Wiki iliyopita niliandika sehemu ya kwanza ya waraka huu. Pamoja na mambo mengine, nilichambua kwa kina sababu moja kati ya tatu zilizonisukuma kuwaandikia waraka huu.

Kabla sijaendelea na sababu ya pili na tatu; leo nachambua kitu muhimu katika harakati za kujikwamua kiuchumi. Kitu hiki ni nguvu ya mtazamo wa mfanyakazi katika eneo la mafanikio.


Nitoe kisa kutoka katika Biblia. Historia ya Wana wa Israeli inaonesha kuwa kuna wakati wakiwa utumwani Misri, kulitokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Farao aliyekuwa anawatetea kufariki. Farao ‘mpya’ alikuwa ni mkorofi na aliwatesa kutokana na kuwapa kazi ya kufyatua matofali ya kujenga mapiramidi yote yanayoonekana pale Misri hadi leo.


Enzi hizo za mateso, akatokea Nabii Musa ambaye alitumwa na Mungu kuwaokoa ili awapeleke Kaanani. Harakati za Nabii Musa zilimwongezea chuki Farao dhidi ya Waisrael na akaapa kuongeza mateso. Awali walikuwa wakifyatua matofali kwa kutumia majani (kata) yaliyokuwa yanaandaliwa na wasimamizi wao (wawakilishi wa Farao).


Baada ya hasira ya Farao kuwaka, akaamuru mambo mawili; mosi, Waisraeli wasiandaliwe tena majani ya kufyatulia matofali; pili, kila Mwisraeli aongezewe maradufu idadi ya matofali aliyokuwa akifyatua awali wakati akipewa majani. Huu ulikuwa wakati mgumu kwao hasa ikizingatiwa kuwa tangu wazaliwe walijua ‘haiwezekani kufyatua matofali bila kutumia majani (kata)’.


Lakini kutokana na adhabu na mateso ya Farao, Waisraeli walitafuta mbadala na kujikuta wakiendelea na kazi ya kufyatua matofali tena kwa idadi mpya waliyopangiwa. Kilichowasukuma hadi kutafuta mbadala ni adhabu na mateso waliyokuwa wakiyapata inapotokea wameshindwa kutekeleza ufyatuaji wa matofali.


Kutoka katika kisa hicho, kuna mambo matatu tunayoyapata. Mosi, ili mtu upambane kupata kitu inategemea na nguvu iliyopo nyuma yake inayokusukuma atafute kitu hicho. Pili, utegemezi unapoondoka akili huwa inakusanya uwezo ambao haujatumika, kuhakikisha kuwa unaanza kujitegemea. Tatu; ‘nguvu ya asili’ (Mungu) huwa inafanya kazi na watu wanaopanga, kufikiri na kujishughulisha.


Nianze na nguvu inayokuwapo nyuma ya mtu kutafuta kitu fulani, ambapo kwa hapa tunaongelea kutafuta mafanikio ya kiuchumi. Kuna nguvu mbili zinazoweza kumsukuma mtu kutafuta mafanikio. Ya kwanza ni ile ambayo kwa Kiingereza inaitwa ‘push power’; na ya pili ni ile inayoitwa ‘pull power’.

 

Katika nguvu ya kwanza unasukumwa kuondoka katika mazingira duni, wakati ile ya pili inakuvuta kuingia katika mazingira bora zaidi hata kama hupo katika hali mbaya sana kimaisha. Iko hivi, unaweza kuzaliwa katika mazingira ya umaskini wa kutupwa na ukawa unakutesa na kukuumiza kichwa. Unapojaribu kutoka katika lindi la umaskini unakuwa ukitumia nguvu ya ‘push power’.

 

Lakini unaweza ukawa umezaliwa kwenye mazingira ya kimaskini, ya kawaida ama ya kitajiri isipokuwa ukatamani kufanikiwa na kufikia hatua fulani ya kibiashara ama ya kimaisha. Kitendo cha kuvutwa na mafanikio yaliyopo mbele yako ndio tunakiita ‘pull power’.

 

Kuna utafiti nimewahi kuusoma unaoeleza nadharia ya watu wa kabila la Wakinga na Wachagga walivyofanikiwa katika ujasiriamali. Utafiti huu ulieleza kuwa Wakinga wamekuwa wakifanikiwa kibiashara kwa kutokana na ‘push power’ wakati Wachagga wanafanikiwa kutokana na ‘pull power’.

 

Inapotokea ndani yako ukawa na moja kati ya hizi nguvu mbili kwa kiwango kikubwa na cha kutosha, ni rahisi na tena inawezekana ukapata upenyo wa kuzalisha fedha ama kupata mafanikio pasipokuwa na fedha. Kwa bahati nzuri, nguvu hizi hazitokei kwa bahati mbaya isipokuwa huamuriwa na mhusika mwenyewe.

 

Kadiri unavyouchukia umaskini ulionao unajenga nguvu ya kukutoa hapo. Kadiri unavyojenga hamasa ya kupata fedha ama mafanikio makubwa ndivyo nguvu ya kukufikisha huko inavyojengeka ndani yako. Ukijua unapoelekea ni rahisi kutafuta njia ya kukufikisha huko.

 

Katika haya maisha, yapo mambo unayoweza kuyatumia kama bidhaa ya kubadilishana fedha. Mambo haya yanajumuisha uhusiano mwema na watu, taarifa sahihi, utu wema, umaarufu, uaminifu unaotambulika na watu, uwezo wako kiakili na mengine yanayofanana na hayo.

 

Hata hivyo, lazima ijulikane kuwa suala la kupata mafanikio (katika fedha na maeneo mengine), linahitaji uwekezaji endelevu wa mwenendo wa maisha ya kawaida. Haiwezekani uwe unaishi maisha ya ovyo, kama ufujaji wa fedha halafu utegemee watu wakuamini katika fedha na kukupa mtaji.


Huwezi kuwa mvivu wa kutafuta taarifa (kujisomea, kubadilishana mawazo, n.k) halafu utegemee kupata ‘deals’ za fedha. Vile vile unatakiwa kuwa makini sana na aina ya watu unaohusiana ama kuwasiliana nao. Haiwezekani uwe unafanya mawasiliano ya ‘ovyo’ kwa asilimia 100 kwa kutumia simu ama mtandao wa kompyuta halafu utegemee kukutana na watu wa maana (potential people).


Vile vile katika kutafuta mafanikio ni muhimu mtu kuachana na visingizio, kwa sababu visingizio ni matokeo ya kukata tamaa hata kama mhusika hujitambui.


Kila mtu mahali alipo ana fursa fulani ambayo bado hajaitumia, inayoweza kumwezesha kupata mafaniko zaidi ya aliyonayo. Si lazima mafanikio hayo uyaone kwa macho, na si lazima uyakamate siku hiyo hiyo; lakini unaweza kuibua mazingira ama mawazo yatakayokuwezesha kupata mafanikio.

 

Kama ilivyokuwa katika kisa cha wana wa Israeli; ndivyo ilivyo kwa wafanyakazi wengi. Mishahara ni midogo, fedha inapoteza thamani kwa kasi na wakati huo huo matumizi ya kimaisha ni makubwa. Maadamu mfanyakazi ungali unaishi, unalazimika kulipa kodi ya nyumba, unatakiwa kula, ada za watoto zinakusubiri achilia mbali ushiriki wako katika shughuli za kijamii kama misiba, harusi na nyinginezo.

 

Hata ukibaki kulalamika, haikusaidii! Kwa sababu, kwa kulalamika haimaanishi maisha yatakuhurumia! Ninapotaja suala la ujasiriamali, wafanyakazi wengi watasema, “Hatuna mitaji”, hivyo haiwezekani kuanzisha miradi ama biashara. Imani kama hiyo ilikuwapo pia kwa Waisraeli pale walipojisemea haiwezekani kufyatua matofali pasipo kuwa na kata.

 

Lakini mbinyo wa mateso ya Farao uliwatia adabu na wakalazimika kujifunza mbinu mpya za kutumia walichonacho kufyatua hayo matofali. Vivyo hivyo kwa wafanyakazi; bila kujali imani yako kuhusu ‘kutowezekana ujasiriamali pasipo mtaji’ ni kubwa kiasi gani.


Lakini kwa mibinyo ya ugumu wa maisha inayokukabili; kwa nini usikubali kutafuta na kujaribu mbinu mpya za kujikwamua kiuchumi? Hapo juu nimetaja nguvu za ‘push power’ na ‘pull power’; naamini wafanyakazi mnaweza kuzitumia zote mbili na zikaleta tija kubwa mno kwenu kiuchumi.

 

Badala ya kusema haiwezekani kujiajiri kutokana na kukosa mitaji, inatakiwa kutumia sababu hii, ‘ya kuondoka utegemezi’ (kulikosababishwa na mishahara isiyotosha) kwa ajili ya kutumia sehemu ya akili ambayo bado haijatumika. Hapa mfanyakazi unalazimika kutumia mshahara kidogo unaoupata kwa kudunduliza.


Hili litakusaidia kupata mtaji wa mradi au biashara itakayokuwa inakuongezea kipato kuliko kuishi kwa kutegemea mshahara pekee. Wafanyakazi wengi mtakubaliana nami kuwa siku hizi mishahara pekee haitoshelezi kutegemewa katika kukupatia uhuru wa kifedha na kiuchumi. Na kama ukisema usubiri ‘mamilioni’ ndipo uanzishe mradi ama biashara utajikuta si tu unakufa maskini, bali pia unaishi maisha ya mateso mno!


Mwisho ni ‘nguvu ya asili’ (Mungu) inavyosaidia wale wanaowaza, kujaribu na kujituma. Kuna uthibitisho wa kiutafiti na kishuhuda unaoonesha kuwa ‘nguvu ya asili’ huleta usaidizi na mtu unajikuta umepata ama umefanikisha malengo kwa namna ya kipekee. Baadhi ya wanasaikolojia wameeleza dhana hii kama, ‘Law of attraction’.


Nihitimishe sehemu hii kwa kuwatia moyo wafanyakazi kuwa inawezekana kupata mafanikio uyapendayo ikiwa utakuwa na mtazamo sahihi kuhusu mafanikio. Tuonane wakati mwingine katika sehemu ya tatu ya waraka huu.

stepwiseexpert@gmail.com, 0719 127 901


1185 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!