu kwa maelfu ya watoto wa Tanzania wanasoma wakiwa wameketi, ama chini katika sakafu zisizosakafiwa, wakiwa wanasoma madarasa mawili ndani ya chumba kimoja, au wakiwa wanasomea chini ya miti. Haya yanafanyika huku wakubwa wakijichagulia magari ya thamani. India yenye ukwasi wa hali ya juu, hakuna kiongozi anayetumia gari la Sh milioni 200. Sisi tunaotembeza bakuri, huwezi kutofautisha gari analotumia rais, waziri, naibu waziri, mkuu wa mkoa, kamanda wa polisi wa mkoa wala mesenja. Kamanda wa Polisi wa Mkoa anapewa Land Cruiser VX V8 ilhali polisi wa kawaida wakishindwa kufika kwenye matukio kwa kukosa mafuta kwenye pikipiki zao! Kama kweli tumedhamiria kupata maendeleo, moja ya maeneo yanayopaswa kudhibitiwa ni hili la magari ya umma.


Kila nikitazama sioni kama kweli Awamu ya Nne inaweza kurekebisha dosari hii kwa muda uliosalia. Pengine huu uwe mkakati wa awali kabisa kwa Serikali ijayo ya Awamu ya Tano. Hizi mbinu za kina Mzee Pinda za “kutakaa” mashangingi, huku walio chini yao wakiyanunua, ni danganya toto. Ni kuwapumbaza Watanzania. Tena basi, yale magari aina ya RAV4 waliyotudaganya kwamba watayanunua, wapo waliokwenda kiwandani kuwanga! Sasa nasikia kiwanda kimeacha kuyatengeneza ili tuendelee kununua mashangingi ya Sh milioni 200!


Ukiitazama picha hii niliyoiambatanisha hapa, ndipo unapoweza kujiuliza, “Kama Hospitali ya Temeke inaweza kuwa kwenye hali hii ya kina mama kubanana kama nguchiro shimoni, hali ikoje kwa ndugu zetu wa Kakonko, Mabui Melafuru, Kasesya, Tandahimba, Rwabununka au Kintinku?” Nikitafakari hili la magari ya umma, namwona Rais Kagame kama mmoja wa viongozi bora kabisa katika Afrika.